Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa ndani bado wanalilia maslahi yao: ILO

Wafanyakazi wa majumbani wakishiriki maandamano kwa ajili ya haki za ajira
ILO
Wafanyakazi wa majumbani wakishiriki maandamano kwa ajili ya haki za ajira

Wafanyakazi wa ndani bado wanalilia maslahi yao: ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Licha ya muongo mmoja wa uwepo wa mkataba wa kimataifa wa haki za wafanyakazi wa ndani,  bado kada hiyo inaendelea kupigania usawa na mazingira bora ya kazi huku janga la ugonjwa wa Corona au COVID19 likionesha dhahiri udhaifu uliopo katika kada hiyo.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya  shirika la Umoja wa Mataifa la Ajira duniani, ILO iliyozinduliwa leo huko Geneva Uswisi. Leah Mushi amefuatilia na kuandaa taarifa ifuatayo. 

Kada ya Wafanyakazi wa ndani imeajiri zaidi ya watu milioni 75.6 sawa na asilimia 4.5 ya wafanyakazi wote duniani na takwimu zinaonesha wanawake ni zaidi ya asilimia 70 wa wafanyakazi hao. 

 Janga la COVID-19 lililoikumba dunia tangu  2019 limeonesha ni namna gani wafanyakazi wake wanavyokosa haki zao, maana wengi walijikuta wakikosa ajira licha ya uwepo wa mkataba wa Kimataifa uliopitishwa miaka 10 iliyopita. 

Myanyakazi wa ndani akifua nguo kwa mikono mjini Delhi India (Picha toka maktaba)
ILO/B. Patel
Myanyakazi wa ndani akifua nguo kwa mikono mjini Delhi India (Picha toka maktaba)

 Ripoti hiyo ya muongo mmoja tangu  kupitishwa kwa Mkataba huo wa haki za wafanyakazi wa ndani imefichua kuwa asilimia 5 hadi  20 ya wafanyakazi wa ndani barani Ulaya, Canada na Kusini mwa Afrika walijikuta wakipoteza kazi wakati wa janga la Corona, na hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Amerika ambapo asilimia ya waliopoteza kazi ilikuwa kati ya 20 mpaka 50. 

 Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy [GII] Ryder amesema janga la Corona limerudisha nyuma harakati za wafanyakazi hao. 

“Janga hili limeonesha uhitaji wa haraka wa kurasimisha kada wa wafanyakazi wa ndani ili kuwahakikishia ufikiaji wao wa kazi bora na kutelekeza sheria za kazi na usalama wa wafanyakazi wa majumbani “ 

Pamoja na changamoto nyingi lakini ripoti hii pia imeonesha uwepo wa matokeo chanya kwa baadhi ya nchi ambazo zimeanzisha sheria za wafanyakazi wa ndani. 

“Wafanyakazi wa majumbani wamejipanga vizuri hivi sasa na wanaweza kujiwakilisha kutetea maslahi na maoni yao. Mashirika yanayotetea haki zao na ya wafanyakazi wa majumbani yamejitwika jukumu muhimu katika maendeleo yaliyopatikana hadi sasa” amewapongeza Mkurugenzi huyo Mkuu  wa ILO. 

Takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi wa ndani wanapatikana katika bara la Asia na Pasifiki ambako kumeajiri zaidi ya nusu ya wafanyakazi wote wa ndani (Milioni 38.3) ikifuatiwa na Amerika ambako kuna wafanyakazi milioni 17.6.