UNESCO na WHO zinahimiza nchi kufanya kila shule kuwa shule ya kuchagiza afya.

UNESCO na WHO zinahimiza nchi kufanya kila shule kuwa shule ya kuchagiza afya.
Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, leo limezindua viwango vya kimataifa kwa shule zinazochagiza afya, ambacho ni kifurushi cha rasilimali kwa shule kuboresha afya na ustawi wa watoto na vijana bilioni1.9 wa umri wa shule.
Shirika hilo linasema kufungwa kwa shule nyingi duniani wakati wa janga la corona au COVID-19 kumesababisha usumbufu mkubwa kwa elimu.
Wanafunzi wanaokadiriwa kuwa milioni 365 wa shule ya msingi walilazimika kuwa bila mlo shuleni na hivyo kuongeza viwango cha mafadhaiko, wasiwasi na maswala mengine ya afya ya akili.
"Shule zina jukumu muhimu katika ustawi wa wanafunzi, familia na jamii zao, na uhusiano kati ya elimu na afya haujawahi kuonekana muhimu zaidi kama sasa," amesema Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani WHO.

Ameongeza kuwa "Viwango hivi vipya vilivyozinduliwa duniani ili kuunda shule ambazo zinakuza elimu na afya, na ambazo zinawapatia wanafunzi maarifa na ustadi wa afya na ustawi wa mustakbali wao wa baadaye, kuajiriwa na matarajio ya maisha."
Kulingana na orodha ya viwango vinane vya kimataifa, kifurushi hicho cha rasilimali kinakusudia kuhakikisha shule zote zinakuza na kuchagiza stadi za maisha, ujuzi wa utambuzi na wa kijamii na mitindo ya maisha bora kwa wanafunzi wote.
Viwango hivi vya kimataifa vitajaribiwa katika nchi za Botswana, Misri, Ethiopia, Kenya na Paraguay.
Mpango huo unachangia lengo lengo la maendeleo namba 13 la mpango mkuu wa kazi wa WHO wa 'kufanya maisha ya watu bilioni 1 kuwa na afya bora' ifikapo mwaka 2023 na ajenda ya elimu ya mwaka 2030 inayoratibiwa na UNESCO.
Mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azouley amesema "Elimu na afya ni haki za msingi za binadamu zinazotegemeana kwa wote, katika msingi wa haki yoyote ya binadamu, na muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Shule ambayo haihusishi afya haifai tena na haikubaliki. Natoa wito kwa sisi sote kuthibitisha kujitolea na jukumu letu, kuifanya kila shule kuwa shule ya kuchagiza afya ”.

Viwango vya kimataifan vinatoa rasilimali kwa mifumo ya elimu kusaidia kukuza afya na ustawi kupitia utawala bora.
UNESCO na WHO zitashirikiana na serikali kuwezesha nchi kubadilisha mfumo na kwenda sanjari na kifurushi hiki kwa muktadha wa mazingira yao maalum. Ushahidi uko wazi. Programu kamili za afya na lishe shuleni zina athari kubwa nzuri kati ya watoto wenye umri wa kwenda shule. Kwa mfano:
• Shule kuwa na njia za kiafya na lishe kwa wasichana na wavulana katika maeneo ya kipato cha chini ambako minyoo na upungufu wa damu huenea kunaweza kuchangia miaka 2.5 zaidi ya watoto kuwa shuleni
• Njia za kuzuia malaria zinaweza kusababisha kupunguzwa kwa utoro kwa asilimia 62%.
• Lishe bora shuleni huongeza viwango vya uandikishaji wa shule kwa asilimia 9% kwa wastani, na mahudhurio kwa asilimia 8%; wanaweza pia kupunguza upungufu wa damu kwa wasichana wa vijana hadi kwa asilimia 20%.
• Kuchagiza kunawa mikono kunapunguza utoro kwa sababu ya magonjwa ya tumbo na upumuaji kwa asilimia 21% -61% katika nchi zenye kipato cha chini.

Upimaji wa bure na miwani ya macho vimesababisha ongezeko la asilimia 5% la wanafunzi wanaofaulu mitihani sanifu katika kusoma na hisabati.
• Elimu kamili ya jinsia inachagiza kuzingatia tabia njema, inakuza afya ya uzazi na masuala ya ngono napia haki, na inaboresha matokeo ya afya ya jinsia na uzazi kama vile kupunguza maambukizi ya VVU na viwango vya ujauzito katika umri mdogo.
• Kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira (WASH) shuleni, pamoja na maarifa juu ya usafi wa hedhi, huwaandaa wasichana kudumisha usafi wa mwili na afya zao kwa heshima, na kunaweza kupunguza idadi ya siku za shule ambazo wasichana wanakosa wakati wa hedhi.
Mtazamo wa kuchagiza afya mashuleni ilielezwa kwanza na WHO, UNESCO na UNICEF mnamo 1995 na kupitishwa katika nchi zaidi ya 90.
Lakini, ni nchi chache tu ambazo zimetekeleza kwa kiwango kikubwa, na hata wachache wamebadilisha mifumo yao ya elimu kujumuisha kukuza afya.
Viwango hivi vipya vya kimataifa vitasaidia nchi kujumuisha kukuza afya katika shule zote na kuinua kiwango cha afya na ustawi wa watoto wao.