Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 29 kushiriki michuano ya Olimpiki Tokyo Japan mwaka huu:UNHCR 

Mkimbizi kutoka Sudan Kusini akiwa NairobI, Kenya kwa ajili ya mazoezi ya mbio na kujiandaa kushirikia michezo ya Olimpiki2020.
© UNHCR/Benjamin Loyseau
Mkimbizi kutoka Sudan Kusini akiwa NairobI, Kenya kwa ajili ya mazoezi ya mbio na kujiandaa kushirikia michezo ya Olimpiki2020.

Wakimbizi 29 kushiriki michuano ya Olimpiki Tokyo Japan mwaka huu:UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC imetangaza ushiriki wa timu ya wakimbizi 29 katika mashindando ya Olimpiki yatakayofanyika Tokyo Japan mwezi ujao.

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi akiipongeza timu hiyo ya wakimbizi na kusema anachotarajia kutoka kwao mwezi Julai ni ushindi.  

Pia amesema UNHCR imekaribisha na kusherehekea tangazo hilo ambalo ni ishara ya mshikamano na wakimbizi. 

Bwana Grandi ameongeza kuwa baada ya miaka ya mafunzo na mazoezi wakimbizi hao 29 watapeperusha bendera ya wakimbizi katika michezo 12 na kutuma ujumbe mzito kwa dunia wa mshikamano na matumaini, huku wakitanabaisha madhila yanayowakabili watu milioni 80 waliotawanywa duniani kote kwa sababu moja au nyingine. 

Michezo hii ya Olimpiki inayofanyika mwaka huu ilikuwa ifanyike mwaka jana 2020 lakini iliahirishwa kwa sababu ya janga la corona au coronavirus">COVID-19.  

Na baada ya tangazo hilo la timu ya wakimbizi jana Jumanne Bwana Grandi amewapa ujumbe mzito wachezaji hao,“Tunajivunia nsana mafanikio yenu na kumbukeni marafiki wapendwa, wanariadha wapendwa. Kwamba kwa kiasi fulani mna majukumu ya ziada. Sio tu kufanya vizuri katika mashindano ambayo ni kazi ya msingi inayowapeleka Tokyo lakini kuwakilisha na kuwapa motisha mamilioni ya wakimbizi na watu waliotawanywa duniani kote ambao watakuwa wakiwaangalia na kujivunia kile mtakachofanikisha.” 

Kwa mujibu wa UNHCR hii itakuwa ni mara ya pili kwa timu ya wakimbizi kushiriki katika michezo ya Olimpiki, baada ya mara ya kwanza kwenye michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio De Janeiro nchini Brazil mwaka 2016. 

Kama sehemu ya ushirikiano wake wa zaidi ya miaka 25 na IOC, UNHCR inafanya kazi na kamati hiyo na ORF kutumia uwezo wa michezo kusaidia kujenga dunia ambayo kila mtu anayelazimika kukimbia anaweza kujenga maisha bora ya baadaye.  

Pamoja na IOC, ORF, kamati ya kimataifa ya watu wenye ulemavu (IPC) na washirika wengine, UNHCR inaongoza wito wa kimataifa wa kuwa na ulimwengu ambao watu wote waliotawanywa, pamoja na wale wenye ulemavu, wanaweza kupata fursa na kushiriki katika michezo.