Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli za chuki zinaongezeka DRC, hatua zichukuliwe:Keita 

Mjini Bunia jmboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Jeanette Buse, mjane akiwa na wanae 4 kwenye kituo cha wakimbizi wa ndani. Wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano ya kikabila jimboni Ituri.
© UNICEF/Guy Hubbard
Mjini Bunia jmboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Jeanette Buse, mjane akiwa na wanae 4 kwenye kituo cha wakimbizi wa ndani. Wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano ya kikabila jimboni Ituri.

Kauli za chuki zinaongezeka DRC, hatua zichukuliwe:Keita 

Amani na Usalama

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Bintou Keita, amelaani vikali kuenea kwa ujumbe unaochochea chuki, vurugu na uhasama baina ya jamii kwenye majimbo kadhaa ya nchi hiyo. 

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa hii leo Bi. Keita ambaye pia ni mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO,amesema "ninatoa wito kwa viongozi wa pande zote za kisiasa na jamii kuacha kutumia lugha za kibaguzi na zenye uchochezi kwa msingi wa ushirika wa kikabila ambao unaweza kusababisha mgawanyiko zaidi katika jamii na mwishowe kuleta vurugu." 

Wito huo unakuja wakati ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakabiliwa na uhamasishaji wa kipekee wa vikosi vya ulinzi na usalama ili kurejesha amani na usalama Mashariki mwa nchi, ambayo inahitaji juhudi kubwa za mshikamano wa kitaifa. 

Kauli hizo za chuki zimezidishwa haswa katika muktadha wa mizozo Mashariki mwa DRC, kuongezeka kwa mapigano kati ya vikundi vyenye silaha vilivyofungamana na jamii katika eneo la Hauts-Plateaux la Kivu Kusini, Kivu ya Kaskazini na Ituri, lakini pia zimebainika kusambaa huko Katanga, Maï-Ndombe na hata Kinshasa. 

Tweet URL

Bintou Keita amekumbusha kwamba “uchochezi wa chuki, vurugu na uhasama ni kinyume cha sheria za kimataifa na sheria za DRC. Ni matumizi mabaya ya haki ya uhuru wa kujieleza, ambayo ni msingi wa jamii ya kidemokrasia,”  
Ameendelea kusema kuwa vitendo kama hivyo vinaashiria tishio kwa amani, usalama na mshikamano wa kitaifa, na huharibu sana mfumo wa kuishi pamoja. 

MONUSCO imesisitiza azma yake ya kuunga mkono juhudi za mamlaka ya Congo kuzuia na kupambana vyema dhidi ya ujumbe unaochochea chuki, vurugu na uhasama kati ya jamii.  

Pia mpango huo umelihimiza bunge la DRC kupitisha muswada  wa kupinga ukabila, ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni katika vikao vya sasa katika Bunge la Kitaifa na iko tayari kusaidia mahakama za DRC  kuanzisha kesi, kwa mujibu wa sheria iliyopo.