Skip to main content

Upimaji wa COVID-19 uzingatie hali ya nchi, WHO yatoa mwongozo

Kituo cha kupima COVID-19 jimboni Ogun, kusini-magharibi mwa Nigeria
WHO
Kituo cha kupima COVID-19 jimboni Ogun, kusini-magharibi mwa Nigeria

Upimaji wa COVID-19 uzingatie hali ya nchi, WHO yatoa mwongozo

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limeboresha mwongozo wake kuhusu upimaji wa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ili kupanua wigo wa mazingira mbalimbali ya virusi hivyo katika nchi tofauti tofauti.

Mwongozo huo wa WHO unaelezea mapendekezo kwa mikakati ya kitaifa ya upimaji na uchunguzi  kwa kutumia vipimo vya kina PCR na vile vya papo kwa papo na wakati huo huo kuzingatia hali ya rasilimali za upimaji zinazopatikana kwa nchi husika.

Hatua hiyo ya WHO imekuja wakati huu ambapo virusi vya Corona vinabadilika na kunyumbulika katika maeneo mbalimbali duniani na vingine kuonekana kuwa vinaambukizika kwa urahisi zaidi kuliko vingine.

WHO inasema uchunguzi wa wakati muafaka na sahihi ni muhimu katika kuzuia kusambaa kwa COVID-19 ikisema, “uchunguzi wowote ule lazima ufuatiliwe na hatua thabiti za afya ya umma ikiwemo kuwatenga wale waliothibitika kuwa na Corona na kuwapatia huduma sahihi huku wale waliokuwa karibu nao wakifuatiliwa na kutengwa vile vile kwenye karantini.” 

Mapendekezo Mapya

WHO inataka nchi ziwe na mkakati wa kitaifa wa upimaji au uchunguzi wa COVID-19 unaoainisha malengo yanayoendana na mabadiliko ya mwongozo mpya kulingana na aina ya mlipuko wa Corona, rasilimali za upimaji zilizopo katika nchi husika.

Halikadhalika upimaji na uchunguzi wa virusi hivyo aina ya SARS-CoV-2 lazima uoanishwe na hatua zozote za ulinzi wa afya ya umma na kuhakikisha kuna huduma za tib ana usaidizi kwa wale ambao watakutwa na virusi vya Corona au wale ambao wamekuwa karibu na wagonjwa hao ili nao pia waweze kufuatiliwa na hivyo kudhibiti kuenea kwa virusi.

WHO pia inataka mtu yeyote ambaye atashukiwa kuwa na COVID-19 basi lazima achunguzwe iwapo ana virusi hivyo aina ya SARS-CoV-2, bila kujali amepatiwa chanjo au la na iwapo amewahi kuugua ugonjwa huo wa au la.

Kwa watu ambao wamekidhi vigezo vya pengine kuwa na COVID-19 basi lazima wapatiwe kipaumbele katika kupimwa ugonjwa huo na iwapo hakuna rasilimali za kutosha kwa ajili ya kupima watu wote wanaoshukiwa kuwa na Corona, basi wafuatao wanapaswa kupatiwa kipaumbele katika uchunguzi.

Makundi hayo ni wale walio hatarini kupata magonjwa hatari, wahudumu wa afya, wagonjwa waliolazwa hospitalini, watu wasio na dalili za Corona lakini wako katika vituo vya huduma ya tiba kwa muda mrefu.