Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania tumejiunga na COVAX ili tupate chanjo ya COVID-19; idadi ya wagonjwa ni zaidi ya 100- Rais Samia

Sinovac-CoronaVac chanjo ya COVID-19
Sinovac
Sinovac-CoronaVac chanjo ya COVID-19

Tanzania tumejiunga na COVAX ili tupate chanjo ya COVID-19; idadi ya wagonjwa ni zaidi ya 100- Rais Samia

Afya

Wakati shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika likionya kuwepo kwa wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 barani Afrika, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema sasa taifa hilo lina wagonjwa zaidi ya 100 na tayari taratibu zinafanyika ili kuingiza chanjo ya COVID-19.

Rais Samia amesema hayo Jumatatu wakati akijibu swali wakati wa mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es salaam ambapo amesema, “nataka niwe mkweli Tanzania tuna wagonjwa katika hili wimbi la tatu. Mpaka taarifa nilizozipata juzi nadhani kuna wagonjwa kama mia moja na, kati yao si chini ya wagonjwa 70 na wako kwenye matibabu ya gesi na wengine wako kwenye matibabu  ya kawaida. Sasa ukiangalia si wengi lakini hatuna budi kujikinga wasiongezeke.

Sasa tumeamua tuchanje, chanjo itakuwa hiari

Kwa kuzingatia hali ya sasa, Rais Samia amesema "Kwa hiyo hatua tuliyochukua kwanza tuliamua kwamba twende na ulimwenguni uanvyokwenda tuchanje na tuchanje kwa hiari. Mtanzania anayetaka atachanja na asiyetaka ataangalia kwa nafsi yake.”

Kwa hiyo tukaharakisha watanzania tukasema na sisi tumo, mengine ya kuagiza na chanjo ipi yatafuata - Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania

Rais Samia amesema uamuzi wao umezingatia kwamba watanzania wengi ambao ni wafanyabiashara wamepata tayari chanjo hizo nje ya nchi, iwe ni Dubai Falme za kiarabu au Afrika Kusini. Amesema watanzania hao tayari wako nchini na wanaendelea na shughuli zao.

Akaeleza tayari wameshajiunga na mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuchagiza upatikanaji wa chanjo COVAX kwa nchi za kipato cha chini akisema, “tarehe 15 Juni ilikuwa mwisho wa kuingia kwa wale watakaopata chanjo mwaka ujao wa 2022. Kama hukusema mimi nimo mpaka tarehe 15 Juni mwaka huu, basi chanjo utakayopata ni mwaka 2023. Kwa hiyo tukaharakisha watanzania tukasema na sisi tumo, mengine ya kuagiza na chanjo ipi yatafuata.”

Ameeleza kuwa kinachofanyika sasa wataalamu wanafanyia kazi ni chanjo ipi ipekwe Tanzania na kwa vipi.

Miongoni mwa nchi za Afrika ambako tayari COVAX imewasilisha chanjo ni pamoja na Rwanda, Uganda, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.