Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 ni tishio kubwa kwa maisha na ustawi wa wakimbizi nchini Uganda:UNHCR/Benki ya Dunia 

Wakimbizi wa Sudan Kusini wakipimwa joto kabla ya kuingia kwenye kituo cha afya cha makazi ya wakimbizi ya Bodibidi nchini Uganda
© UNHCR/Esther Ruth Mbabazi
Wakimbizi wa Sudan Kusini wakipimwa joto kabla ya kuingia kwenye kituo cha afya cha makazi ya wakimbizi ya Bodibidi nchini Uganda

COVID-19 ni tishio kubwa kwa maisha na ustawi wa wakimbizi nchini Uganda:UNHCR/Benki ya Dunia 

Wahamiaji na Wakimbizi

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa kwa njia ya simu na  shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na Benki ya Dunia unaonyesha hali mbaya ya janga la corona au COVID-19 kwa maisha ya wakimbizi nchini Uganda na kudhihirisha haja ya kuimarishwa msaada kwa jamii za wakimbizi, ili kupunguza mateso yanayosababishwa na janga hilo. 

Utafiti huo unaonyesha kuwa wakimbizi nchini Uganda wamekuwa katika hali mbaya zaidin ya wenyeji katika upande wa masuala muhimu ya ustawi wa kijamii, kama ajira, uhakika wa chakula na afya ya akili.  

Matokeo haya ya utafiti yanaongezea rekodi ya UNHCR ya ongezeko la kutisha la idadi ya kujiua miongoni mwa wakimbizi, inayohusishwa na athari mbaya za janga la kijamii na kiuchumi. 

Joel Boutroue mwakilishi wa UNHCR Uganda amesema “Wakati janga hilo limeathiri jamii zote, wakimbizi wameathiriwa sana. Kukiwa na wimbi la pili la COVID-19 linaloendelea nchini Uganda, nina wasiwasi sana kwamba hali ya maisha ya wakimbizi inaweza sio kuzorota tu lakini kuwa mbaya zaidi.” 

Uganda inahifadhi wakimbizi wengi zaidi barani Afrika, ambapo milioni 1.5 wanatoka Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.  

Watoto wanastahili furaha na mazingira ya amani.
© UNHCR/Jordi Matas
Watoto wanastahili furaha na mazingira ya amani.

Hadi kufikia Machi 2021, viwango vya ajira kwa jamii hizi vilikuwa vimepungua hadi asilimia 32, ikiwa imeshuka kwa asilimia 24 ukilinganisha na nyakati za kabla ya amri ya kugfungwa kila kitu kujikinga na COVID-19. 

Tofauti na wenyeji baada kushuka kiwango cha ajira hapo awali, viwango vya ajira kwa jamii hizo za wenyeji viliweza kurudi tena kwenye viwango vya kabla ya janga la COVID-19. 

Nusu ya wakimbizi walioshiriki katika utafiti huo walidhaniwa kuishi chini ya mstari wa umaskini sasa ikilinganishwa na asilimia 44 iliyokuwepo kabla ya janga la COVID-19.  

Karibu asilimia 36 hawakuwa na fursa ya upatikanaji wa dawa wakati zinahitajika na hawakuweza kupata kiwango cha kutosha cha maji ya kunywa.

Anurith, mkimbizi kutoka DRC akisaka hifadhi Uganda.
VIDEO YA UNHCR
Anurith, mkimbizi kutoka DRC akisaka hifadhi Uganda.

Changamoto ya uhakika wa chakula  

 Kutokuwa na uhakika wa chakula miongoni mwa wakimbizi kunapimwa kutokana na kaya zilizoishiwa  chakula, na kiwango kilikuwa kikubwa zaidi kwa wakimbizi kuliko katika jamii za wenyeji (asilimia 64 kwa wakimbizi dhidi ya asilimia 9 kwa wenyeji).  

Wakimbizi walilazimika kupunguza kiwango na idadi ya milo kwa siku.  

