Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Joto la kupindukia na la hatari laighubika Amerika ya Kaskazini (WMO)

Seattle imerekodi kiwango cha juu zaidi cha joto nchini Marekani
Unsplash/Alex Mertz
Seattle imerekodi kiwango cha juu zaidi cha joto nchini Marekani

Joto la kupindukia na la hatari laighubika Amerika ya Kaskazini (WMO)

Tabianchi na mazingira

Magharibi mwa Canada na kaskazini mwa Amerika wamekumbwa na hali mbaya ya joto kali ambalo wakati mwingine linazidi nyuzi joto 45 ° C, na kuvunja rekodi za kihistoria katika miji kadhaa. 

Kulingana na Shirika la hali ya hewa duniani (WMO), hili ni "wimbi la joto la kipekee na hatari", ambalo linaenea kaskazini magharibi mwa Amerika na magharibi mwa Canada katika maeneo ambayo yamezoea hali ya hewa ya baridi. Joto linaweza kufikia hadi 45 ° C wakati wa mchana kwa siku tano au zaidi, na usiku pia ukiwa na joto kali sana.

"Joto hili kali linaleta tishio kubwa kwa afya ya binadamu, kilimo na mazingira, kwani ukanda huo haujazoea joto kama hilo na watu wengi hawana viyoyozi," amesema Clare Nullis msemaji wa OMM huko Geneva, wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jumanne, akibainisha kuwa rekodi nyingi zimevunjwa, na  "ni ngumu kuzifuatilia". 

Picha ya Mawingu katika jimbo la Colorado, Marekani
WMO/Guillaume Hobam
Picha ya Mawingu katika jimbo la Colorado, Marekani


Rekodi ya miaka 84 imevunjwa nchini Canada 
Kwa mujibu wa WMO, huko Canada, kwa mfano, rekodi ya miaka 84 ilivunjwa Jumapili iliyopita.  
Jamii ya Lytton, British Columbia, ilichapisha kipimajoto cha njuzi joto 46.6 ° C. Hii ni nyuzi  joto 1.6 ° C juu kuliko rekodi ya awali iliyowekwa Julai 5 mwaka 1937.  
Chini ya saa 24 baadaye, Lytton ilivunja rekodi hii tena, kwa kufikia nyuzi joto 47.9 ° C jana Jumatatu  28 Juni 2021. 

Katika eneo la baridi, Yukon na maeneo ya Kaskazini Magharibi pia yalirekodi hali ya joto kupita kawaida kwa wakati wote, sio tu mwezi huu wa Juni, bali wakati wote wa mwaka.  
"Hali hii ni ya kawaida kwa maeneo kama Mashariki ya Kati kuliko katika jimbo ambalo ni makazi ya milima ya Rocky na hifadhi ya kitaifa ya Glacier," ameongeza Bi Nullis.

Kupanda kwa joto kulianza Ijumaa iliyopita na kukafikia kilele mapema wiki hii kwa eneo la pwani na katikati ya wiki kwa maeneo ya ndani ya British Columbia kisha joto litahamia Mashariki hadi Alberta. 
"Joto la wakati wa usiku ni kubwa kuliko wastani wa joto la mchana mwishoni mwa Juni, hali ambayo ni mbaya sana. Watu wanalazimika kwenda kwenye maktaba na kwenye vituo vya manunuzi ili kupata kiyoyozi kwa masaa machache.” Armel Castellan, mtaalam wa hali ya hewa na mazingira Canada, alinukuliwa na taarifa ya mwandishi wa habari wa WMO. 

 

Shirika la hali ya hewa duniani limesema maeneo mengi duniani yatashuhudia ongezeko la joto mwaka 2020
WMO/Kabelo Tamocha
Shirika la hali ya hewa duniani limesema maeneo mengi duniani yatashuhudia ongezeko la joto mwaka 2020


Nyuzi joto 50 ° C katika eneo la Sahara 
Upande wa pili wa mpaka wa Canada, mji wa Seattle uliweka rekodi mpya ya nyuzi joto 40 ° C (104 ° F) Jumapili na kuvunja rekodi hiyo Jumatatu kwa kufikia nyuzi joto  41.7 ° C sawa na (107 ° F).  
Pia huko Marekani, Portland ilivunja rekodi mara mbili:  kwanza  nyuzi joto 42 ° C (108 ° F) Jumamosi na kishja nyuzi joto 44.4 ° C (112 ° F) Jumapili. 
Mahali pengine ulimwenguni, hasa sehemu za kaskazini tayari zinapata hali ya kipekee ya msimu wa majira ya joto kuanzia Afrika Kaskazini, hadi Rasi ya Arabia, hadi Ulaya ya Mashariki.  
Mashariki, hadi Irani na kaskazini magharibi mwa bara la India. Joto la juu la kila siku linazidi nyuzi joto 45 ° C  na katika maeneo kadhaa hata hufikia nyuzi joto 50 ° C katika  eneo la Sahara. 
Urusi ya Magharibi na maeneo ya karibu na bahari ya Caspian pia yalipata hali ya joto isiyo ya kawaida.  
Katika sehemu za ukanda huo haswa Moscow, joto linatarajiwa kufikia nyuzi joto 30 ° C wakati wa mchana na kubaki juu ya nyuzi joto 20 ° C usiku. 
Maeneo karibu na bahari ya Caspian yanatarajiwa kupata joto linalofikia nyuzi joto 40 ° C na kusalia juu ya nyuzi joto 25 ° C usiku.  

Hali ya hewa duniani mwaka 2020
Source: WMO
Hali ya hewa duniani mwaka 2020


Kulingana na WMO, kuna uwezekano kwamba rekodi hizi za joto zitavunjwa wakati wa wimbi hili la joto na ni mawimbi ya joto ya mara kwa mara katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi. 
Hali hizi za hewa za joto mwanzoni mwa msimu wa joto zinakuja kutokana na  kuongezeka kwa mabadiliko ya tabianchi.  
Joto la dunia tayari liko nyuzi joto 1.2 ° C juu ya viwango vya kabla ya maendeleo ya viwanda. 
"Mawimbi ya joto yanazidi kuwa ya mara kwa mara na makali, kwani viwango vya gesi chafuzi husababisha joto la ulimwengu kuongezeka," amesema msemaji wa WMO. 
Kwa mujibu wa taarifa ya WMO kuhusu mabadiliko ya tabianchi duniani iliyotolewa mwaka 2019, watu walio katika mazingira magumu zaidi ambao wana umri wa miaka 65 au zaidi milioni 220 waliathirika na ongezeko baya la joto joto mwaka 2018, ikilinganishwa na wastani wa kipindi cha kumbukumbu katika historia cha mwaka 1986-2005. 


Walakini, hatari zinazohusiana na hali ya hewa kwa afya, maisha, uhakika wa chakula, usambazaji wa maji, usalama wa binadamu na ukuaji wa uchumi zinatarajiwa kuongeza na kiwango cha  joto kwa nyuzi joto 1.5 ° C na kisha kuongezeka zaidi na kufikia nyuzi joto 2 ° C. 
"Kwa kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5 ° C badala ya nyuzi joto  2 ° C, tunaweza kupunguza kwa milioni 420 idadi ya watu walio kwenye hatari ya mawimbi makali ya joto",imeonya ripoti ya mwisho, ya kikundi cha kinachojumuisha serikali na wataalam wa mabadiliko ya tabianchi (IPCC).