Ruzuku za IFAD zatunusuru na maambukizi ya COVID-19

Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo -IFAD umewawezesha wanakijiji nchini Ethiopia kujipatia kipato kupitia mradi wa uchimbaji wa mifereji ya kuzuia maji yasiharibu mazingira na kudhibiti mmonyomoko wa udongo uliokuwa ukiathiri kilimo na hivyo kuwakosesha mapato. Mradi huo pia umewawezesha kujinusuru na maambukizi ya corona.
Ukanda wa nyanda za juu nchini Ethiopia, kundi la vijana hamsini wakiendelea na shughuli za ujenzi wa mabwawa kwa kutumia mawe na kuchimba mifereji ya kupitisha maji ili kuweza kuendeleza kilimo cha umwagiliaji wakati wa mvua chache na kuthibiti mmomonyoko wa udongo wakati wa mvua kubwa.
Eneo hili hapo awali lilikuwa ni shamba kubwa la kilimo, lakini mvua kubwa zimeondosha udongo kwa kiasi kikubwa na kuwaacha wakulima wakiwa na mazao ambayo ni haba kutosha chakula na kuuza ili wapate fedha za kujikumu.
Kupitia ruzuku kwa vijiji masikini vilivyoathirika na janga la corona zinazotolewa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo -IFAD vijana hawa wameona nuru ing’aayo kwenye maisha yao
“Faida ya kazi yetu kwa jamii yetu ni kuwa tunahifadhi mazingira tusipate mmomonyoko wa udongo na vijana katika jamii yetu wanapata ajira na kujipatia kipato cha kuweza kujikimu” amesema Terrefe Tsega mmoja wa wajenzi.
Ruzuku hiyo pia imekuwa kwa namna moja ahueni kujiepusha na janga la corona au COVID-19 kwakuwa wananchi wa Kijiji hiki kwasasa hawasafiri kwenda kusaka ajira nje ya kijiji chao ili kujipatia fedha za kujikimu hali ambayo pia ingewaweka hatarini kupata maambukizi ya COVID-19.
“Hela tunazopata hapa zimebadilisha maisha yetu. Ukiniuliza mimi, kwanza sasa tunaweza kununua kondoo na kupata chakula, pili, tunaweza kula mayai sababu tunafunga kuku, na tatu, tuna uwezo wa kununua nguo kwa Watoto wetu na tunaishi bila wasiwasi.”
Wakati Dunia ikiendelea kupambana na athari za janga la corona na mabadiliko ya tabia nchi, kazi inayofanywa na vijana hawa inasadia kuhifadhi mazingira, kurejesha uoto wa asili na kwakufanya hivyo wanajihakikishia kipato kutoka kwenye mazao ya kilimo, na chakula kwa familia zao.