Nchi mbili za Afrika zachaguliwa kuingia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

11 Juni 2021

Nchi za Ghana na Gabon kutoka Afrika zimechaguliwa hii leo kuingia kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa miaka miwili kuanzia januari 1, 2022 pamoja na nchi nyingine tatu. 
 

Nchi hizo nyingine ni ni Albania, Brazil na Umoja wa falme za kiarabu zimefanya jumla ya nchi tano zilizopigiwa kura nyingi na wajumbe wa baraza kuu la umoja wa mataifa wakati wa uchaguzi uliofanyika makao makuu ya umoja wa mataifa New York, Marekani. 

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Volkan Bozkir akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa amesema, “nazipongeza nchi hizo tano ambazo zimechaguliwa kwa kura nyingi kuingia baraza la usalama, nchi hizo zitajiunga na India, Ireland, Kenya, Mexico na Norway pamoja na wanachama wa kudumu wa baraza la usalama ambao ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani.”

Nchi hizo tano zinachukua nafasi za nchi 5 zilizo maliza muda wake ambazo ni Niger, Estonia, vietnam, Tunisia pamoja na Saint Vincent na Grenadines. 

Nje ya mkutano wa Baraza, Waziri wa mambo ya nje ya Albania, Olta Xhacka, amesema anaamini nchi ndogo zilizochaguliwa zitaleta mchango mkubwa wa ushirikiano “ni dhahiri nchi ndogo ni watazamaji wa historia wakati maamuzi makubwa yanafanyika, lakini hii ni fursa yetu, sio tuu kutazama lakini pia kushawishi maamuzi hayo makubwa kwa manufaa ya wote, ambao ni ulimwengu na sio tuu nchi au ukanda. Tunaamini tutashiriki kwenye baraza hili kuleta ladha tofauti ya mtaani au namna nchi ndogo zinavyonufaika sana na ushirikiano wa kimataifa na tunaamini tutakuwa mfano bora wa kuleta watu pamoja kuishi pamoja na kushirikiana.”

Hii ni mara ya kwanza kwa Albania kuingia katika baraza la usalama la umoja wa Mataifa. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter