Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na WFP wameniondoa ujinga na sasa nalipia ada wanangu na nimejenga nyumba- Germaine

Germaine, mnufaika wa mradi wa WFP wa kutengeneza sabuni akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto wake.
© WFP/Arete/Fredrik Lerneryd
Germaine, mnufaika wa mradi wa WFP wa kutengeneza sabuni akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto wake.

FAO na WFP wameniondoa ujinga na sasa nalipia ada wanangu na nimejenga nyumba- Germaine

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika jimbo la Tanganyiko huko cchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mizozano baina ya jamii ya mji wa Kabalo sasa imesalia historia baada ya miradi ya uwezeshaji amii inayotekelezwa na mashirika ya  Umoja wa Mataifa kuleta siyo tu utengamano bali pia kuinua vipato vya wanajamii wakiwemo wajane

Miongoni mwa wajane hao ni Germaine Kitenge, mama wa watoto wanane na ana umri wa miaka 47. Miaka sita iliyopita maisha yake yalikuwa ya kifukara akisema, “mume wangu alikuwa mwalimu na mimi nilikuwa nauza unga sokoni. Tulihangaika sana kwa sababu mshahara wa mume wangu ulikuwa kidogo sana. Kupata chakula hapa Kabalo ilikuwa ni vigumu. Siku nzima nilimalizia sokoni kuchuuza unga.”

Mwaka 2014 mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo, FAO likaja na mradi wa kuwapatia pembejeo za kilimo kama vile mbegu, huku lile la mpango wa chakula WFP likiwapatia stadi za kusoma na fedha za kuboresha biashara zao akisema, “nashukuru Mungu kwa sababu ya FAO na WFP hivi sasa tuna chakula kingi. Walituletea mradi ambapo kilimo cha mihogo ni bora, halikadhalika kilimo cha karanga na mpunga. Tumepatiwa pia majembe pamoja na magunia ya kisasa ya kuhifadhi mavuno yetu."

Kikundi cha wanawake wa Kabalo jimboni Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakitengeneza sabuni ikiwa ni sehemu ya mradi unaoratibiwa na WFP.
© WFP/Arete/Fredrik Lerneryd
Kikundi cha wanawake wa Kabalo jimboni Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakitengeneza sabuni ikiwa ni sehemu ya mradi unaoratibiwa na WFP.

Pamoja na kilimo, Germaine na kikundi cha wanawake Kabalo wanatengeneza sabuni na kuuza akisema, “baada ya mafunzo ya kusoma na kuandika, niliweza kujifunza kutengeneza sabuni, kazi ambayo imeniwezesha kulisha familia yangu. Nimevuna kilo 300 za mpunga baada tu ya kupokea mbegu bora. Nilipouza nilipata fedha za kutosha kununua vitabu na kalamu watoto wangu walipofungua shula. Nilinunua pia matofali ya kujengea nyumba yangu mpya.”

Matumaini ya Germaine hivi sasa ni kwamba kilimo bora na kazi ya kutengeneza sabuni vitamwezesha kuelimisha vyema zaidi watoto wake shuleni ili waweze kuwa na maisha na elimu bora zaidi kuliko yeye.

Na kwa kuwa jamii sasa zinafanya kazi pamoja, mvutano baina ya jamii tofauti umemalizika kwa kuzingatia kuwa mizozo ya mara kwa mara imekuwa ndio chanzo cha njaa katika majimbo la Mashariki mwa DRC na jimboni Tanganyika.

WFP inapanga kufikia watu milioni 8 mwaka huu pekee huko DRC kwa kuwapatia chakula, mgao wa fedha na vyakula vyenye virutubisho.