Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mtoto mwenye umri wa miezi 7 huko Tigray Magharibi nchini Ethipia akila biskuti yenye virutubisho kwa lengo la kuboresha afya yake.

Watoto 33,000 hatarini kufa nchini Ethiopia- UNICEF

© UNICEF/Esiey Leul Kinfu
Mtoto mwenye umri wa miezi 7 huko Tigray Magharibi nchini Ethipia akila biskuti yenye virutubisho kwa lengo la kuboresha afya yake.

Watoto 33,000 hatarini kufa nchini Ethiopia- UNICEF

Afya

Takriban watoto 33,000 katika eneo ambalo halifikiki la Tigray nchini Ethiopia wana utapiamlo mkali na wanakabiliwa na vifo iwapo msaada wa haraka hautapatikana, imesema taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta Fore iliyotolewa leo jijini New York, Marekani. 
 
 

Fore amesema, tatizo ni kubwa na UNICEF inaomba msaada wa dharura kutoka kwa wafadhili, wakati wanapanua mipango yao yakuwafikia watoto wote wenye uhitaji kwa haraka kabla hawajachelewa.
“Watoto hawa ni miongoni mwa zaidi ya watoto milioni 2.2 kaskazini mwa Ethiopia ambao wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, pamoja na takriban 140,000 huko Tigray ambao wanakabiliwa na njaa kiwango cha 5. UNICEF inakisia watoto 56,000 chini ya miaka 5 huko Tigray watahitaji matibabu kwa mwaka huu kutokana na utapiamlo mkali, hii ni mara sita zaidi ya wastani wa mwaka kwa mkoa huo," amesema Bi. Fore

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF amegusia pia tatizo la kukosa lishe kwa wajawazito na wanawake wanaonyonyesha ambalo limefikia zaidi ya asilimia 40, likihatarisha maisha ya watoto wachanga na wanawake waliojifungua.

Uharibifu wa miundombinu ya kusaidia kutoa huduma, imesababisha hali kuwa mbayá zaidi kwani misaada inayotegemewa na watoto imeshindwa kuwafikia. Watoa huduma ya afya wamekuwa wakipokea vitisho na kudhalilishwa, hali inayosababisha wengi kushindwa kurudi kutoa huduma. Uharibifu wa miundombinu ya maji imesababisha uhaba mkubwa wa maji safi na salama ya kunywa.

“Haya mambo yamesababisha hali kuwa mbayá zaidi na huenda ikasababisha mlipuko wa magonjwa, watoto wenye utapiamlo wapo kwneye hatari mbayá zaidi ya kufa. Maeneo yanayohifadhi watoto na familia yana hatari kubwa ya kupata makusambaza magonjwa sababu ya msongamano wa watu na hali mbayá ya usafi,” ameongeza Bi. Fore

UNICEF imeahidi kufanya kila juhudi kuhakikisha kuzuia vifo visitokee na lengo lao ni kufikia watoto wote mkoani huko ambao wapo kwenye hali mbayá kiafya, waliokosa lishe, maji safi, huduma za usafi, shule na usalama.

Halikadhalika shirika hilo linaamini kufanya kazi pamoja na washirika wake ili kuhakikisha kila mtoto mwenye utapiamlo anapata matibabu ya kuokoa maisha yake.