Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Kumekuwa na ongezeko la watu wazima wanaotumia dawa za kulevya.

Tutumie takwimu za kisayansi kupambana na matumizi ya Dawa za Kulevya: Guterres

Unsplash/Cristian Newman
Kumekuwa na ongezeko la watu wazima wanaotumia dawa za kulevya.

Tutumie takwimu za kisayansi kupambana na matumizi ya Dawa za Kulevya: Guterres

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres ameziasa nchi wanachama kuhakikisha zinatumia takwimu zinazotolewa na wanasayansi katika kufanya maamuzi yao ili kuokoa maisha ya wananchi wengi zaidi akitolea mfano namna sayansi ilivyoweza kuleta afueni kwenye mapambano ya janga la Corona au COVID-19.


Kupitia ujumbe wake wa Siku ya kimataifa ya udhibiti wa dawa ya Kulevya na kuzuia usafirishaji haramu akiwa mjini New York Marekani Guterres amesema, ingawa maambukizi ya virusi vya ukimwi yamepungua lakini takwimu za watu wanaotumia dawa za kulevya hazijapungua.
“Ripoti mpya iliyotolewa wiki hii na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Madawa na Uhalifu – UNODC imeonesha vifo vitokanavyo na matumizi ya dawa za kulevya vimeongezeka katika muongo uliopita. Maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kwa watu wazima duniani kote yamepungua kwa miaka ya hivi karibuni, lakini sio kwa watu wanaojichoma dawa za kulevya, ambao wanafikia asilimia 10 ya waathirika wapya kwa mwaka 2019. “
Guterres amesema ingawa nchi zinashirikiana kudhibiti usafirishaji haramu wa dawa za kulevya lakini nchi nyingi zenye kipato cha chini zina mifumo dhaifu ambayo inaruhusu biashara hiyo kuendelea. Pia amegusia suala la dawa zinazo dhibitiwa matumizi yake.
“kuna utofauti mkubwa sana kwenye nchi zenye kipato cha chini na cha kati katika suala la upatikanaji wa dawa muhimu zinazodhibitiwa. Kwa mfano, wataalamu wa matibabu Afrika Magharibi na Kati katika mwaka 2019 walikuwa na wanatoa dozi 4 za dawa za maumivu kila siku kwa wakazi Milioni Moja, Wakati Amerika ya Kaskazini idadi ya vipimo ilikuwa karibu 32,000”
Pia ameshauri vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka wahusika wakuu wa usafirishaji wa dawa za kulevya badala ya kuwakamata tuu watumiaji iwapo wanataka kumaliza tatizo hili katika nchi zao. 
Katibu Mkuu Guterres amezihimiza nchi wanachama kutumia takwimu kutafuta suluhu, “uwepo wa takwimu bora utasaidia kutambua mwenendo na kuwezesha ufuatiliaji wa wakati halisi wa njia za usafirishaji zinazohama haraka. Mifumo ya kutoa tahadhari mapema ya kisayansi itasaidia kutabiri vitisho vitakavyo ibuka vya dawa za kulevya” 

 

Mtumiaji wa mihadarati akitumia dawa  mbadala kwa ajili ya kuondowa hamu ya mihadarati
Picha/IRIN/Sean Kimmons
Mtumiaji wa mihadarati akitumia dawa mbadala kwa ajili ya kuondowa hamu ya mihadarati

 

   Ripoti ya UNODC imesemaje?

 


Mapema wiki hii Mkurugenzi mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusikana Madawa na Uhalifu – UNODC Ghada Waly alitoa ripoti iliyoonesha idadi ya watu wanaotumia mihadarati duniani imeongezeka na kwamba mwaka 2020 pekee duniani kote watu milioni 275 walitumia mihadarati ikiwa ni ongezeko la asilimia 22. 
Waly amesema sasa wanaendesha kampeni ya #Onesha Takwimu za dawa za kulevya. Okoa Maisha kwakuwa takwimu za watumiaji wa dawa hizo haramu wanapoteza maisha na kuondoa nguvu kazi ya dunia inazidi kuongezeka. 


“Zaidi ya watu milioni 36 wamepata shida kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya, dawa hizi zimesababisha vifo vya takriban watu nusu milioni kwa mwaka 2019. Kampeni hii inalenga kuelimisha Umma, watoa maamuzi na wahudumuwa afya umuhimu wa kufanya maamuzi kwa kutumia takwimu halisi zinazo onesha ukubwa wa tatizo” amesema Mkurugenzi huyo mtendaji wa UNODC


 Pia mkurugenzi huyu amesisitiza umuhimu wa nchi kufanya maamuzi ya kudhibiti kwa kutumia taarifa na takwimu za kisayansi ili waweze kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya ambayo kwa upande wa watumiaji wake kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi hayajapungua. 
“Tufanye habari zilizo hakikiwa kuwa ndio mshirika wetu wakati huu tunapo shughulikia changamoto za dawa za kulevya ulimwenguni na tufanye uwajibikaji wa pamoja wakati tukiwa na maono ya kuhakikisha kila mmoja wetu anakuwa na afya njema”