Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twatamani kurejea nyumbani lakini hali ni muhali- Wakimbizi Chad

Watoto wakimbizi wakicheza katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Fourkoloum magharibi mwa nchi hiyo.
UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakimbizi wakicheza katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Fourkoloum magharibi mwa nchi hiyo.

Twatamani kurejea nyumbani lakini hali ni muhali- Wakimbizi Chad

Wahamiaji na Wakimbizi

Miaka kadhaa baada ya kukimbia vijiji vyao nchini Chad kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na vikundi vilivyojihami maelfu ya wakimbizi wa ndani na wakimbizi kutoka nchi jirani bado wanashindwa kurejea makwao na wanajaribu kujenga maisha yao katika jamii zilizowakaribisha nchini humo.

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR inamuonesha Alimi Abali baba mwenye umri wa miaka 52 mkimbizi wa ndani nchini Chad ambaye kwa sasa yeye, wake zake watatu pamoja na watoto 11 wanaishi katika kambi ya Forkoloum jirani na ziwa  Chad baada ya kukimbia vikundi vilivyojihami kuvamia kijiji chao na kuua ndugu zake saba na wengine 13 kutekwa nyara. 

“Waliua watu, hivyo tukakimbia”, anasema Alimi ambaye kufumba na kufumbua alijikuta anaanza maisha ya ukimbizi ndani ya nchi yake. 
Miaka 7 iliyopita walifika kambini hapa idadi ya watu ilikuwa ndogo, lakini sasa kwa macho huwezi kuona mwisho wa kambi, vibanda vya wakimbizi vimejaa eneo hili ambapo takwimu zinaonesha kuna zaidi  ya wakazi 450,000, kati yao zaidi ya 400,000 ni wakimbizi wa ndani kama Alimi. 
"Tulipofika hapa, tulikuwa kama wageni. Tulilala chini ya miti, hatukuwa na chochote. Kisha tukaenda msituni na kukusanya majani na kuni na tukaja hapa kujijengea makazi yetu. Mashirika ya kibinadamu pia yalitusaidia. Walitujengea nyumba mbili.” 
 
Kambini hapa shughuli mbalimbali zinaendelea, mmoja wa wake za Alimi kwa msaada wa fedha kutoka UNHCR ameweza kufungua duka la vyakula, Alimi hukaa na kuwafundisha Watoto wake, wake zake wengine huendelea na shughuli za nyumbani kama kutwanga nafaka kwa ajili ya mlo wa siku. 

Ingawa nchini Chad, mashambulizi dhidi ya raia yameendelea kupungua kwa miaka ya hivi karibuni,  bado kuna hatari inayowafanya washindwe kurejea makwao

"Tunachotaka sasa tukiwa hapa ni kujifunza kitu ambacho kinaweza kutusaidia baadaye. Hatuwezi kwenda nyumbani. Tunasubiri kuona kile tunachofanya kesho na kesho kutwa. 
 
Katika ukanda huu wa ziwa Chad kuna zaidi ya wakimbizi elfu 30 waliorejea nyumbani Chad kutoka nchi jirani kufuatia kuongezeka kwa vitisho vya waislamu wenye siasa kali.