COVID-19 yasababisha kupungua kwa kiwango cha uchangiaji damu Afrika- WHO 

14 Juni 2021

Leo ni siku ya kuchangia damu duniani ambapo kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani,  WHO mwaka huu siku hiyo inajikita na vijana na mchango wao katika kuokoa maisha kwa kujitolea damu. Kauli mbiu ikiwa“Toa damu na kuhakikisha dunia inaendelea kuishi”.  

Nako barani Afrika katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara WHO inasema  kiwango cha uchangiaji wa damu kimeshuka kwa asilim ia 17 tangu kuzuka kwa janga la Corona au COVID-19 na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa katika huduma muhimu za afya maisha na uwezo wa watu kuishi. 

Takwimu za shirika hilo zinaonesha kwamba kila mwaka zaidi ya wanawake 196,000 wanafariki dunia kutokana na changamoto za ujauzito na nyingi zikiwa ukosefu wa damu na hivyo shirika hilo limechagiza uchangiaji damu ili kuwapa uhai kina mama na watoto.  

Tathimini ya WHO Afrika 

Tathimini ya WHO imegundua kuwa mzunguko wa mwendo wa uchangiaji damu katika ukanda wa Afrika umepungua kwa asilimia 25 na mahitaji ya damu yamepungua kwa asilimia 13, na huku kukiwa na kusimamishwa kwa baadhi ya upasuaji wa kawaida katika nchi zingine na watu wachache wanaotafuta huduma katika vituo vya afya.  

Karibu watu milioni 7 wanahitaji kuongezewa damu kila mwaka katika ukanda wa Afrika. 

WHO inasema kaulimbiu ya siku ya kuchangia damu mwaka huu ni ya kuonyesha mchango muhimu wa wachangiaji wa damu katika kuokoa maisha na kuboresha afya za wengine. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti, amesema “kukatizwa kwa usambazaji thabiti wa damu salama kunaweza kutishia maisha. Tunashukuru sana ishara ya kujitolea ya wachangiaji wa damu na tunahimiza nchi zianzishe na kuimarisha mifumo ya kuongeza michango ya damu ya hiari, ".  

WHO inashirikiana na mashirika kama vile Muungano wa Damu kwa ajili ya Afrika uliozinduliwa Novemba mwaka 2020, Shirika la wanawake wa Kwanza wa Afrika kwa maendeleo na sekta binafsi ili kuboresha upatikanaji na usambazaji wa damu bora. 

Kwa kushirikiana na Facebook, WHO imeanzisha huduma ya uchangiaji damu ya kikanda, ambayo inaunganisha watu na benki za damu zilizo karibu.  

Nyenzo hiyo sasa inafanyakazi katika nchi 12 na zaidi ya watumiaji milioni 3.8 wa Facebook wamejiandikisha kujulishwa juu ya fursa za uchangiaji damu.    

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter