Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia Eswatini zatia hofu UN: Chonde chonde serikali kubali mazungumzo

Mfalme Mswati III wa Ufalme wa Eswatini wakati akihutubia Baraza Kuu la un mwezi Septemba mwaka 2019
UN/Cia Pak
Mfalme Mswati III wa Ufalme wa Eswatini wakati akihutubia Baraza Kuu la un mwezi Septemba mwaka 2019

Ghasia Eswatini zatia hofu UN: Chonde chonde serikali kubali mazungumzo

Haki za binadamu

Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, imeelezea wasiwasi kuhusu mlipuko wa ghasia katika siku za karibuni huko Eswatini ghasia ambazo zimeripotiwa kusababisha mauaji au kujeruhiwa kwa makumi kadhaa ya watu waliokuwa wanaandamana kudai demokrasia.

Msemaji wa ofisi hiyo Liz Throsell amewaambia waandishi wa habari hii leo huko Geneva Uswisi ya kwamba “ghasia zilianza mwezi Mei mwaka huu wakati wanafunzi waliandamana kudai sheria ichukue mkondo wake baada ya mwanachuo kudaiwa kufa mikononi mwa polisi. Mwishoni mwa mwezi Juni maandamano yalishamiri na kufanyika kila siku yakidai demokrasia huko Eswatini zamani ikiitwa Swaziland, ambapo waandamanaji wanapaza sauti dhidi ya hali ya kiuchumi na kisiasa.”
 
Bi. Throsell amesema wamepokea ripoti ya matumizi ya nguvu kupita kiasi, manyanyaso na vitisho kutoka vikosi vya usalama huku baadhi ya waandamanaji wakiripotiwa kutia moto majengo na magari na kuweka vizuizi barabarani.

“Ingawa hali hivi sasa inaripotiwa kutulia, bado tuna hofu ya kuendelea tena kwa ghasia. Tunaomba mamlaka zizingatie misingi ya haki za binadmu na zirejeshe utawala wa kisheria hasa kupunguza matumizi ya nguvu kupita kiasi,” amesema msemaji huyo wa ofisi ya kamishna wa haki za binadamu akiongeza “tunatoa wito kwa serikali kuhakikisha kunafanyika uchunguzi huru, haki na usioegemea upande wowote kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki ikiwemo vitendo vinavyodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama.”

Halikadhalika serikali ya Ufalme wa Eswatini ianze mazungumzo kujadili chanzo cha wananchi kuanzisha maandamano.

Ofisi hiyo imesema itaendelea kushirikiana na serikali ya Eswatini ili kuimaisha uendelezaji wa haki za binadamu ikiwemo kusaidia na kutoa mwongozo wa kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu hakikisho la uhuru wa watu kujieleza, kuandamana na kujiunga kwenye vikundi kwa amani.