Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufungaji wa intaneti kudhibiti wakosoaji umeota mizizi duniani

Serikali zinazidi kubinya kwa makusudi matumizi ya intaneti ili kudhibiti ubadilishanaji wa taarifa
Unsplash/Avi Richards
Serikali zinazidi kubinya kwa makusudi matumizi ya intaneti ili kudhibiti ubadilishanaji wa taarifa

Ufungaji wa intaneti kudhibiti wakosoaji umeota mizizi duniani

Haki za binadamu

Hii leo Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limejulishwa juu ya kuota mizizi kwa tabia ya serikali kufunga huduma za intaneti na simu za mkononi kama njia mojawapo ya kuendelea kukaa madarakani na kuziba midomo wakosoaji.

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa Clement Voule amesema hayo leo akiwasilisha ripoti yake mbele ya mkutano wa 47 wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, ripoti ikipatiwa jina “Komesha ufungaji wa intaneti.”

Bwana Voule ameonya kuwa ufungaji wa intaneti unazidi kushamiri na unafanyika kwa utalaamu wa hali ya juu kiasi kwamba ni vigumu kubaini.

Amesema mbinu hivi sasa zinatumiwa siyo tu na serikali za kidikteta bali pia katika nchi ambazo zilionekana kuzingatia demokrasia na zisizo na demokrasia na hivyo kudumaza mielekeo ya demokrasia.

Ametoa mfano wa nchi za Amerika ya Kusini ambako huduma za intaneti zilifungwa au kubinywa katika nchi za Nicaragua na Venezuela mwaka 2018, lakini tangu wakati huo Colombia, Cuba na Ecuador nazo zimeripotiwa kufunga huduma hizo wakati wa maandamano ya umma..

Kupunguza kasi ya intaneti

Mtaaamu huyo amesema idara za usalama kimakosa zimekuwa zikitumia mbinu zao kubanya kasi ya intaneti katika baadhi ya maeneo ili kuzuia waandamani kuwasiliana kabla na wakati wa maandamano.

“Huwa wanalenga apu mahsusi ya mtandao wa kijamii na maeneo na jamii fulani,” amesema Bwana Voule akiongeza kuwa uvurugaji wa huduma za intaneti umeendelea wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 na kuzuia watu kupata huduma za msingi za afya.

Mifano ya nchi zifungazo intaneti

Akitaja baadhi ya maeneo, mtaalamu huyo ametaja Bangladesh ambako wakazi wa wilaya ya Cox’s Bazar ambako kuna wakimbizi walikuwa bila intaneti kwa siku 355 kuanzia mwezi Septemba mwaka 2019.

Hiyo ilitokana na madai kuwa wakimbizi wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar waliandamana kuadhimisha miaka miwili tangu vikosi vya usalama huko nchini mwao vianze mashambulizi kwenye jimbo la Rakhine, tukio ambalo Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wakati huo, 
Zeid Ra’ad Al Hussein alifananisha na utoweshaji wa kabila.

Mara tu baada ya intaneti kufungwa, polisi na askari wa Bangladesh waliripotiwa kuingia kwenye kambi na kuanza kukamata, kupiga na kukamata watu na kuweka zuio la kutembea huku mamlaka zikichukua simu za kiganjani na kukataza wakimbizi wasinunue kadi za simu.

Ghasia Ethiopia

Zaidi ya watu milioni 100 nchini Ethiopia waliathiriwa na kufungwa kwa mtandao wa intaneti kwa wiki tatu mwezi Julai mwaka 2020, amesema mtaalamu huyo wa haki za kukusanyika na kuandamana kwa amani.

Hali hiyo ya kufungwa kwa mawasiliano kulifuatia maandamano yaliyochochewa na mauaji ya tarehe 29 mwezi Juni ya Hachalu Hundessa, mwanamuziki mashuhuri kutoka kabila la Oromo, hali ambayo ilikwamisha kazi ya kuthibitisha idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa wakati wa msako wa waandamanaji.

Huko Mali nako mawasiliano ya mtadano wa kijamii yalizuiwa kidoo kwa siku 5 wakati wa maandamano ya kusaka marekebisho ya kisiasa, hali ambayo pia mtaalamu huyo anasema ilitokea huko Iraq mwaka 2019, Iran mwezi Novemba 2019 kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta.