Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara umeme bado ni ndoto kwa wengi- Ripoti 

7 Juni 2021

Ingawa katika muongo mmoja uliopita idadi kuwa ya watu duniani wamepata fursa ya nishati ya umeme kuliko wakati mwingine wowote , katika ukanda wa Afrika ulio Kusini mwa Jangwa la Sahara idadi ya watu wasio na nishati hiyo imeongezeka.  

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya kimataifa likiwemo la Umoja wa Mataifa la nguvu za atomiki, IAEA, shirika la kimataifa linalohusika na nishati jadidifu IRENA, Idara ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na maendeleo DESA, Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani,  WHO
Ripoti hiyo inayofuatilia hatua zilizopigwa katika utimizaji wa lengo namba 7 la malengo ya maendeleo endelevu linalohusu nishati, imeonya kwamba endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa nishati ya umeme basi dunia haitoweza kutimiza lengo la kuhakikisha fursa  ya kuwa na nishati ya gharama nafuu, ya kuaminika na endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.  

Ripoti imesisitiza kwamba “lazima pengo la usawa katika nishati lizibwe na suluhu endelevu zipatikane zikilenga nchi za Afrika ambazo zimeachwa nyuma katika lengo la kimataifa la fursa ya kimataifa ya nishati kwa wote.” 

Nyaya za umeme Afrika
World Bank/John Hogg
Nyaya za umeme Afrika

NIGERIA, DRC NA ETHIOPIA HAZINA UMEME WA KUTOSHA 

Kwa mujibu wa ripoti katika miaka 10 iliypopita tangu mwaka 2010, hatua zimepigwa katika ufikiaji wa lengo namba 7 la nishati lakini hatua hizo haziko sawia katika kanda mbalimbali. 

Watu zaidi ya bilioni moja wamepata fursa ya nishati ya umeme duniani kote lakini wakati huo huo watu milioni 30 wengi wakiwa kutoka katika mataifa ya Afrika athari za janga la Corona au COVID-19 zimefanya washindwe kumudu huduma za nishati ya umeme na nchi zinazoongoza kwa kutokuwa na fursa kubwa ya nishati hiyo ni Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Ethiopia ambayo sasa imeipuku India na kushika namba tatu duniani kwa kukosa nishati hiyo muhimu. 

Duniani kote ripoti inasema, idadi ya watu wasiokuwa na huduma ya umeme ilipungua kutoka bilioni 1.2 mwaka 2010 hadi milioni 759 mwaka 2019.  

Huduma za umeme kupitia suluhisho jadidifu zinazidi kushika kasi. Idadi ya watu waliounganishwa na gridi ndogo imeongezeka zaidi ya mara mbili kati ya 2010 na 2019, kutoka watu milioni 5 hadi watu milioni 11.  

Lakini, chini ya sera za sasa ilizopangwa na athari kubwa za janga la COVID-19, watu wanaokadiriwa kuwa milioni 660 bado hawatakuwa na fursa ya nishati hiyo ifikapo mwaka 2030, na wengi wao wakiwa Kusini mwa Jangwa la Sahara. 

THELUTHI MOJA YA WAKAZI WA DUNIA HAWANA UMEME

Wakati huo huo, watu wengine bilioni 2.6 walibaki bila nishati safi ya kupikia mwaka 2019, ikiwa ni theluthi moja ya idadi ya watu wote ulimwenguni.  

Udumavu mkubwa wa maendeleo ya upatikanaji wa nishati hiyo tangu mwaka 2010 husababisha mamilioni ya vifo kila mwaka kutokana na matatizo ya kupumua yanayosababishwa na moshi wa kupikia, na bila hatua za haraka za kuongeza nishati safi ya kupikia dunia itapungukiwakatika kutimiza lengo lake kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030. 

Hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara imeelezwa imeelezwa kuwa ongezeko la idadi ya watu ni kubwa kuliko fursa ya kufikia nishati hiyo, hivyo watu milioni 910 katika ukanda huo wanakosa nishati safi ya kupikia.  

Taa za sola zinapatiwa chaji badala ili zitumiwe na wavuvi badala ya koroboi za mafuta ya taa. Mradi huu umepata ufadhili wa UNEP, Tanzania.
UN/Tanzania
Taa za sola zinapatiwa chaji badala ili zitumiwe na wavuvi badala ya koroboi za mafuta ya taa. Mradi huu umepata ufadhili wa UNEP, Tanzania.

Nchi 20 za juu zenye upungufu mkubwa wa nishati hiyo zinashikilia asilimia 81 ya idadi ya watu duniani ambao wanaishi bila kupata mafuta safi na teknolojia.  

Kati ya hizi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia, Madagaska, Msumbiji, Niger, Uganda na Tanzania walikuwa na idadi ya chini au sawa na asilimia 5 ya watu wao ndio walio na fursa ya  kupata nishati safi ya kupikia.  

