Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika n'gwe yake ya mwisho Guterres aahidi mshikamano na kuondokana na COVID-19

António Guterres (kulia) akila kiapo cha kuwa Katibu Mkuu wa UN kwa kipindi cha pili mbele ya Rais wa mkutano wa 75 wa  Baraza Kuu la UN Volkan Bozkir.
UN/Eskinder Debebe
António Guterres (kulia) akila kiapo cha kuwa Katibu Mkuu wa UN kwa kipindi cha pili mbele ya Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN Volkan Bozkir.

Katika n'gwe yake ya mwisho Guterres aahidi mshikamano na kuondokana na COVID-19

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Ijumaa ameteuliwa tena kuendelea na wadhifa huo wa Ukatibu Mkuu kwa kipindi cha pili, akiahidi kwamba kusaidia dunia kuondokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 kuwa ndio kipaumbele chake.

Akila kiapo ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mbele ya Rais wa Baraza hilo Volkan Bozikir na wawaklishi wa nchi wanachama, Bwana Guterres amesema anatambua dhamana kubwa aliyobeba katika kipindi hiki muhimu zaidi duniani.

Dunia iko njiapanda

“Hakika tuko katika njiapanda, tukikabiliwa na maamuzi yatakayokuwa na athari kwetu. Mienendo inabadilika. Kanuni za awali zinabadilishwa,“ amesema Guterres akiongeza kuwa “tunaandika historia yetu wenyewe kwa maamuzi tunayopitisha hivi sasa. Inaweza kuwa pande zozote: kuvunjika na kusongesha majanga au kusonga na kuleta matumaini kwa mustakabili usioharibu mazingira na bora kwa kila mtu. Kuna sababu za kuwa na matumaini.”

Bwana Guterres alikuwa mgombea pekee kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Awamu yake ya kwanza ilianza mwezi Januari mwaka 2017.

Aliteuliwa na nchi yake Ureno na kupitishwa kwa kauli moja na Baraza Kuu kabla ya idhinisho kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kushika wadhifa huo kwa awamu ya pili kuanzia Januari 2022 hadi Desemba 2026.

Tweet URL

Kubadili mwelekeo 

Akitoa hotuba yake kwa lugha za kiingereza, kifaransa na kispanyola ambazo ni lugha miongoni mwa lugha sita rasmi za Umoja wa Mataifa, Guterres amechambua jinsi COVID-19 imesababisha vifo, imesambaratisha mbinu za kujipatia kipato huku ikifichua ukosefu wa usawa. Na wakati huo huo nchi zinakabaliwa na changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa bayonuai.

Amesema ni muhimmu sana kuondoakana na janga la Corona, na wakati huo huo mwelekeo wa kujikwamua kiuchumi na kijamii unapaswa kufanyika katika misingi ya haki.

“Changamoto yetu kubwa ambayo wakati huo huo ni fursa kubwa zaidi ni kutumia janga hili kubadili mwelekeo, kusonga kuelekea dunia iliyojifunza na inayosongesha haki, uchumi usioharibu mazingira kwa kuimarisha ushirikiano fanisi wa kimataifa na kushughulikia changamoto za kimataifa,” amesema Guterres.

Zama za mabadiliko

Wakati mwelekeo umekabiliwa na majukumu makubwa, Katibu Mkuu ameelezea imani yake kwamba yanaweza kutekelezwa kwa mafanikio makubwa kutokana na mambo kadhaa ikiwemo kujituma kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa duniani kote, lakini kukiambatana na umuhimu wa kuboresha kile wanachofanya sasa, kufanya uchambuzi wa kina wa takwimu na kupunguza urasimu usiokuwa wa lazima.

Ijapokuwa dunia imebadilika mno, ahadi za Umoja wa Mataifa zinasalia zile zile lakini nchi zinapaswa kushirikiana katika mbinu mpya ili ahadi hizo ziweze kutimizwa.

Ametoa wito kwa nchi kutumia fursa ya sasa ya mabadiliko wakati akisisitiza pia umuhiu wa kujumuisha sauti za makundi mengine kwenye meza ya mazungumzo yakiwemo mashirika ya kiraia, sekta binafsi na vijana.

Uwiano na usawa kwenye chanjo

“Hatma ya marekebisho ya sasa inapaswa kuwa ni mshikamano na usawa,” amesema Guterres akiongeza kuwa “lakini uwiano unahitaji kuanza sasa: Chanjo zinahitajika kupatikana kwa kila mtu kila mahali na lazima tuweke mazingira endelevu na jumuishi katika kujikwamua iwe kwa nchi zinazoendelea na zilizoendelea. Na hii ina safari ndefu.
Bwana Guterres ameonya kuwa nchi zinapaswa kukabiliana na nakisi ya sasa ya uaminifu iwapo hilo linatakiwa kufanikiwa.

“Sana sana tunahitaji kufanya kila kitu kukabiliana na mgawanyiko wa kimkakati wa dunia na mahusiano ya uthabiti wa kimataifa yasiyo na tija. Lazima yashughulikiwe moja kwa moja,” amesema Guterres.