Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Watoto wakimbizi wakichota maji katika eneo la Maradi Niger.

Asilimia 99 ya Watoto Niger hawajui kusoma na kuandika:Benki ya Dunia

© UNICEF/Juan Haro
Watoto wakimbizi wakichota maji katika eneo la Maradi Niger.

Asilimia 99 ya Watoto Niger hawajui kusoma na kuandika:Benki ya Dunia

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya mtoto wa Afrika, ndoto za kutimiza ajenda ya bara hilo ya mwaka 2040 ya kuwa na bara la Afrika linalomfaa mtoto wa Afrika ikiwemo katika suala la kupata elimu, kwa Niger huenda lisitimie kwani asilimia 99 ya watoto wenye umri wa miaka 10 ni wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika.

 

Mwanafunzi Salif Namaka amesema ana imani na usemi usemao elimu ndio msingi wa maendeleo, na elimu ndio inayompa mtoto maarifa ya kukabili mustakabali autakao lakini anahoji je, itawezekana kwa taila lake la Niger.


Kwa mujibu wa Benki ya Dunia asilimia 99 ya Watoto wa umri wa miaka 10 ni maamuma nchini Niger, hawajui A wala B, na zaidi ya nusu ya watoto wa umri wa miaka 7 na 12 hawako shuleni kwa sababu ya ukosefua wa rasilimali na mahali ya kusomea.

Mohamed Garba ni mwalimu katika moja ya shule nchini humo amesema, “Lengo letu ni kuwaelimisha Watoto lakini kwa bahati mbaya shule ni kama imetelekezwa , tuna idadi kubwa ya wanafunzi madarasani, wanafika 100 kwa darasa na unaona mwalimu hawezi kukidhi mahitaji ya watoto wote. Bila kuwa na miundombinu ya kutosha hatuwezi kutimiza malengo yetu ya elimu.” 


Kauli hiyo inaungwa mkono na mwalimu Mariam Hamadou "hawana rasilimali zinazohitajika ikiwemo vitabu vya kufundishia na vifaa vingine muhimu."

 Wanafunzi hupaswa kumaliza miaka 12 shuleni lakini asilimia kubwa ya wanafunzi Niger hukaa shuleni wastani wa miaka 5.3 pekee, sababu kubwa ikiwa ni vita, mila na desturi na kubwa zaidi kutokuwa na rasilimali. 
Kwa kutambua umuhimu wa kutimiza lengo la elimu nchini humo, Benki ya dunia imeanzisha mradi ujulikanao kama “Kuboresha usomaji kwa ajili ya matokeo chanja katika elimu “ au LIRE. 


Mradi huo unasaidia juhudi za serikali kuimarisha mfumo wa elimu Niger, lakini pia utaboresha mazingira ya kazi kwa walimu na hasa kwenye maeneo yenye mizozo, ili wavulana na wasichana kama mwanafunzi Samira Adamou ambaye ni binti pekee kwenye familia yake waweze kupata elimu bora na kufikia uwezo wao.


Akiwa na matumaini makubwa  Samira anasema ”Ni wajibu wangu kujikita na masomo kwa sababu nina kaka mmoja tu mkubwa na tayari anafanyakazi, mdogo wangu anatakiwa kufuata nyayo zangu na ninatumai kuwafanya wazazi wangu wahisi fahari kubwa kwa kusoma kwa bidi kwani wananitumainia”