Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali si hali Tigray, baa la njaa linanyemelea na hospitali hazifanyi kazi:UN

Mtoto wa mwaka mmoja akipatiwa lishe ya utapiamlo katika kituo cha Afya katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia
© UNICEF/Mulugeta Ayene
Mtoto wa mwaka mmoja akipatiwa lishe ya utapiamlo katika kituo cha Afya katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia

Hali si hali Tigray, baa la njaa linanyemelea na hospitali hazifanyi kazi:UN

Amani na Usalama

Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa leo yameelezea hofu yake kuhusu hali ya sintofahamu inayoendelea kughubika jimbo la Tigray nchini Ethiopia kutokana na vita vinavyoendelea licha ya wito uliotolewa na serikali wa kusitisha uhasama huku kukiwa na hali mbaya ya chakula inayoelekea kwenye baa la njaa na uwezekano wa milipuko ya magonjwa. 

Onyo hilo linatokana na taarifa kwamba Jumatatu vikosi vinayounga mkono upinzani vimeripotiwa kuingia katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mekelle, baada ya karibu miezi minane ya mapigano makali. 

Kufuatia uporaji wa vifaa vya video vya ofisi zake huko Mekelle, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetoa taarifa kulaani wahusika wa uporaji huo na kusonta kidole kwa kikosi cha ulinzi cha Kitaifa cha Ethiopia. 

Mapema mwezi huu, shirika hilo lilionya kuwa watoto 140,000 wana utapiamlo mkali na wako katika hatari ya kufa, endapo msaada hautapatikana kuwanusuru. 

Tuna hofu kubwa sana  "Tumeona ripoti ambazo zimekuja na UNHCR ina wasiwasi mkubwa juu ya maendeleo ya hivi karibuni ndani ya Tigray, haswa katika mji mkuu wa Mekelle", amesema Boris Cheshirkov, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).  

Ameongeza kuwa "Ingawa tunashukuru kwamba wafanyakazi wetu wote wako salama na tunajua waliko, bado tuna wasiwasi juu ya ukosefu wa mawasiliano, kwani nishati ya umeme na mitandao ya simu havifanyi kazi. Hii imefanya iwe vigumu zaidi kwa wafanyakazi wetu kufanya kazi zao na kutoa msaada wa kibinadamu". 
"Tunatoa wito wa utulivu na kujizuia na tunatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kutii sheria za kimataifa za kulinda raia, pamoja na watu ambao wamehama makazi yao na kuhakikisha kuwa wafanyikazi wa kibinadamu wanaweza kuendelea kutekeleza majukumu yao na kufikia watu wengi kadiri wanavyoweza ambao wanahitaji msaada muhimu kwa sasa.” ameendelea kusema Bwana. Cheshirkov. 

Wakimbizi kutoka Tigray wanaokimbia machafuko.
OCHA/Gabriela Vivacqua
Wakimbizi kutoka Tigray wanaokimbia machafuko.

 


Kuimarisha usalama: WHO 

Akiunga mkono wasiwasi huo, msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO) Tarik Jasarevic amesema mjini Geneva Uswisi kwamba shirika hilo "linachukua hatua za kuimarisha usalama na ustawi wa wafanyakazi wetu, lakini wakati huo huo tunaendelea kutoa shughuli pale inapowezekana kufanya hivyo. Hii ni pamoja na katika kambi za wakimbizi wa ndani, ufikiaji wa huduma muhimu za kiafya na kuongeza idadi ya kliniki za afya zinazotembea katika jamii ambazo ni vigumu kuzifikia.” 

Zaidi ya hayo Bwana. Jasarevic  ameongeza kuwa "Ni wazi tuna wasiwasi juu ya uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, ugonjwa wa ukambi na malaria katika mkoa huo. Kwa kuongezea, mkoa wa Tigray pia uko katika ukanda ambao hukumbwa na homa ya uti wa mgongo na uko katika hatari ya kuzuka kwa homa ya manjano." 

Baada ya mzozo wa miezi nane kati ya wanajeshi wa serikali ya Ethiopia na wale watiifu kwa jeshi kubwa la mkoa la Tigray People's Liberation Front (TPLF), hospitali "hazifanyi kazi", watu wanaendelea kukimbia na njaa "inakaribia", Bwana Jasarevic amesisitiza . 

Pia kuna hatari kubwa ya magonjwa ya kuambukiza na yanayoweza kuzuiliwa na chanjo yanayosambaa kwa sababu ya ukosefu wa chakula, maji safi, makazi salama na upatikanaji wa huduma za afya.

Hatari hii ni "halisi", afisa huyo wa WHO amesema. "Sababu hizi zote zikichanganya ni kichocheo halisi kwa magonjwa makubwa zaidi."