Ripoti ya FAO yaangazia vitisho dhidi ya mifumo ya chakula ya watu wa asili 

25 Juni 2021

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, pamoja na kituo cha kimataifa cha utafiti wa kilimo kwa nchi za kitropoki, CIAT,  wametoa leo utafiti mpya unaotambulisha mamia ya aina mbalimbali za mimea na wanyama ambazo watu wa asili ulimwenguni wanategemea na kutunza ili kuzalisha chakula endelevu na kuongeza baiyonuai na pia wametoa onyo la kuongezeka kwa vitisho dhidi ya mifumo hii ya ya chakula. 

Ripoti hiyo iliyopewa jina la Mfumo wa Chakula wa Watu wa Asili, Maarifa ya uendelevu na uthabiti kutoka kwa mstari wa mbele wa mabadiliko ya tabianchi, imezinduliwa leo Ijumaa. 

"Watu wa asili wamekuwa siku zote wavumbuzi mahiri, wakijifunza kutoka kwa kila mmoja na kutengeneza njia ya kimfumo, kwa kuzingatia uchunguzi." amesema Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu. 

"Lazima tushirikiane nao, ili kujifunza na kuunda maarifa kwa wanadamu wote." Qu ameongeza.  

Takribani watu milioni 500 katika nchi zaidi ya 90 wanajitambulisha kama Watu wa asili, na maarifa ya jadi ya kipekee yanayotoa fursa nyingi za uhakika wa chakula na uhifadhi ulio usalama. Mifumo nane ya chakula ya watu wa kiasili huchunguzwa kwa kina na kuwekwa wazi kuwa kati ya mifumo endelevu zaidi ulimwenguni.  

FAO inasema watu wa asili wanazalisha mamia ya bidhaa za chakula kutoka katika mazingira bila kumaliza maliasili na kufikia viwango vya juu vya kujitosheleza. Kwa visiwa vya Solomon, kwa mfano watu wa MelanesiansSI wanachanganya kilimo cha misitu, kukusanya chakula cha mwituni na uvuvi ili kuzalisha asilimia 70 ya mahitaji yao ya lishe. Katika eneo la Aktiki yaani eneo la baridi nchini Finland, kupitia uvuvi, uwindaji na ufugaji, watu wa Inari Sámi hutoa asilimia 75 ya protini wanayotumia. 

“Leo mifumo hii iko katika hatari kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na upanuzi wa shughuli mbali mbali za viwanda na biashara.” Imeeleza ripoti. 

Ripoti mpya inawakilisha kazi ya ushirikiano na utafiti katika maeneo husika kwa kushirikianma na mashirika ya watu wa asili na vituo vya utafiti kote ulimwenguni. Waandishi wa ripoti wanasisitiza hitaji la dharura la Serikali na jamii ya kimataifa kuanzisha na kutekeleza sera za kitamaduni ambazo zinaunga mkono juhudi za watu wa kiasili kulinda mifumo yao ya chakula. 

"Licha ya kuishi kwa karne nyingi, mifumo ya chakula ya watu asili inaweza kutoweka katika miaka ijayo kwa sababu kadhaa zinazotishia maisha yao ya baadaye," Amesisitiza Juan Lucas Restrepo, Mkurugenzi Mkuu wa CIAT kisha akaongeza akisema, “watafiti lazima wasikilize na kujifunza kutoka kwao kuunga mkono juhudi za kudumisha maarifa ya mababu.” 

Mifumo ya chakula ya watu wa asili iliyochanganuliwa katika chapisho hili ni pamoja na ile ya watu wa Baka nchini Cameroon, watu wa Inari Sami huko Finland, Khasi, Bhotia na Anwal nchini India, watu wa MelanesiSI katika Visiwa vya Solomon, watu wa Kel Tamasheq nchini Mali. , watu wa Tikuna, Cocama na Yagua huko Colombia, na Maya Ch'orti 'huko Guatemala. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter