Idadi ya wanaojifungua kwa njia ya upasuaji usio wa lazima inaongezeka:WHO 

17 Juni 2021

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO inasema kiwango cha wanawake kujifungua kwa njia ya upasuaji kinaongezeka duniani kwa idadi inayoashiria taratibu zisizo za lazima za kiafya na zinazoweza kuletya madhara. Flora nducha amefuatilia ripoti hiyo na kuandaa taarifa hii 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WHO suala la kujifunfua kwa njia ya upasuaji limeanza kuwa kama kitu cha kawaida duniani kote ambapo mwanamke 1 kati ya 5 sawa na asilimia 21% ya uzazi wote.  

Utafiti  wa ripoti hiyo imeonya kwamba idadi hii itaendelea kuongezeka kwa miaka kumi ijayo, na kufikia karibu theluthi  au asilimia 29% ya uzazi wote unaweza kufanyika kwa njia ya upasuaji ifikapo mwaka 2030. 

“Wakati kujifungua kwa njia ya upasuaji kunaweza kuwa ni kwa muhimu na kwa kuokoa maisha, lakini pia kunaweza kuwaweka wanawake na watoto katika hatari isiyo ya lazima ya shida za kiafya za muda mfupi na muda mrefu ikiwa kutafanywa wakati hakuna haja ya kitabibu ya kufanya hivyo.” Imeongeza ripoti. 

Dkt. Ian Askew mkurugenzi wa WHO idara ya afya ya uzazi utafiti na program ya pamoja ya Umoja wa Mataifa HRP amesema “Kujifungua kwa upasuaji ni muhimu sana kwa kuokoa maisha katika hali ambayo kujifungua kwa kawaida kunaweza kusababisha hatari, kwa hivyo mifumo yote ya afya lazima ihakikishe upatikanaji wa huduma hiyo kwa wanawake wote kwa wakati inapohitajika. Lakini kujifungua kote kwa upasuaji kunakofanyika sasa kunahitajika kwa sababu za kiafya. Taratibu zisizohitajika za upasuaji zinaweza kuwa na madhara kwa mama na mtoto wake. ” 

Dkt. Askew ameongeza kuwa kujifungua kwa upasuaji kunaweza kuwa muhimu tu kiatika hali kama vile uchungu wa muda mrefu au mama kushindwa kusukuma mtoto, hatari ya kupoteza mama na mtoto, au kwa sababu mtoto amelala katika hali isiyo ya kawaida tumboni.  

 Hata hivyo amesema kama ilivyo kwa upasuaji wa aina yoyote unaweza kuwa na hatari. “Hatari hizo ni pamoja na uwezekano wa kutokwa na damu nyingi na nzito, kupata maambukizi, kuchukua muda mrefu kupona baada ya kujifungua, ucheleweshaji wa kuanza unyonyeshaji na ukaribu wa ngozi kwa ngozi na mtoto, na uwezekano wa kuongezeka kwa changamoto katika ujauzito wa baadaye.” 

Kadiatu Sama, ambaye hakupata huduma yoyote ile wakati wa ujauzito na ambaye mwanae alizaliwa mfu, akiwa anafarijiwa na muuguzi wa kike kwenye wodi ya wazazi ya hospitali ya serikali nchini Sierra Leone.
© UNICEF/Pirozzi
Kadiatu Sama, ambaye hakupata huduma yoyote ile wakati wa ujauzito na ambaye mwanae alizaliwa mfu, akiwa anafarijiwa na muuguzi wa kike kwenye wodi ya wazazi ya hospitali ya serikali nchini Sierra Leone.

Pengo katika huduma za kujifungua kwa upasuaji 

Kwa mujibu wa ripoti kuna tofauti kubwa katika fursa za wanawake kufikia huduma za upasuaji, kulingana na mahali wanapoishi duniani.  

Katika nchi zilizoendelea kidogo, karibu asilimia 8% ya wanawake walijifungua kwa njia ya upasuaji na asilimia 5% tu ulifanyika katika nchza Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikionyesha pengo kubwa la upatikanaji wa upasuaji huu wa kuokoa maisha. 

Kinyume chake, katika nchi za Amerika ya Kusini na Caribbea, viwango viko juu ambapo wanawake 4 kati ya 10 sawa na asilimia (43%) ya vizazi vyote.  

Katika nchi tano (Jamhuri ya Dominika, Brazil, Cyprus, Misri na Uturuki), kujifungua kwa njia ya upasuaji sasa kunazidi kiwango cha kujifungua kwa njia ya kawaida. 

Ripoti inasema duniani kote uzazi wa njia ya upasuaji umeongezeka kutoka karibu asilimia 7% mwaka 1990 hadi asilimia 21% leo, na idadi inakadiriwa kuendelea kuongezeka kwa muongo huu wa sasa.  

Ikiwa hali hii itaendelea, ifikapo mwaka 2030 viwango vya juu zaidi vinaweza kuwa katika Asia ya Mashariki ikitarajiwa asilimia (63%), Amerika ya Kusini na Caribbea asilimia (54%), Asia ya Magharibi asilimia (50%), Afrika Kaskazini asilimia (48%) Kusini mwa Ulaya asilimia (47%) Australia na New Zealand asilimia (45%), utafiti huo unaonyesha. 

Mwanamke ambaye mtoto wake alizaliwa mfu baada ya uchungu wa zaidi ya saa 10, akiwa amelala kwenye wodi ya wazazi nchini Sierra Leone.
© UNICEF/Olivier Asselin
Mwanamke ambaye mtoto wake alizaliwa mfu baada ya uchungu wa zaidi ya saa 10, akiwa amelala kwenye wodi ya wazazi nchini Sierra Leone.

Huduma zinahitajika kushughulikia hali hii 

Ripoti inasema sababu za ongezeko kubwa la uzazi kwa njia ya upasuaji  hutofautiana sana kati ya ya nchi na nchi na ndani ya nchi.  

“Na vichocheo ni pamoja na sera za sekta ya afya na ufadhili, kanuni za kitamaduni, maoni na mazoea, viwango vya kuzaliwa njiti, na ubora wa huduma za afya.” 

Badala ya kupendekeza viwango maalum vya malengo, WHO inasisitiza umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya kipekee ya kila mwanamke katika ujauzito na wakati wa kujifungua. 

"Ni muhimu kwa wanawake wote kuweza kuzungumza na watoa huduma za afya na kuwa sehemu ya uamuzi juu ya uzazi wao, hasa wakipata habari za kutosha ikiwa ni pamoja na kuelezwa hatari na faida. Msaada wa kihisia ni jambo muhimu sana katika huduma bora wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua, ”amesema Dkt. Ana Pilar Betran, afisa matibabu wa WHO na HRP. 

Muuguzi akiwa amevalia glovu na barakoa wakati anahudumia mtoto mchanga kujikinga na virusi vya corona katika kituo cha afua cha Port Bouet nje ya mji wa Abijan Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Frank Dejongh
Muuguzi akiwa amevalia glovu na barakoa wakati anahudumia mtoto mchanga kujikinga na virusi vya corona katika kituo cha afua cha Port Bouet nje ya mji wa Abijan Côte d'Ivoire.

Mapendekezo ya WHO 

WHO inapendekeza hatua zingine zisizo za kitabibu ambazo zinaweza kupunguza uzazi wa njia ya upasuaji usio wa lazima, kwa muktadha wa huduma bora ya hali ya juu na ya heshima: 

• Njia za kielimu ambazo zinazowashirikisha wanawake katika kupanga mipango ya kujifungua kwao kama vile warsha za maandalizi ya kujifungua, programu za kupumzika na msaada wa kisaikolojia pale unapotakiwa, kwa wale walio na hofu ya maumivu au wasiwasi na utekelezaji wa mipango hiyo unapaswa kujumuisha ufuatiliaji na tathmini inayoendelea. 

• Matumizi ya miongozo ya kliniki inayotegemea ushahidi, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mazoezi ya sehemu ya upasuaji katika vituo vya afya, na kutoa maoni kwa wakati kwa wataalam wa afya juu ya matokeo ya utafiti. 

• Mahitaji ya maoni ya pili ya kitabibu kwa uamuzi wa kujifungua kwa njia ya upasuaji katika mazingira ambayo hili linawezekana. 

• Kwa madhumuni pekee ya kupunguza kiwango cha kujifungua kwa njia ya upasuaji, hatua zingine zimejaribiwa na nchi zingine lakini zinahitaji utafiti mkubwa zaidi: 

• Mfano wa huduma za ukunga na madaktari wa uzazi, ambapo huduma hutolewa hasa na wakunga, kwa mmsaada wa saa 24 kutoka kwa daktari mtaalamu wa uzazi 

• Mikakati ya kifedha inayosawazisha gharama inayotozwa kwa uzazi wa njia ya kawaida na ule wa njia ya upasuaji. 

 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter