Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huko Tigray watu 400,000 wana njaa ya kupindukia- OCHA

Yeshialem Gebreegziabher, mwenye umri wa miaka 27 akiwa na binti yake, Kalkidan Yeman mwenye umri wa miezi 6 ambaye sasa anaugua unyafuzi. Wako katika kituo cha afya cha Aby Adi hko Tigray.
UNICEF
Yeshialem Gebreegziabher, mwenye umri wa miaka 27 akiwa na binti yake, Kalkidan Yeman mwenye umri wa miezi 6 ambaye sasa anaugua unyafuzi. Wako katika kituo cha afya cha Aby Adi hko Tigray.

Huko Tigray watu 400,000 wana njaa ya kupindukia- OCHA

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umetaka kuwa na fursa isiyo na vikwazo vyovyote ya kuwasilisha misaada ya kibinadamu jimboni Tigray nchini Ethiopia sambamba na kukoma kabisa kwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wanaosambaza misaada hiyo.
 

Ombi hilo limetolewa na Kaimu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, Ramesh Rajasingham wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa ni kikao cha kwanza cha wazi cha baraza hilo kuhusu mgogoro unaondelea kaskazini mwa Ethiopia.

Hotuba ya afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa imetoa taswira ya ya ‘kiza’ jimboni Tigray ikionesha kuwa watu 400,000 wamevuka hata kile kiwango cha kawaida cha njaa na wengine milioni 1.8 wako hatarini kujiunga nao.

“Takribani watu milioni 1.7 wamepoteza makazi kutokana na mapigano jimboni Tigray kati ya vikosi vya serikali na kikosi cha ulinzi wa Tigray ambapo 60,000 kati yao wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Sudan,” amesema Rosemary DiCarlo Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya siasa na ujenzi wa amani.

Bi. DiCarlo amesema matukio mengine zaidi ya 1,200 ya ukatili wa kingono na kijinsia yameripotiwa, idadi ambayo amesema inaweza kuwa kidogo tu ya matukio halisi katika mzozo huo ambao unaathiri zaidi wanawake na watoto.

Msaada wa kibinadamu ndio tegemeo kuu

“Maisha ya idadi kubwa ya wananchi wa Tigray yanategemea uwezo wetu wa kuwafikishia chakula, dawa, vvyakula vyenye virutubisho na misaada mingine ya kibinadamu,” amesema Kaimu Mkuu huyo wa OCHA akiwajulisha wajumbe 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ni kwa mantiki hiyo amesema wanahitaji kuwafikia wananchi hao sasa na siyo wiki ijayo na hivyo akatoa wito wa kuweza kuwafikishia misaada bila vikwazo vyovoyte “nikimaanisha kuwa sheria ya kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu lazima izingatiwe na makundi yote yanayopigana ili tuweze kufikisha misaada bila vikwazo.”

Mkutano wa Ijumaa ulikuwa mkutano wa kwanza wa wazi kabisa tangu mzozo wa Tigray uanze miezi minane iliyopita, ijapokuwa baraza hilo limeshakuwa na vikao 6 na mijadala lakini ya faragha.

Mkutano huo umefanyika siku nne baada ya Ethiopia kutangaa sitisho la mapigano kwa minajili ya kupitisha misaada ya kibinadamu, sitisho ambalo hata hivyo jeshi la ulinzi la Tigray ambalo linadhibiti mji mkuu wa jimbo hilo Mekele na miji mingine haijakubaliana nalo.

Mapigano yakome

Bwana Rajasingham ametumia kikao hicho kutaka kukoma kwa mapigano ili misaada ipitishwe bila vikwazo vyovyote na kwamba “ni muhimu tuchukue hatua haraka na bila kizuizi chochote.”

Viongozi hao wote wawili wametumia hotuba zao kulaani mashambulizi ya kulenga wahudumu wa kibinadamu ambayo yamesababisha vifo vya wafanyakazi wapatao 12, wakiwemo watatu kutoka shirika la madaktari wasio na mipaka, MSF wiki iliyopita.