Skip to main content

Nchi za Afrika ya Kati zimedhibiti vyema COVID-19-UN

Msanii akichora picha kwenye ukuta jinsi ya mbinu za mtu kujikinga dhidi ya virusi vya COVID-1 nchini Jamhuri ya afrika ya kati, CAR..
MINUSCA/Screenshot
Msanii akichora picha kwenye ukuta jinsi ya mbinu za mtu kujikinga dhidi ya virusi vya COVID-1 nchini Jamhuri ya afrika ya kati, CAR..

Nchi za Afrika ya Kati zimedhibiti vyema COVID-19-UN

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ukanda wa Afrika ya Kati François Louncény Fall amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa harakati za serikali kwenye ukanda huo pamoja na wadau wao kukabili janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 zimewezesha ukanda huo kuwa wenye idadi ndogo zaidi ya wagonjwa na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo barani Afrika.
 

Bwana Fall ambaye pia ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika ukanda wa AFrika ya Kati, UNOCA, mesema COVID-19 imeendelea kuathiri shughuli zetu lakini hali imeendelea kuwa bora kutokana na mipango mchanganyiko ya utoaji wa chanjo na uhamasishaji wa kujikinga, mipango ambayo inatekelezwa na serikali kwenye ukanda huu.”

UNOCA inasimamia nchi za Angola, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Equatorial Guinea, Gabon, Rwanda na Sao Tome na Principe.

Mwakilishi huyo amesema eneo hilo ndio linasalia kuwa na idadi ndogo ya maambukizi na vifo kutokana na COVID-19 ambapo “hadi tarehe 15 mwezi Mei, takwimu rasmi zinaonesha idadi ya wagonjwa ni 222,882 na kati yao hao waliofariki dunia ni 3,635.”

Amesema mikakati ya kinga iliwezesha hata serikali ya Burundi kuitisha kikao cha 51 cha kamati ya ushauri ya masuala ya ulinzi Afrika ya Kati, UNSAC, kikao kilichofanyika kwa njia ya kawaida tarehe 28 mwezi Mei mjini Bujumbura na kudhihirisha “mnepo wa eneo la Afrika ya Kati la kusaka kujikwamua kiuchumi na kijamii huku likizingatia hatua za kujikinga na COVID-19.”

Kampeni ya taarifa kuhusu COVID-19 kwenye mji mkuuu wa CHad, N'Djamena.
© UNICEF/Martina Palazzo
Kampeni ya taarifa kuhusu COVID-19 kwenye mji mkuuu wa CHad, N'Djamena.

Usalama Chad

Akizungumzia amani na usalama Bwana Fall  amegusia Chad ambako amesema hali ya utulivu ilizorota kufuatia kifo cha Rais Idriss Déby Into.

“Yaliyojiri baada ya kifo chake yamedhihirisha changamoto zinazokabili ukanda huu pindi kunapotokea mabadiliko ya ghafla ya serikali. Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono juhudu ya Muungano wa Afrika na Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati, ECCAS ili hatimaye kuunga mkono harakati za mazungumzo jumuishi na hatimaye kipindi cha mpito cha kurejesha utawala wa kidemokrasia na kikatiba,” amesema Bwana Fall.

Kuhusu vitisho vya Boko Haram kwenye Ziwa Chad, Mwakilishi huyo amesema ni jambo linalomtia wasiwasi mkubwa. “Na zaidi ya hayo, kwa mujibu wa ripoti, vikundi kinzani vya kigaidi ikiwemo Boko Haram na kile cha Islamic West Africa Province vimekuwa vikipambana kusaka umiliki wa eneo hili. Timu ya hivi karibuni ya UNOCA na ofisi ya Umoja wa MAtaifa Afrika Magharibi, UNOWAS imebaini kuwa kadri hali ya usalama inavyozidi kudorora kwenye eneo hili, ushirikiano baina ya nchi zinazoathiriwa na mashambulizi kutoka kwa magaidi hayo unapaswa kuimarishwa.”

Halikadhalika amesema mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka huku rasilimali zikipungua na hali ya maisha ya makundi yaliyo hatarini kama vile wakimbizi, wanawake na watoto na viijana zinazidi kudorora.
Bwana Fall amesihi Baraza la Usalama liongeze muda wa UNOCA ambao unamalizika hivi karibuni, ili hatimaye iweze kuendeleza harakati za kusongesha amani na usalama kwenye ukanda huo. “Katika ripoti yake, Katibu Mkuu amependekeza kuwa muda wa UNOCA uongezwe kwa miaka mitatu kuanzia tarehe mosi mwezi Septemba mwaka 2021 hadi tarehe 31 Agosti mwaka 2024.”