Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mungu anatuambia tusipoteze matumaini nami sijapoteza yangu: Mkimbizi Mihret

Wakimbizi kutoka Tigray wanaokimbia machafuko.
OCHA/Gabriela Vivacqua
Wakimbizi kutoka Tigray wanaokimbia machafuko.

Mungu anatuambia tusipoteze matumaini nami sijapoteza yangu: Mkimbizi Mihret

Wahamiaji na Wakimbizi

Mihret Gerezgiher mwenye umri wa miaka 25 ni mkimbizi kutoka Ethiopia lakini sasa anaishi katika makazi  ya wakimbizi  ya Tunaydbah Mashariki mwa Sudan. Alilazimika kukimbia na nguo alizovaa tu na kuacha kila kitu machafuko yaliposhika kasi jimboni kwake Tigray Novemba 2020, unyama alioushuhudia anasema bado unampa jinamizi kila alalapo

Katika makazi ya wakimbizi ya Tunaydbah Sudan Mehret anakumbuka yaliyomsibu akisema hakutegemea angeweza kutoka akiwa hai, aliogopa sana na ilikuwa usiku wa manane. 
Alivyonusurika anasema asilani hawezi kusahau kwani ilimbidi kujificha msituni kwa siku 4 na kisha kutembea mwendo mrefu hadi kuwasili hapa Sudan, ameshuhudia ukatili na unyawa wa hali ya juu ambao bado unasumbua fikra zake kila uchao. “Ilikuwa kama tunaangalia hadithi kwenye runinga, lakini ilikuwa si hadithi bali inatutokea sisi katika maisha yetu. Watoto na kina mama walibakwa, wanawake wanateseka, kina mama walikuwa wanajifungua na kulazimika kukimbia kwa miguu siku hiyohiyo. Tulikuwa na bahati sana kunusirika” 

Mihret ambaye kwa taaluma ni muhandisi licha ya aliyoshuhudia , kupoteza kazi yake na uwezo wa kujikimu kimaisha anasema kamwe hatokata tamaa anamatumaini na mustakbali wake “Nilikuwa mkufunzi wa masuala ya ujenzi na sasa hapa nafanyakazi kama msimamizi wa eneo. Mungu anatuambia tusipoteze matumaini, nami sitopoteza  bali natumai kuwa na amani katika nchi yangu. Hapo awali hatukujua tahamani ya amani lakini sasa tunatambua umuhimu wake kwasababu tumeipoteza.” 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR maelfu kwa maelfu ya raia wa Ethiopia wamevuka mpaka na kuingia Sudan ambako shirika hilo sasa limewahamishia kwenye makazi maalum ya wakimbizi na wadau wanawapa msaada wa kibinadamu unaohitajika. 

Hata hivyo shirika hilo linasema fedha zaidi zinahitajika kukidhi mahitaji ya wakimbizi hao na wakimbii wa ndani waliotawanywa jimboni Tigray.