Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa wa kijinsia waangaziwa zaidi huko Paris Ufaransa

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia ufunguzi wa jukwaa la kizazi cha usawa hii leo huko Paris nchini Ufaransa
UN
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia ufunguzi wa jukwaa la kizazi cha usawa hii leo huko Paris nchini Ufaransa

Usawa wa kijinsia waangaziwa zaidi huko Paris Ufaransa

Wanawake

Hii leo huko Paris nchini Ufaransa kumeanza jukwaa la siku tatu la kusaka kusongesha usawa wa kijinsia kwa kujumuisha vijana katika kufanikisha lengo hilo namba 5 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo unafanyika kwa kuzingatia kuwa miaka 25 baada ya mkutano wa kimataifa wa wanawake huko Beijing nchini China, bado usawa wa jinsia unasalia ndoto kwa maeneo mengi. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women, hadi sasa hakuna taifa linaloweza kujinasibu kuwa limefikia usawa wa kijinsia katika nyanja zote, na ndipo likaunda kikosi kazi cha vijana 40 wa kusongesha kizazi cha usawa au generation Equality. Miongoni mwao ni Abel Koka wa shirika la Restless Development kutoka Tanzania ambaye yuko tayari Paris akieleza matarajio yao akisema, “tuko hapa kuhakikisha kwamba yale malengo  ya kuleta usawa wa kijinsia katika jamii yanatolewa matamko mahsusi na siyo ahadi tu lakini ni nini kinaenda kufanyika kuleta usawa wa kijinsia.”

Tulipomuuliza tangu kuundwa kwa kikosi kazi hicho kuna mafanikio yoyote, Bwana Koka amesema, “tangu tumeanza kazi na UN-Women mwaka 2019 tumeona mabadiliko mengi kwa sababu mwanzoni vijana walikuwa hawapewi nafasi ya kushiriki katika ngazi za maamuzi lakini pia vijana walikuwa hawashiriki katika harakati za usawa wa kijinsia, lakini kupitia kikazi hiki cha Umoja wa Mataifa au UN-Women tumeweza kuonesha vijana kuwa usawa wa kijinsia hauwezi kupatikana bila sisi kuwa katikati ya harakati na juhudi mbalimbali za kuleta usawa wa jinsia. Na kwa kufanya hivyo tumeshiriki katika kuandaa midahalo mbali mbali ambako vijana wametoa mawazo yao ni nini kifanyike ili usawa wa kijinsia uweze kupatikana.”

Pichani kati ni Paul Siniga, balozi kijana wa SDGs na mchechemuzi wa kampeni ya He4She akiwa kwenye picha na wanafunzi wa kike.
UN Tanzania
Pichani kati ni Paul Siniga, balozi kijana wa SDGs na mchechemuzi wa kampeni ya He4She akiwa kwenye picha na wanafunzi wa kike.

Akizungumzia fursa za kusongesha ajenda ya usawa wa kijinsia, mjumbe huyo wa kikosi kazi cha UN-Women chenye wajumbe 40 kutoka maeneo mbalimbali duniani amesema nuru na fursa ipo kwa sababu viongozi sasa hivi tofauti na hapo awali wameanza kusikiliza vijana nini wanataka ili kuleta usawa wa jinsia katika jamii. Lakini pia mataifa yameona fursa ya kuwekeza kwenye juhudi mbali mbali za kuleta usawa wa jinsia. “Kwa hiyo naweza kusema nuru ipo kwa sababu kile kilichofanywa Beijing mwaka 1995 vijana wanasukuma sasa hivi kwa kuwahimiza viongozi wao kuleta mabadiliko chanya ya kumweka msichana na mwanamke katika ngazi au  chachu ya maendeleo.”

Alipoulizwa iwapo kuna vipingamizi Bwana Koka amesema ni vijana au jamii kutoelewa kwa kina kuhusu usawa wa jinsia na faida zake katika jamii. “Pia vijana wanakosa rasilimali katika kusongesha ajenda ya kupeleka usawa wa jinsia kwenye jamii. Hivyo tunaomba wapitisha maamuzi kuona ni namna gani wanawekeza katika rasilimali fedha, vifaa lakini pia mafunzo mbalimbali kwa vijana na jamii ili waelewa faida za usawa jinsia. Ili nao waweze kuunga juhudi kwenye kutatua changamoto mbalimbali zinazozuia mwanamke na msichana kuwa na haki sawa baina yake na wanaume na wavulana.”

Tweet URL

Guterres naye azungumza

Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonnio Guterres amesema usawa wa kijinsia ni suala la madaraka na nguvu katika dunia ambayo bado wanaume ndio wanaongoza kwa kiasi kikubwa.

Kwa mantiki hiyo anasema ni nadra sana madaraka mtu anapatiwa na hivyo ni lazima unyakue. Amesema suala la usawa wa kijinsia ni moja ya vipaumbele vyake vitano na hivyo ataweka mazingira bora ya kujenga usawa huo.

“Kufikia haki sawa, sheria kandamizi na baguzi duniani kote lazima zifutwe na kuwepo na usawa kisheria. Wanawake walio katika sekta za kiuchumi zisizo rasmi wanaendelea kubeba gharama ya janga la Corona au COVID-19 bila kusahau ukosefu wa usawa kwenye malipo ya ujira na hifadhi ya jamii.” Amesema Guterres.

Amerejelea pia hoja ya kuibuka zaidi na ongezeko la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana wakati huu wa COVID-19 akisema kutokomeza hali hiyo ni lazima hatua zozote zile ziwe kitovu cha sera na malengo ya viongozi wote.

Ametamatisha kwa kuzungumzia umuhimu wa mazungumzo au mijadala baina ya vizazi akitaka kuruhusiwa kwa vijana kuwa sehemu ya kupitisha maamuzi katika jamii ya leo ya kidijitali.