Na katika upande wa Habari njema Indonesia, Cambodia na Myanmar wanapiga hatua kila mwaka katika kipindi chote cha uandishi na tathimini ya ripoti hii. 

NJIA YA KUZIBA PENGO

Ripoti hiyo inachunguza njia anuwai za kuziba pengo hilo ili kufikia SDG7, na moja ya njia kubwa ni kuongeza kiwango cha matumizi ya nishati jadidifu  ambazo zimethibitisha ustahimilivu kuliko sehemu zingine za sekta ya nishati wakati wa janga la COVID-19.  

Wakati nishati jadidifu au mbadala imeshuhudia ukuaji ambao haujawahi kutokea katika muongo mmoja uliopita, sehemu kubwa ya matumizi ya nishati ilibaki kuwa thabiti wakati matumizi ya nishati ya ulimwengu yalikua kwa kiwango sawa.  

Nishati jadidifu zina nguvu zaidi katika sekta ya umeme, zilifikia karibu asilimia 25 mwaka 2018, wakati maendeleo katika sekta ya kupasha joto na uchukuzi yamekuwa polepole sana. 

Zaidi ya theluthi moja ya ongezeko la uzalishaji wa nishati mbadala mwaka 2018 inaweza kuhusishwa na Asia ya Mashariki inayochangiwa na unyakuzi mkubwa wa nishati ya jua au sola na ya upepo nchini China. 

Maendeleo makubwa zaidi ya kiwango cha nchi katika nishati mbadala kwa mwaka 2018 yalionekana nchini Uhispania, kwa sababu ya uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji, ikifuatiwa na Indonesia ambapo uzalishaji wa haraka wa nishati itokanayo na kinyesi imebeba jukumu kubwa.  

Ili kuongeza kwa kiasi kikubwa sehemu ya nishati mbadala kulingana na lengo la SDG 7, juhudi za sasa zinahitaji kuharakishwa katika sekta zote za matumizi ya nishati hiyo kwa watumiaji katika mahitaji ya jumla ya nishati. 

Uboreshaji wa kiwango cha nishati (wakala wa ufanisi wa nishati) unasonga mbali zaidi kutoka kwenye lengo lililowekwa la  SDG7 kufikia 2030.  

Kiwango cha uboreshaji wa nishati ya msingi ulimwenguni mwaka 2018 kilikuwa asilimia 1.1 ikilinganishwa na 2017, kikiwa ni kiwango cha chini cha wastani cha maboresho tangu 2010.  

Uboreshaji wa kila mwaka hadi 2030 sasa utahitaji wastani wa asilimia 3 ikiwa tunataka kufikia lengo imesema ripoti. 

Kuongeza kasi ya maendeleo katika kanda na viashiria vyote itahitaji kujitolea kwa nguvu kwa kisiasa, mipango ya muda mrefu ya nishati, sera za kutosha na motisha ya kuongeza kasi ya utafutaji wa suluhu endelevu za nishati. 

UFADHILI WA KIMATAIFA WAHITAJIKA

Mtiririko wa kifedha wa kimataifa kwa umma kwenda nchi zinazoendelea ili kusaidia nishati safi ulifikia dola bilioni 14 mwaka 2018, ukiwa umepungua kwa asilimia 35 kutoka kiwango cha juu kabisa cha dolabilioni 21.9 mwaka uliotangulia.  

Ripoti inasemka lakini, mwenendo wa jumla wa mtiririko wa kifedha kwa umma umekuwa mzuri katika muongo mmoja uliopita, na kuongezeka mara tatu katika kipindi cha  kati yam waka 2010-18 ikionekana kuwa na wastani wa ongezeko kwa miaka mitano.  

Mwenendo huu, hata hivyo, unafichamapengo muhimu ya usambazaji, na ahadi za kifedha zimejikita katika nchi chache na kwa hivyo kushindwa kufikia wengi wale wanaohitaji zaidi msaada wa kimataifa.  

Nchi 46 zilizo na maendeleo duni zaidi (LDCs) zilipokea asilimia 20 tu ya msaada wa kifedha wa umma kwa kipindi cha kati ya mwaka 2010-18 na jumla ya dola bilioni 2.8 mwaka 2018 kiwango sawa na cha mwaka 2017 lakini chini kuliko kiwango cha mwaka 2016 na 2015.  

Msaada wa kifedha wa kimataifa unahitaji kuongezwa zaidi na kulenga zaidi nchi hizo ambazo ziko nyuma zaidi kufikia lengo la SDG 7.  

Katikati ya janga la COVID-19, ambalo limeongeza sana mtazamo wa hatari ya wawekezaji na kuhamisha vipaumbele vya ufadhili wa umma katika nchi zinazoendelea, msaada wa kimataifa wa kifedha kwa umma ni muhimu zaidi kuliko hapo awali ili kukuza viwango vya uwekezaji vinavyohitajika kufikia SDG 7. 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter