Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaonya juu ya hatari ya pengo la chanjo kwa wasio na utaifa

Kombo Asuman Kombo na familia yake, alihudhuria warsha ya kutokuwa na utaifa
© UNHCR/Roger Arnold
Kombo Asuman Kombo na familia yake, alihudhuria warsha ya kutokuwa na utaifa

UNHCR yaonya juu ya hatari ya pengo la chanjo kwa wasio na utaifa

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limeonya leo kwamba watu wengi wasio na utaifa duniani wanaweza kukosa chanjo kutokana na kukosa uraia uraia uthibitisho wa kitambulisho. 

 Akizungumzia hali hiyo mkuu wa masuala ya ulinzi wa kimataifa wa UNHCR Gillian Triggs amesema  “Kuna mamilioni ya watu wanaojulikana kuwa  hawana utaifa kote ulimwenguni, bila utaifa wa nchi yoyote. Hii ina athari kubwa kwa haki zao za kimsingi za binadamu, na sasa wanaweza pia kutengwa katika kupata chanjo za kuokoa maisha.” 
Katika ripoti yake ya hivi karibuni juu ya athari za COCID-19 kwa idadi kubwa ya watu wasio na uraia au utaifa , shirika linabainisha kuwa mipango mingi ya kitaifa ya chanjo haitoi ufafanuzi juu ya chanjo kwa watu wasio na utaifa. 

UNHCR inaonya kuwa watu wengi ambao hawana utaifa au nyaraka za kitambulisho watatengwa isipokuwa tu endapo mataifa yatafanya juhudi fulani kuwafikia na kushughulikia changamoto maalum ambazo wanaweza kukabiliwa nazo.  
Ripoti hiyo mpya inatoa mapendekezo na mifano ya mazoea mazuri ya serikali katika suala hili, ikiwa ni pamoja na kukubali aina mbadala za uthibitisho wa utambulisho wa mtu. 
"Kwa nia ya kulinda maisha ya watu na kuhakikisha afya ya umma, mipango ya chanjo ya kitaifa lazima itekelezwe kwa njia jumuishi iwezekanavyo. Kwa kuzingatia kuwa watu wengi wasio na utaifa tayari wanakabiliwa kutojumuishwa na kutengwa, hivyo vizuizi vya ufikiaji huduma lazima vishughulikiwe na uzingatiaji maalum utolewe kwa hali yao, "amesema Triggs. 

Baada ya safari ngumu na ya machungu baharini, mkimbizi mrohingya kutoka Myanmar (kulia) ameungana tena na dada yake (katikati) katika jimbo la Aceh nchini Indonesia
© UNHCR/Jiro Ose
Baada ya safari ngumu na ya machungu baharini, mkimbizi mrohingya kutoka Myanmar (kulia) ameungana tena na dada yake (katikati) katika jimbo la Aceh nchini Indonesia

Tangu mwanzo wa COVID-19 wasio na utaifa wanatengwa 

Tangu mwanzo wa janga hilo, watu wengi wasio na utaifa wanaendelea kukabiliwa na shida katika kupata huduma za afya na huduma za kijamii.  
Wengi wanaweza kuogopa kujitokeza kupimwa au kutibiwa kwa sababu ya kutokuwa na haki ya kisheria , ambayo inaweza kuwaweka katika hatari ya kuzuiliwa au kufukuzwa nchini.  
Gharama ya matibabu, pamoja na chanjo, inaweza pia kuwa kikwazo kwa watu wasio na utaifa, kwani kawaida hazichangiwi na miradi ya kitaifa, ya huduma ya afya. 
UNHCR, ambayo ina wajibu rasmi la Umoja wa Mataifa la kuzuia na kupunguza idadi ya watu wasio na utaifa, na kuwalinda watu wasio na utaifa, inasema idadi ya watu wa duniani kote wasio na utaifa ni angalau watu milioni 4.2 katika nchi 94. Kwa sababu ya hali ya kutokuwa wazi ya suala hili, takwimu halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi. 

Serikali ya Kenya imetoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 600 kutoja jamii ya Washona, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwalinda na hatua ya kwanza kuelekea kumaliza tatizo la utaifa kwa watu 3,500 nchini humo.
UNHCR KENYA/Rose Ogolla
Serikali ya Kenya imetoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 600 kutoja jamii ya Washona, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwalinda na hatua ya kwanza kuelekea kumaliza tatizo la utaifa kwa watu 3,500 nchini humo.

Changamoto za kusajili wanaozaliwa ni hatari 

Zaidi ya mwaka mmoja tangu kuzuka kwa janga la COVID-19, UNHCR pia inaonya kwamba usumbufu katika huduma za usajili wa kuzaliwa unasababisha hatari mpya za ukosefu wa utaifa. 
Huku nchi kadhaa zikiwa zimesimamisha huduma za usajili wa raia kutokana na janga hilo, usajili wa kuzaliwa ambao ni muhimu katika kuhakikisha ustahiki wa utaifa umeathiriwa. 
Shirika hilo la wakimbizi linasema nchi ambazo huduma za usajili wa kuzaliwa zilisimamishwa kwa sehemu au zote sasa zinaripoti viwango vya chini vya usajili wa kuzaliwa na vile vile wako nyuma katika kushughulikia suala hilo.  
Kampeni zinazolenga kusajili watoto wanaozaliwa katika maeneo ambayo ni magumu kuyafikia walio hatarini kutokuwa na utaifa pia zimesimamishwa katika mazingira mengi. 
Hatari za ukosefu wa utaifa zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa vikundi vya watu wachache ambao ndio idadi kubwa ya watu wasiojulikana na wasio na utaifa.