Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu UN alaani mauaji ya wafanyakazi wa misaada Tigray na kutaka hatua zichukuliwe

Daktari akimfanyia uchuguzi mtoto Zinabu na kumpatia matibabu na kumuelimisha mama yake jinsi ya kuhakikisha binti yake anakuwa na afya njema
© UNICEF
Daktari akimfanyia uchuguzi mtoto Zinabu na kumpatia matibabu na kumuelimisha mama yake jinsi ya kuhakikisha binti yake anakuwa na afya njema

Katibu Mkuu UN alaani mauaji ya wafanyakazi wa misaada Tigray na kutaka hatua zichukuliwe

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mauaji ya wafanyakazi watatu wa shirika la Misaada la madaktari wasio na mipaka MSF yaliyofanyika huko Tigray nchini Ethiopia na kutaka wahusika wa mauaji hayo wakamatwe na kuchukuliwa hatua stahiki. 

Kupitia taarifa yake aliyoitoa hi leo Mjini New York Marekani Guterres amesema “Nimeshtushwa sana na mauaji ya wafanyakazi hao, hii haikubaliki kabisa na ni ukiukwaji wa kutisha wa sheria za kimataifa za haki za kibinadamu. Wahusika lazima wapatikane na waadhibiwe vikali.” 

Pia Guterres ametuma salamu za pole na mshikamano kwa washirika wa Umoja wa Mataifa, watoa huduma ya misaada ya kibinadamu ambao wanahatarisha maisha yao kwa kutoa ulinzi na unafuu kwa watu wa Tigray.

 

    Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN naye alaani Mauaji hayo 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachellet akiwa Geneva Uswisi amelaani mauaji ya wafanyakazi hao na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike. 
“Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na haki za binadamu ni raia pia kwahiyo kamwe hawawezi kulengwa kamwe mapigano. Pande zinazohusika kwenye mizozo ni lazima ziheshimu mikataba ya kimataifa ya haki za kibinadamu na haki za watoa misaada ya kibinadamu.”  
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa hii leo amesema mauaji haya ya kushangaza yanakuja wakati wanaendelea kupokea ripoti za ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu huko Tigray. “kuna haja ya kufanya uchunguzi kwa wakati unaofaa, kwa uwazi na kwa kina juu ya mauaji ya wenzetu wa masuala ya kibinadamu na kutoa ripoti zote za ukiukwaji wa haki za binadamu na wahusika lazima wawajibishwe” amesisitiza Bachellet
 

Mwanamke akipokea dawa katika kituo cha afya huko Tigray nchini Ethiopia
© UNICEF/Mulugeta Ayene
Mwanamke akipokea dawa katika kituo cha afya huko Tigray nchini Ethiopia

 

    Taarifa ya kuuwawa 

Hapo jana Rais wa Shirika la MSF, Christos Christou kupitia tovuti ya shirika hilo alitoa taarifa hiyo ya kuhuzunisha ikionesha namna wafanyakazi wake walivyo uwawa ambayo imesema “Maria Hernandez ambaye alikuwa ni Mratibu wa dharura, Yohannes Halefom Reda ambaye alikuwa ni Mratibu msaidizi na Tedros Gebremariam Gebremichael ambaye alikuwa ni deriva, walikuwa wakisafiri tarehe 24 juni alasiri wakati walipo poteza mawasiliano nao. Asubuhi ya tarehe 25 juni, gari lao lilipatikana tupu na mita chache umbali, wakakuta miili yao wakiwa wameshauwawa.”
Taarifa hiyo imesema hakuna maneno yanayoweza kufikisha ujumbe wa huzuni waliyonayo, Mshtuko na hasira dhidi ya shambulio hilo baya. Na pia hakuna maneno yanayoweza kutuliza maumivu ya familia za wafiwa na mateso ya familia zao ambao wamewapa pole.
“Tunalaani shambulio hili kwa wenzetu kwa maneno yenye nguvu Kali zaidi na tutahakikisha tunapambana kuelewa kilichotokea. Maria, Yohannes na Tedros wlaikuwa huko Tigray wakitoa msaada wa watu, na haiingii akilini kuwa malipo yake ni kutoa Uhai wao. Tunatuma salamu za rambirambi kwa familia zao na tunaomba watu wote tuheshimu faragha kwa familia za wafiwa katika kipindi huki kigumu sana.” 
   

      Salamu za Rambirambi 

Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula- WFP David Beasley kupitia mtandao wake wa Twitter na Facebook amelaani mauaji hayo na kutuma salamu za pole kwa wafiwa, ndugu na marafiki katika kipindi hiki kigumu. 
“Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa WFP duniani tunatuma sala zetu na salamu za pole kwa wafanyakazi wa Shirika la Madaktaru wasiokuwa na Mipaka kwa mauaji ya kikatili wakati wakijaribu tu kusaidia wengine wnaohitaji sana msaada” 


Salamu za pole pia zimetumwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Maraifa la kuhudumia wahamiaji -IOM Antonio Vitorino  “Tumeshtushwa sana na mauaji ya wafanyakazi wa MSF huko Tigray ambao wlaikuwa wakihudumia watu walio katika mazingira magumu zaidi. Salamu zetu za rambirambi ziende kwa familia zao, marafiki na wafanyakazi wenzao. IOM inalaani kwa maneno makali kulenga wahudumu wa misaada katika mizozo”