Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wajumuishwa vyema kule walikokimbilia

Wakimbizi wa Burundi waishio Tanzania wakiwa na mabango yao wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani katika kambi yao ya Mtendeli mkoani Kigoma.
UNHCR/Magdalena Kasubi
Wakimbizi wa Burundi waishio Tanzania wakiwa na mabango yao wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani katika kambi yao ya Mtendeli mkoani Kigoma.

Wakimbizi wajumuishwa vyema kule walikokimbilia

Wahamiaji na Wakimbizi

Siku ya kimataifa ya wakimbizi duniani imeadhimishwa duniani kote tarehe 20 mwezi huu wa Juni. Maadhimisho haya yanafanyika wakati hivi sasa kuna zaidi ya watu milioni 80 duniani kote ambao wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na vita, ghasia na mateso na hivyo kujikuta wameacha kila kitu. 

 

Tweet URL

Hii ina maana wanatakiwa waanze maisha mapya ugenini, iwe ndani ya nchi yao au nje ya nchi. Ni kwa kuzingatia hilo ujumbe wa siku ya wakimbizi duniani mwaka huu ni Kwa pamoja tunaponya, tunajifunza na tunang’aa! Kinachomulikwwa ni kwa vipi kule walikoenda wanapata huduma za afya, elimu na michezo? Hicho ndicho msingi wa mada kwa kina yetu hii leo ikimulika zaidi ujumuishaji wa wakimbizi kwenye michezo na afya. 

Mada yetu imeanzia katika utambulisho wa timu ya wakimbizi itakayoshiriki mashindano ya olimpiki ya TOKYO 2020 yanayoanza mwezi ujao.

Miongoni mwao ni Rose Lokonyen, Paulo Amotun kutoka Kenya. Angelina Nadai na James Nyak kutoka Sudan Kusini bila kusahau Dorian Kalatela kutoka Congo-Brazaville.
Aliyetangaza ni Rais wa kamati ya kimataifa ya olimpiki Thomas Bach kutoka Geneva Uswisi huku wanariadha wakiwa maeneo mbalimbali wakipata matokeo hayo kwa njia ya mtandao.
Jumla ya wakimbizi 25 walifuzu kujiunga na timu hiyo kati ya 56 waliokuwa wanajiandaa kwa mazoezi. Baada ya kutangazwa wakaulizwa hisia zao..

Watoto wakimbizi wakicheza katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Fourkoloum magharibi mwa nchi hiyo.
UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakimbizi wakicheza katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Fourkoloum magharibi mwa nchi hiyo.

Wanasema Asante sana! Asante Sana! Nashukuru Mno! Nina furaha mno! Nataka kulia!!!

Ndipo Bwana Basch akamweleza, “lia! Usizuie hisia zako! Unajua kama mwanamichezo kila wakati ni vizuri kuachia hisia zako na kwa njia hiyo, ili roho yako iwe huru kwa ajili ya mashindano na utendaji wako kimichezo.”

Hii ni mara ya pili kwa timu ya wakimbizi kushiriki michezo ya Olimpiki. Mara ya kwanza ilkuwa Rio De Janeiro nchini Brazil mwaka 2016 kiongozi wa msafara akiwa mwanariadha nguli, Tegla Loroupe kutoka Kenya ambaye pia ndiye anaongoza msafara huo mwaka huu. Bi. Loroupe ambaye mwaka 2016 alipata tuzo ya Umoja wa Mataifa hakuficha furaha yake baada ya uteuzi wa timu ya wakimbizi atakayoongoza na kuahidi ya kwamba. “Kama mwanariadha mstaafu, naamini nitaweza kusaidia wanamichezo wetu wote kutoka mabara matano ya dunia, nitabadilishana nao uzoefu kwa kuzingatia mimi mwenyewe nilikotoka hadi nilipo sasa. Wanamichezo hawa waliochaguliwa na IOC, siyo tu watajiwakilisha wenyewe au IOC bali pia wakimbizi duniani kote.”

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi akaulizwa hatua hii ya wakimbizi kwenda olimpiki kuna maana gani na ndipo akasema, “Ina maana kwamba inaonesha wakimbizi vijana wana uwezo wa kushindana. Inatoa matumaini kwa wakimbizi wote, na pia inatuma ujumbe chanya kwa jambo ambalo mara nyingi ni gumu na tata.”

Soundcloud

Na kisha akawaambia kwamba “Muwakilishe na muwafanye mamilioni na mamilioni ya wakimbizi duniani kote ambao watakuwa wanatazama wajivunie kile mtakachofanikisha.”

Ujumuishaji si katika michezo pekee bali pia kwenye huduma za afya ambako huko nchini Uganda, kumekuwepo na ongezeko la asilimia 70 la wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Idadi kubwa ni wanawake na watoto na hivyo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, linahakikisha chanjo muhimu kama vile polio na surua zinapatiwa wajawazito na watoto wa wakimbizi na wenyeji wao.

Jennifer Atieno mwenye umri wa miaka 7 akiwa amekumbatia paka wake karibu na makazi duni ya Kibera jijini Nairobi, Kenya.
UNICEF/Sigfried Modola
Jennifer Atieno mwenye umri wa miaka 7 akiwa amekumbatia paka wake karibu na makazi duni ya Kibera jijini Nairobi, Kenya.

Yakobo Kahesi ni mratibu wa shirika la kiraia la African Humanitarian Action linalopatiwa msaada na UNICEF.

Bwana Kahesi anasema, “UNICEF imechukua hatua sahihi, imeongeza idadi ya chanjo iliyokuwa inatupatia ili watu wote wapatiwe. Wametupatia pia jokofu kubwa ili ubaridi uwe sahihi. Msaada wa UNICEF unatuhakikishia ubora wa huduma zetu na hii ni hakikisho kwa wanufaika wetu ya kwamba wanapata chanjo wanazotakiwa kupata na kwa wakati sahihi.”

Huko Tanzania hususan mkoani Kigoma katika kambi ya wakimbizi ya Mtendeli kulifanyika maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyoambatana na mechi mpira wa miguu kati ya wakimbizi na wenyeji wao wa Kakonko na wakimbizi waliibuka washindi. 

Baada ya hapo elimu jumuishi. Wanafunzi viziwi wakaonesha ujuzi wao wa kufanya hesabu mwalimu akifundisha kwa lugha ya alama na hii ikathibitisha kuwa ujumuishi wa wakimbizi katika nchi wanakokimbilia ni jawabu la kustawi kwa pamoja.