Kulingana na takwimu za UNHCR mwenyewe, “njia hasi za kukabiliana na maisha kama kutoa ngono ili kuishi na ndoa za utotoni zilienea zaidi wakati wa janga la COVID-19 kwa sababu ya ugumu wa maisha wa kiuchumi na kupunguzwa kwa msaada wa chakula.” 

Mara mbili zaidi wakimbizi walilazimika kukopa pesa ili kukabiliana na dharura ya COVID-19 ikilinganishwa na jamii zilizowakaribisha.  

Sambamba na hilo ugumu wa maisha ulikuwa mara tatu kaya za wakimbizi ambazo hazikupokea msaada wowote wa kijamii kama vile uhamishaji wa pesa, msaada wa chakula na msaada mwingine muhimu katika mji mkuu, Kampala. 

Wakati huo huo, msongo wa mawazo uliathiri wakimbizi, mara kumi zaidi kuliko jamii iliyowakaribisha (asilimia 54 ya wakimbizi dhidi ya asilimia 5 ya wenyeji). 

Wakimbizi wa Sudan Kusini waliopo nchini Uganda
WFP/Henry Bongyereirwe
Wakimbizi wa Sudan Kusini waliopo nchini Uganda

Kwa upana zaidi, matokeo ya janga la COVID-19 yaliongeza hali ya kukata tamaa miongoni mwa wakimbizi.  

Uchunguzi tofauti wa UNHCR umebaini kwamba idadi ya jumla ya majaribio ya kujiua na kukamilika kati ya wakimbizi mwaka 2020 iliongezeka kwa asilimia 129 ikilinganishwa na 2019, na jumla ya visa 347 vya kujiua vilitokea mwaka jana.  

Takwimu za kujiua katika robo ya kwanza ya  mwaka 2021 zinatia wasiwasi vile vile na matukio 76 yamerekodiwa katika kipindi hicho, ikilinganishwa na matukio  68 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.  

Kesi nyingi zinawahusu wasichana walioathiriwa na unyanyasaji wa kijinsia wakati visa vya unyanyasaji wa kijinsia vimerekodiwa kuongezeka karibu mara mbili ikilinganishwa na robo ya kwanza ya 2020, na kufikia matukio 1,394.  

Ukosefu wa kipato na uhaba wa chakula ndani ya kaya za wakimbizi vimechangia kwa kiasi kikubwa matukio haya. 

UNHCR na wadau wanaendelea kusaidia 

Gugu-Mbatha-Raw akiwa ameketi na mkimbizi katika kituo cha wanawake kwenye makazi ya wakimbizi ya Nakivale nchini Uganda 2019
© UNHCR/Caroline Irby
Gugu-Mbatha-Raw akiwa ameketi na mkimbizi katika kituo cha wanawake kwenye makazi ya wakimbizi ya Nakivale nchini Uganda 2019

 Kwa kushirikiana na serikali, UNHCR na washirika wake wanaendelea kutoa ulinzi na msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi nchini Uganda, na kuunga mkono juhudi kuelekea mwitikio kamili wa wakimbizi.  

Ili kukabiliana na janga hilo, washirika wa kusaidia wakimbizi wameongeza juhudi mara mbili kuhakikisha mwendelezo wa huduma za kuokoa maisha na kupunguza athari za COVID-19. 

"Ninapongeza mtazamo wa Uganda  wa ujumuishi wa wakimbizi na natoa wito kwa jamii ya kimataifa kuzingatia kwa karibu mapungufu katika mahitaji ya kimsingi ya watu walio katika mazingira magumu," amesema Boutroue.  

 Ameongeza kuwa "Rasilimali zaidi zinahitajika kukidhi sio tu mahitaji ya msingi ya wakimbizi, pamoja na chakula na upatikanaji wa maji, lakini pia kutoa msaada bora kwa maisha ya kila siku, elimu na afya ya akili." 

UNHCR na Benki ya Dunia, pamoja na Ofisi ya takwimu ya Uganda, wamefuatilia athari za kiuchumi na kijamii za janga la COVID-19 kwa wakimbizi katika awamu tatu za utafiti wa kupitia simu mwezi Februari na Machi 2021.