Uwekezaji katika sayansi duniani waongezeka, lakini nchi zatofautiana

11 Juni 2021

Uwekezaji wa fedha katika sayansi duniani kote yaliongezeka kwa asilimia 19 kati yam waka 2014 na 2018, sambamba na ongezeko la idadi ya wanasayansi ambalo ni kwa asilimia 12.7, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO iliyozinduliwa leo huko Paris nchini Ufaransa.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina Kasi dhidi ya muda kwa maendeleo ya kisasa, inaonesha kuwa kasi ya ongezeko la matumizi ya sayansi inachochewa zaidi hivi sasa kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Nchi zinatofautiana

Hata hivyo ripoti hiyo inaonesha tofauti kubwa sana katika ongezeko hilo la uwekezaji katika sayansi kati ya nchi na nchi ambapo ni Marekani na China zinachangia theluthi mbili au asilimia 63 ya ongezeko hilo.
Huku nchi 2 kati ya 5 zikiwa nyuma zaidi kwa kuwekeza asilimia 1 tu ya pato lao la ndani,  GDP katika utafiti wa kisayansi, ikimaanisha kwamba “uwanja wa sayansi bado ni suala la uthabiti na nguvu na uwezo.”
Ripoti hiyo inachapishwa kila baada ya miaka mitano na inaweka bayana mtazamo wa sayansi na sera za kisayansi.
Tafiti kuhusu akili bandia au AI pamoja na masuala ya maroboti ndio zinashika kasi zaidi ambapo kulikuwepo na machapisho 150,000 mwaka 2019 pekee huku nchi za kipato cha chini na kati zikiongeza mchango wao kwenye tafiti hizo kwa ongezeko la asilimia 25.3 mwaka 2019 ikilinganishwa na asilimia 12.8 mwaka 2015.

Roboti aliyepatiwa jina la Sophia ni miongoni mwa  ubunifu wa hali ya juu kwenye akili bandia.
UN /Manuel Elias
Roboti aliyepatiwa jina la Sophia ni miongoni mwa ubunifu wa hali ya juu kwenye akili bandia.

Vikwazo vya kupata tafiti mpya

Pamoja na ongezeko la tafiti bado matokeo ya tafiti hizo yanakuwa ni vigumu kupatikana duniani kote, “licha ya kasi kubwa ya tafiti iliyochochewa na vita dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19, bado kuna vikwazo vingi vya matokeo ya tafiti hizo kupatikana bila usumbufu duniani kote. Mfano, zaidi ya asilimia 70 ya machapisho hayapatikani kwa watafiti wengi.”
Ni kwa mantiki hiyo ripoti hiyo inaonesha vikwazo hivyo vya matokeo ya utafiti kupatikana kwa urahisi kwa kila mtafiti na hivyo kutaka mbinu za usambazaji wa matokeo hayo zibadilishwe.

Ripoti pia inataka uwepo wa makundi tofauti kwenye tafiti ikisema “theluthi moja tu ya watafiti ni wanawake. Ingawa usawa umepatikana katika masomo ya sayansi, ado kuna safari ndefu katika nyanja zingine. Mfano wanawake ni asilimia 22 tu kwenye ajira za nyanja ya akili bandia au AI. Hatuwezi kuruhusu ukosefu huu wa usawa kwenye jamii uendelee kuota mizizi kwa sayansi ijayo.”

Badala yake UNESCO kupitia ripoti hiyo inataka sayansi iunganishe binadamu wote katika kukabili changamoto za sasa na zijazo.

“Imáni ya umma kwa sayansi lazima irejeshwe” inasema ripoti hiyo na kukumbusha kuwa sayansi ya leo inachangia katika kuumba dunia ya kesho na ndio maana “ni muhimu kupatia kipaumbele lengo la ubinadamu la uendelevu kupitia sera za kisasa za sayansi.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter