Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nashukuru UNICEF imenitoa kwenye mgodi hatarishi- Mtoto Clement

Mtoto mkazi wa Kipushi jimboni Katanga-Juu nchini DRC akiwa amebeba chekecheo la madini ya shaba.
UNICEF/Giacomo Pirozzi
Mtoto mkazi wa Kipushi jimboni Katanga-Juu nchini DRC akiwa amebeba chekecheo la madini ya shaba.

Nashukuru UNICEF imenitoa kwenye mgodi hatarishi- Mtoto Clement

Haki za binadamu

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto limechukua hatua kuwaondoa watoto wachimbaji madini kwenye eneo la Kipushi, jimboni Katanga-Juu na kuwapeleka shuleni, hatua ambayo imeleta furaha kwa watoto hao. 
 

Maisha ya kila siku ya watoto hao yalikuwa ni kupasua miamba kwa kwa kutumia vifaa duni na mikono kwa lengo la kusaka madini.

Wanawake nao hawakuwa nyuma katika kazi ya kuponda mawe penginepo bahati itawaangukia.

Ni taswira kutoka video ya UNICEF katika eneo la Kipushi jimboni Katanga Juu nchini DRC!  Umaskini umefikisha watoto na wanawake eneo hili.

Clement Kapanda mtoto mwenye umri wa miaka 12 ni manusura wa hali hii na mwokozi wake ni UNICEF na akiwa darasani akizungumza na mfanyakazi wa UNICEF anasema alikuwa anatumikishwa kwenye uchimbaji madini na wakati mwingine hakuwa na chakula.

Kwenye video hiyo, Clement anaonekana akitumbukia kwenye mashimo marefu yeye na mwenzake kwenye tochi na yeye akiwa na chuma ili kupasua miamba! 

Wengine walitumia vifaa duni kupasua mawe yaliyokwishachimbwa na hata kuharibu mikono na miguu yao.
Video hiyo inaonesha mchakato mzima wa uchimbaji madini kuwa hatarini na hatma yake ni malori kufika eneo hili na kubeba vifusi kupeleka vitakiwapo.

UNICEF sasa imemuondoa Clement machimboni na kumweka darasani na anaonekana akisikiliza kwa makini, na anaandika katika daftari alilopatiwa na shirika hilo na hata alipopatiwa fursa kwenda ubaoni, alikwenda na kujibu maswali.
Clement anasema sasa ana furaha na ili kuepusha watoto kama Clement kutotumikishwa tena, wahudumu wa kijamii wanapita sasa na kwenye machimbo  kuwasihi wazazi wapeleke watoto wao shuleni ili wapate haki yao ya msingi ya kuendelezwa.