Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
WFP imesema watu Milioni 41 duniani, ikiwemo Nigeria ( Kwenye Picha) wapo kwenye Hatari ya kukumbwa na baa la njaa

Tusaidie watu wenye Njaa kabla hatujaanza kutoa takwimu za waliokufa: WFP

UNOCHA/Eve Sabbagh
WFP imesema watu Milioni 41 duniani, ikiwemo Nigeria ( Kwenye Picha) wapo kwenye Hatari ya kukumbwa na baa la njaa

Tusaidie watu wenye Njaa kabla hatujaanza kutoa takwimu za waliokufa: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula David Beasley ameonya kwamba njaa  imeshaingia katika baadhi ya nchi na itaendelea kuathiri mamilioni ya watu iwapo hakuna msaada wa haraka utakaopatikana kuwasaidia wanaokabiliana na baa la njaa, na familia zisizofikika  kutokana na migogoro. 

Akihutubia mkutano wa bodi ya WFP Beasley amesema anavunjika moyo kwa kile wanachokabiliana nacho na anapata hofu kubwa akitolea mfano mwaka 2011 nchini Somalia ambako watu 260,000 walikufa kwa njaa, na wakati taarifa za baa la njaa zinatangazwa rasmi nusu ya watu walikuwa wameshakufa, nakusema hatuwezi kuendelea na majadiliano ya idadi ya wanaokufa  wakati watu wanahitaji msaada.
”Idadi ya watu walio kwenye mzunguko wa njaa inaongezeka kila tunapofunga macho na kufumbua, njaa imeongezeka kutoka makadirio ya watu milioni 34 mwanzoni mwa mwaka huu hadi milioni 41 kufikia mwezi Juni. Bila msaada wa dharura wa chakula mshtuko mdogo tuu ukitokea utatusukuma kwenye hali mbaya ya njaa”
Tathmini iliyofanyika hivi karibuni kuonesha watu 584,000 tayari wanakabiliwa na hali ya njaa huko nchini Ethiopia, Madagascar, Sudan Kusini na Yemen. 
Nigeria na Burkina Faso pia zinawasiwasi sana kwa sababu miezi ya hivi karibuni kumekuwa na mfumuko wa watu katika kiwango cha daraja la 5 la vipimo vya njaa au  IPC.
Uchunguzi wa WFP pia umebaini ongezeko la njaa kali kutoka watu milioni 27 mwaka 2019 mpaka Watu milioni 41 mwaka huu 2021 na imeonesha kuwa nchi 43 zipo kwenye hatihati ya kupata njaa iwapo tu kitu chochote kitawashtua na kuathiri nchi zao. 
“Nataka kusisitiza jinsi hali ilivyo mbaya huko nje. Leo watu milioni 41 njaa inabisha hodi kwenye milango yao. Gharama ya kuwafikia inakaribia dola za Marekani bilioni 6, tunahitaji ufadhili na tunauhitaji sasa” amesisitiza Beasley
Kuyumba kwa uchumi, migogoro na hali mbaya ya hewa vimechangia kuongezeka kwa njaa lakini pia ongezeko la bei vya vyakula mwaka huu pia ni moja ya vichocheo. Bei ya mahindi duniani imepanda kwa 90% kwa mwaka huu huku bei ya ngano ikiongezeka kwa takriban 30%.
TAGS: Njaa, ukame, misaada ya kibinadamu, WFP, David Beasley