Umoja wa Mataifa wajengea uwezo wakulima Dodoma nchini Tanzania

18 Juni 2021

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la chakula na kilimo, FAO nchini Tanzania linatekeleza kwa vitendo uamuzi wa umoja huo wa kutangaza mwaka huu wa 2021 kuwa mwaka wa mboga mboga na matunda kama njia ya kuelimisha watu kuhusu umuhimu na faida za mbogamboga na matunda kwa afya zao na pia kiuchumi. 
 

 

Wanakikundi 32 wakulima mkoani Dodoma wamekuwa wakilima mazao hayo katika eneo la ekari 31, lakini chini ya ufanisi. Sasa FAO imechukua hatua kwa  kuwapelekea msaada wa vifaa ikiwemo pembejeo.

Msaada ni mbegu bora na usafiri

Charles Tulahi Mwakilishi Msaidizi wa FAO nchini Tanzania amesema vifaa hivyo ni pamoja na mbegu za matunda na mboga mboga, mbolea na pikipiki vyote vikiwa na thamani ya dola elfu 17.

Akifafanua sababu za kupeleka mradi huo, Bwana Tulahi amesema wazo la mradi walipata kutoka halmashauri ya jiji la Dodoma, ambao walitambua kikundi cha Ilolo “na sisi tukaja hapa tukathibitisha ni kikundi kizuri na kina watu wanaojituma na wanashirikiana vizuri na sisi tukiwaunga mkono basi watakuwa mfano mzuri kwa jiji la Dodoma na mkoa mzima wa Dodoma na hivyo tunaweza kuchangia zaidi kwenye kuimarisha afya za wanajamii lakini pia katika kipato cha wahusika.”

FAO Tanzania imesema walibaini kuwa kikundi hicho cha wakulima cha Ilolo kilikuwa na changamoto ya mbegu na hivyo imewapatia mbegu bora ili katika msimu ujao wapande mbegu bora na kwa utalaamu na hivyo wapate mazao mengi zaidi na wafanikiwe zaidi.

“Halikadhalika afisa ugani anayehudumia kikundi hiki yuko mbali, tukaona ni vyema tumletee pikipiki ambayo tumeletea, ambayo itamwezesha kuhudumia kikundi hiki kwa ufanisi zaidi. Matarajio yetu ni kwamba watazalisha kwa ukubwa na wakipata elimu ya ujasiriamali na lishe bora wataweza kuboresha kipato na lishe yao na wataweza kufanya mambo makubwa ambayo wasingweza kufanya kwa kilimo walichokuwa wanafanya hapo awali,”  amefafanua Bwana Tulahi.

Tumepewa vitabu na mafunzo sasa kazi kwetu - Mkulima

Wilson Udoba, mkulima mwanakikundi akatoa shukrani akisema “ujio huu wa mradi huu wa mboga mboga na matunda, mimi binafsi nashukuru mno na napenda kutoa shukrani za dhati kwani umetuletea mambo mengi ambayo tutajifunza wanakikundi cha Ilolo tarafa ya Kikombo jiji la Dodoma.”

Lakini hali ilikuwa vipi kabla ya mradi? Martha Msihi ni mwanakikundi anasema ilikuwa si shwari kwa sababu “kabla ya mradi huu kuja tulikuwa tunamwagilia kwa madumu na madebe kwa kubeba kwa mikono na maji tulikuwa tunatumia gharama kubwa kwa kuchimba visima kwa gharama zetu. Lakini kuja huu mradi mambo yamekuwa rahisi tumeletewa maji na tunamwagilia kwa mpira. Maratarajio yetu kuwa mradi utaendelea ili tujikwamue kiuchumi. Tunashukuru sana na wasitusahau na pia wapelekee na wengine.”

Afisa kilimo wa kata ya Kikombo, Madey Gidarta kupitia mradi huu wa FAO amepatiwa pikipiki, ambapo anasema pikipiki hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa sababu mara nyingi katika ripoti zao usafiri umekuwa ni kikwazo kikubwa kutokana na eneo analosimamia kuwa ni kubwa. “Inaweza kuwa siyo kwamba changamoto zimetatuliwa kwa asilimia 100 lakini kwa kweli wametusaidia na kama unavyoona tayari tumeshaandaa mashimo kwa ajili ya kupanda mbegu bora.”

Kwa Peter Matata Mwenyekiti wa kikundi cha Ilolo shukrani kwake zaidi ni kwa serikali na FAO kwa kushirikiana na kuruhusu mradi huo huku akitoa ujumbe kwa wakulima akisema, “tunashukuru kwa kuwa tumepata vitabu na tutazingatia na kilimo hiki kitatukwamua.”

Na mkulima mwanakikundi Wilson Udoba, akaelekeza sauti yake kwa wakulima wenzake akisema tayari wamepatiwa elimu ya kilimo bora, wazingatie ushauri wa wataalamu na wazingatie vitabu ambavyo wamepatiwa ili wapate matunda na mboga mboga bora zaidi.
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter