Nchi za G7 lazima zihakikishe fursa ya chanjo kwa nchi zinazoendelea:wataalam wa haki UN 

10 Juni 2021

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wametoa wito kwa viongozi wa nchi za uchumi mkubwa zaidi ulimwenguni G7 kuhakikisha watu katika ukanda wa Kusini wa dunia wanapata usawa wa chanjo ya corona au COVID-19 na wasiruhusu dhamira ya faida kudhoofisha afya na usawa wa duniani. 

Katika taarifa yao iliyotolewa mjini Geneva Uswis wataalam hao wamesema "Kila mtu ana haki ya kupata chanjo ya COVID-19 ambayo ni salama, inayofaa, kwa wakati unaofaa na kwa misingi inayotegemea matumizi ya maendeleo bora ya kisayansi,"  

Nawataalam wameyasema hayo kabla ya mkutano wa viongozi wa G7 utakaofanyika nchini Uingereza kuanzia tarehe 11-13 Juni. 

Wameongeza kuwa "Sasa ni wakati wa mshikamano na ushirikiano wa kimataifa kutoa msaada mzuri kwa serikali zote katika juhudi zao za chanjo na kuokoa maisha na sio wakati wa majadiliano ya muda mrefu au ya kushawishi kuweka vizuizi ili kulinda faida za kampuni." 

Wataalam wamesisitiza kuwa utengenezaji wa haraka wa chanjo salama na madhubuti dhidi ya COVID-19 haukufuatiwa na hatua za haraka za kuhakikisha usawa wa upatikanaji katika nchi zote na kanda zote. 

Programu ya utoaji chanjo kubwa kabisa duniani ilipoanza India Januari 2021.
© UNICEF/Ruhani Kaur
Programu ya utoaji chanjo kubwa kabisa duniani ilipoanza India Januari 2021.

“Mabilioni ya watu ukanda wa Kusini mwa dunia wanaachwa nyuma. Wanaona chanjo kama ishara au fursa kwa ulimwengu ulioendelea. Hali hii itaongeza mzozo bila sababu, itaongeza sana idadi ya waliokufa na kuongeza msukosuko wa kiuchumi, ikiwezekana kupanda mbegu za machafuko ya kijamii." wameonya wataalam hao. 

Wamehimiza kwamba viongozi wa G7 lazima wahakikishe kipaumbele chao cha juu ni kulinda haki za maisha na afya za watu katika hali mbaya sana ya kijamii na kiuchumi wakati ambapo mamilioni wanakabiliwa na umaskini na njaa. 

Wataalam hao wamekumbusha taarifa yao yam waka jana inayoonya kuhusu  gharama za janga la COVID-19 kwa binadamu  

"Inashangaza kwamba, kulingana na ripoti za shiorika la afya duniani WHO, chini ya asilimia moja ya chanjo zote zilizotolewa hadi sasa ndio zimekwenda kwa nchi zenye kipato cha chini”. 

Wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa haki miliki hazina kikwazo kwa uzalishaji wa gharama nafuu na kupanua usambazaji huo wa chanjo.  

Pia wamezitaka kampuni za dawa kujiunga na jopo la masuala ya teknolojia ya COVID-19 linalosimamiwa na WHO (C-TAP) kwa ajili ya kushiriki ujuzi, takwimu, na kuwezesha uhamishaji wa teknolojia. 

Wataalm hao wakumbusha kuwa wakati Mkataba wa TRIPs juu ya haki miliki unatoa mabadiliko kadhaa, pamoja na uwezekano wa kutoa leseni ya lazima katika hali ya dharura ya kitaifa, hizo bado hazitoshi kukabili janga la sasa. 

"Kuongeza uzalishaji wa chanjo salama lazima kuchukue nafasi ya kwanza kuliko kufaidika na janga hili la kimataifa," wamesisitiza na kuongeza kuwa "Mataifa lazima yahakikishe kuwa ulinzi wa kisheria kwa umiliki na hati miliki haudhoofishi haki ya kila mtu kupata chanjo salama, kwa wakati unaofaa na inayofaa." 

Chanjo ya COVID-19 ikisafirishwa na mtumbwi kuelekea kisiwa cha Bwama, moja ya maeneo magumu kufikika katika wilaya ya Kabale Magharibi mwa Uganda
© UNICEF/Catherine Ntabadde
Chanjo ya COVID-19 ikisafirishwa na mtumbwi kuelekea kisiwa cha Bwama, moja ya maeneo magumu kufikika katika wilaya ya Kabale Magharibi mwa Uganda

Wataalam pia wameyakumbusha mataifa kuchukua hatua kulingana na kanuni za uongozi za Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na haki za binadamu na kuhakikisha kwamba taasisi za kimataifa kama vile shirika la biashara duniani (WTO) "hazizuii uwezo wa nchi wanachama kutimiza jukumu lao la kulinda au kuzuia biashara kutokana na kuheshimu haki za binadamu ”. 

Wataalm wameangazia pia hitaji la kuimarisha uwezo wa nchi zinazoendelea kuzalisha chanjo zao wenyewe kwa kuhakikisha msaada wa kifedha na kiufundi kwa utengenezaji wa ndani ambapo tayari nchi zingine zinaanza na kulinda ufikiaji wa viambato vinavyohitajika kwa uzalishaji. 

Wataalam hao wameidhinisha taarifa ya hivi karibuni na kamati ya haki za kiuchumi, Kijamii na kiutamaduni ya Umoja wa Mataifa ambayo imesema kutopatikana kwa usawa kwa chanjo kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea sio tu ni ubaguzi, lakini pia kunadhoofisha maendeleo katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu. 

"Tumevutiwa sana na jukumu ambalo asasi za kiraia na wanaharakati wengine  wanalifanya katika kukuza msaada kutoka kwa mataifa na wadau mbali mbali la wito wa chanjo ambayo inapaswa kupatikana kwa wote, kila mahali na bila malipo," wamesema wataalam hao. 

 

  

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter