Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wanaosafirishwa kwa njia haramu wanakabiliwa na madhila makubwa:UNODC

Ripoti ya utafiti ya UNODC kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu (HTMSS)
UNODC
Ripoti ya utafiti ya UNODC kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu (HTMSS)

Wahamiaji wanaosafirishwa kwa njia haramu wanakabiliwa na madhila makubwa:UNODC

Haki za binadamu

Ripoti ya utafiti mpya iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa na Uhalifu UNODC imesema, wahamiaji ambao wanatumia mitandao ya usafirishaji haramu kukimbia nchi zao mara nyingi wanakabiliwa na ukatili wa kupindukia, mateso, ubakaji na kutekwa wakiwa njiani au wanaokoshikiliwa mateka.  

Kwa mujibu wa utafiti huo uliojikita na usafirishaji haramu wa binadamu na sehemu ya wahamiaji (HTMSS), licha ya ukubwa wa uhalifu unaotendeka katika suala hili ni hatua kidogo sana zilizochukuliwa na mamlaka za kitaifa na katika visa vingine maafisa wanahusika katika uhalifu huo.  
 
Ripoti imesema katika maeneo ambao usafirishaji haramu huo umeshamiri ni pamoja na njia safari kupitia Afrika Kaskazini na Magharibi, bahari ya Mediterranean a Amerika ya Kati.  
 
Pia utafiti huo uliopewa kichwa“Ukatili na kutelekezwa-mtazamo wa kijinsia katika usafirishaji haramu wa wahamiaji na hatua” umemulika aina mbalimbali za ukatili wanaotendewa wanaume na wanawake na kuelezea sababu na vichocheo vya  kufanyika kwa ukatili wakati wa operesheni za usafirishaji haramu.  
 


     Yaliyojiri katika utafiti 

"Utafiti wetu umeonyesha kuwa vurugu hutumiwa na wasafirishaji au wahusika wengine kama aina ya adhabu, vitisho au kulazimisha, na mara nyingi hufanywa bila sababu maalum," amesema Morgane Nicot, kiongozi wa timu ya maendeleo ya maarifa ya HTMSS. 
Ameongeza kuwa "Tumegundua kwamba wahamiaji wa kiume kimsingi wanafanyishwa kazi za shuruti na unyanyasaji wa kimwili wakati wanawake wanakabiliwa zaidi na unyanyasaji wa kijinsia, na kusababishiwa mimba zisizohitajika na utoaji mimba. Jinsia zote zinaweza kukabiliwa na unyama na udhalilishaji.” 
Ripoti imeongeza kuwa usafirishaji haramu wa wahamiaji ni uhalifu wenye faida ambayo inajumuisha upangaji wa mipaka isiyo halali dhidi ya malipo kwa watu ambao wana hamu ya kuondoka nchi zao lakini hawana njia halali za kuondoka 
Watu hawa wanaweza kuwa wanakimbia majanga ya asili, mizozo au mateso au kutafuta ajira, elimu na fursa za kuungana tena na familia zao. 
 

Wahamiaji na wakimbizi wengi wa Afrika wanapenda kwenda Djibouti ni sehemu hususan wale wanaotoka Ethipia, Eritrea na Somalia
IOM/Alexander Bee
Wahamiaji na wakimbizi wengi wa Afrika wanapenda kwenda Djibouti ni sehemu hususan wale wanaotoka Ethipia, Eritrea na Somalia

  Hakuna hatua Madhubuti zinazochukuliwa 

Kwa mujibu wa ripoti ingawa kuna hatima mbaya ya maelfu ya wahamiaji wanaosafirishwa ambao kila mwaka hufa baharini, huangamia jangwani au kunyong'onyea kwenye makasha wanamosafirishiwa imeandikwa, lakini kuna habari kidogo zinazopatikana juu ya kwanini vitendo vya machafuko na unyanyasaji vinasababishwa kwa wahamiaji, je! Hii ina athari gani kwao , na jinsi gani inashughulikiwa na mamlaka. 
“Hii ndiyo sababu tuliamua kufanya utafiti huo wa lazima. Utafiti wetu pia unachambua jinsi maafisa wa kutekeleza sheria wanavyokabiliana na kesi za usafirishaji haramu wa wahamiaji na inaangazia jinsi ilivyo vigumu kushtaki uhalifu kama huo, "amesema Bi Nicot. 

Mahojiano mazito na wahamiaji waliosafirishwa kwa njia haramu na maoni kutoka kwa washirika wa UNODC ambao hufanya kazi moja kwa moja na wahamiaji wanaonyanyaswa wanathibitisha kuwa utumiaji wa vurugu umeenea katika njia nyingi zinaziotumiwa kwa usafirishaji wa magendo. 

Lakini, ripoti imeongeza kuwa kuna ushahidi mdogo kwamba uhalifu kama huo husababisha uchunguzi au kesi za kisheria, haswa katika nchi za usafirishaji ambapo makosa yametendeka. 
"Madhila ambayo wahamiaji hupitia wakati wa biashara ya usafirishaji wa magendo sio mara zote hurekodiwa au hakuna ushahidi wa kutosha kudhihirisha ukali wa adhabu zilizotolewa na mahakama za kitaifa dhidi ya wasafirishaji haramu," amelezea Morgane Nicot. 

Wahamiaji wengine hawapendi kuripoti unyanyasaji kwa sababu wanaweza kuchukuliwa kama wahalifu, labda kwa sababu ya hali yao isiyo ya kawaida au kwa kutoa mimba, kufanya ngono nje ya ndoa au na watu wa jinsia moja, vitendo ambavyo vinaadhibiwa katika nchi zingine. 
 


  Kuhusika kwa watu wanaopaswa kulinda wahamiaji

Morgane Nicot  amesema "Wahamiaji pia hawajitokezi kwa sababu sehemu kubwa ya dhuluma hutoka kwa maafisa wa umma ambao wanaweza pia kushiriki katika operesheni nzima ya magendo. Maafisa hawa ni pamoja na walinzi wa mpakani, maafisa wa polisi na wafanyikazi ambao hufanya kazi katika vituo vya kizuizini.” 

Utafiti huo umetoa mwongozo kwa wataalamu wa haki ya makosa ya jinai juu ya jinsi ya kuchunguza na kushtaki kesi za vurugu na unyanyasaji wakati wa shughuli za usafirishaji haramu wa wahamiaji, wakati wa kuzingatia mahitaji yanayohusiana na kijinsia na udhaifu wa wahamiaji wanaohusika. 
Pia imeorodhesha msururu wa mapendekezo kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa juu ya njia za kukabiliana na vinavyosababisha usafirishaji haramu wa wahamiaji, kulinda na kusaidia wahamiaji na kupata hukumu kwa kesi za uhalifu huu.

"Ikiwa tunataka kukabiliana vyema na uhalifu unaohusiana na biashara haramu ya usafirishaji  wa wahamiaji na kuwapa wahamiaji ambao wamepata kiwewe kinga na msaada unaofaa, basi lazima tuelewe ni kwanini unyanyasaji huu unatokea," amesema Bi Nicot wa UNODC. 

Ameongeza kuwa “Tunahitaji kufahamu zaidi athari za muda mfupi na za muda mrefu za ukatili huo kwa watu mbalimbali na wa jinsia tofauti na jinsi gani mamlaka za kitaifa zinaweza kutoa haki kwa waathirika wa uhalifu huu. Utafiti wetu ni hatua muhimu ya mwelekeo sahihi.” amehitimisha Bi. Nicot