COVID-19 yashika kasi Afrika, chanjo ni haba, Uganda hali si  hali

10 Juni 2021

Idadi ya wagonjwa wa Corona au COVID-19 inavyoendelea kuongezeka kwa wiki tatu mfululizo barani Afrika huku chanjo ikisalia kuwa haba, mataifa 47 kati ya 54 barani humo yanaelekea kutofikia lengo la kutokuwa yamepatia chanjo angalau asilimia 10 ya wananchi wake ifikapo mwezi Septemba mwaka huu. 

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Brazaville, Congo, akisema kufikia lengo la chanjo itawezekana iwapo tu bara hilo litapokea chanjo nyingine milioni 225. 

Viwango hivyo vipya vya uchanjaji COVID-19 vilitangazwa hivi karibuni wakati wa Baraza Kuu la Afya Duniani, ambalo ndilo chombo cha juu cha kuweka sera za kiafya ulimwenguni, na sasa ni nchi 7 pekee ndio zina mwelekeo wa kufikia lengo hilo. 

Waziri wa afya akizuru wagonjwa wa COVID-19, Qena, Misri.
Khaled Abdul-Wahab
Waziri wa afya akizuru wagonjwa wa COVID-19, Qena, Misri.

Hali ni mbaya zaidi Uganda, Zambia na Misri 

Idadi ya wagonjwa wa COVID-19 Afrika inapokaribia milioni 5, maambukizi mapya yanaongezeka kila wiki kwa takribani asilimia 20 na kuwa wagonjwa zaidi ya Elfu 88 kila wiki ilipofika tarehe 6 mwezi huu wa Juni. 

Mwelekeo unaongezeka katika nchi 10 huku mataifa manne yakiwa na ongezeko la asilimia 30 katika siku 7 zilizopita ikilinganishwa na wiki iliyotangulia. 

Asilimia 72 ya wagonjwa wote wapya wameripotiwa Misri, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda na Zambia. 

Mkurugenzi huyo wa WHO kanda ya Afrika, amesema “idadi ya wagonjwa milioni 5 inapokaribia Afrika, na awamu ya tatu ya COVID-19 nayo ikinyemelea, watu wengi walio hatarini wanasalia kwenye uwezekano wa kupata COVID-19. Chanjo ndio iliyothibitika kuzuia maambukizi na vifo. Kwa hiyo nchi lazima zipatiane chanjo hizo. Kupatiana chanjo ndio suala la uhai au kifo Afrika.” 

Muhudumu wa afya akitoa chanjodhidi ya COVID-19 nchini Sudan Kusini
© UNICEF/Bullen Cho Mayak
Muhudumu wa afya akitoa chanjodhidi ya COVID-19 nchini Sudan Kusini

 

Mgao wa chanjo kwa Afrika 

Ikiwa imepatiwa dozi milioni 32, Afrika inakuwa imepata chini ya asilimia 1 ya zaid iya chanjo bilioni 2.1 zilizosambazwa duniani. Ni asilimia 2 tu ya wakazi bilioni 1.3 wa Afrika ndio wamepata chanjo ya kwanza na ni waafrika milioni 9.4 ndio wamepata chanjo kamili. 

Hata hivyo Dkt. Moeti amepongeza hatua ya Rais wa Marekani Joe Bide ya kununua chanzo milioni 500 aina ya Pfizer na kupatia nchi 92 za kipato cha chini na kati barani Afrika, hatua ambayo imetangazwa wakati Ufaransa nayo imetangaza itachukua hatua kama hiyo kupitia COVAX. 

Mataifa ya Afrika yaliyojipanga vizuri 

Nchi kadhaa za Afrika zimerekebisha mifumo yao ya utoaji chanjo zikiwemo Côte d'Ivoire na Niger huku WHO ikipendekeza pia kusongesha huduma hizo hadi vijijini na kuhakikisha chanjo zinatolewa kabla ya muda wake kumalizika.  

WHO inapongeza pia nchi za Afrika zilizochukua hatua kubadili mtazamo hasi dhidi ya chanjo za COVID-19 na hivyo kuwepo kwa ongezeko la mahitaji ya chanjo miongoni mwa wananchi. 

Tafiti ya WHO, UNICEF na kamati ya kimataifa ya hilal nyekundu, IFRC inaonesha kuwa imani ya chanjo ya COVID-19 miongoni mwa wananchi katka ukanda wa Afrika ya Kati na Magharibi ndio uko chini zaidi ambapo ni asilimia 60. 

Kwa sasa video mbalimbali zinasambazwa kukabili matangazo potofu dhidi ya chanjo, matangazo yanapitishwa kwa njia tofauti ikiwemo mitandao ya kijamii. 
 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter