Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Theluthi mbili ya watoto Sudan Kusini wanahitaji msaada wa kibinadamu- UNICEF 

Watoto wakinywa uji uliopikwa na mama yao baada ya kupokea mgao kutoka kwa WFP, Pibor nchini Sudan Kusini.
WFP/Marwa Awad
Watoto wakinywa uji uliopikwa na mama yao baada ya kupokea mgao kutoka kwa WFP, Pibor nchini Sudan Kusini.

Theluthi mbili ya watoto Sudan Kusini wanahitaji msaada wa kibinadamu- UNICEF 

Msaada wa Kibinadamu

Kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya uhuru wa Sudan Kusini tarehe 9 mwezi huu wa Julai, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeonya kuwa watoto milioni 4.5 nchini humo wanahitaji msaada wa kibinadamu, ikiwa ni sawa na watoto wawili katika kila watoto watatu.  

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo katika miji ya New York, Marekani, Nairobi, Kenya na Juba, Sudan Kusini inasema takwimu hizo zinadhihirisha kuwa matumaini ya kwamba uhuru wa nchi hiyo ungalileta nuru mpya kwa watoto yametoweka. 

“Ghasia na mizozo, mafuriko, ukame na hali mbayá za hewa zinazochochewa na mabadiliko ya tabianchi na janga la kiuchumi vimesababisha ongezeko la ukosefu wa uhakika wa chakula na kufanya Sudan Kusini kuwa miongoni mwa nchi zenye majanga makubwa zaidi ya kibinadamu,” imesema ripoti hiyo iliyotathmini madhara ya janga la kibinadamu kwa watoto. 

Kama hiyo haitoshi, hata mkataba wa hivi karibuni wa amani ambao umetekelezwa kwa kiasi kidogo, nao pia umeshindwa kuwa tiba kwa changamoto zinazokabili watoto na vijana Sudan Kusini. 

“Matumaini ambayo watoto na familia zilipata wakati wa uhuru wa nchi hiyo mwaka 2011 yamegeuka kuwa kukata tamaa na ukosefu wa matumaini kabisa,” amesema Henrietta Fore Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF akiongeza kuwa utoto wa idadi kubwa ya watoto wenye umri wa miaka 10 nchini Sudan Kusini hii leo umegubikwa na ghasia, majanga na ukiukwaji wa haki. 

Kiwango cha vifo vya watoto wachanga kiko juu ambapo mtoto 1 kati ya 10 hatarajiwi kufikisha umri wa miaka mitano. 

Watu milioni 8.3 Sudan Kusini wanahitaji misaada ya kibinadamu, kiwango ambacho ni cha juu kuliko ilivyokuwa wakati wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati yam waka 2013 hadi 2018. 

Watoto milioni 1.4 wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo uliokithiri au unyafuzi mwaka huu pekee, idadi ambayo ni kubwa tangu mwaka 2013. Elimu nayo imekuwa ni mkwamo kwa watoto ambapo watoto milioni 2.8 hawako shuleni huku janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 lilisababisha shule kufungwa kwa miezi 14 na hivyo watoto wengine milioni 2 kushindwa kwenda shuleni. 

Hata hivyo licha ya ukosefu wa usalama, UNICEF imeendelea kushirikiana na wadau kuongeza uwezo wa kupima na kutibu watoto wenye utapiamlo na kuhakikisha kuna huduma za majisafi na salama pamoja na huduma za kujisafi. 

Changamoto inasalia kuwa ni fedha ambapo UNICEF inasema ili iweze kuendeleza huduma zake inahitaji kuchangiwa ombi lake la dola milioni 180, ombi ambalo hadi sasa limechangiwa kwa theluthi moja pekee.