Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvuvi haramu unapoteza hadi tani milioni 26 za samaki kwa mwaka - FAO 

Wavuvi wakishusha mzigo katika soko la samaki.
UN Photo/M Guthrie
Wavuvi wakishusha mzigo katika soko la samaki.

Uvuvi haramu unapoteza hadi tani milioni 26 za samaki kwa mwaka - FAO 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo Juni 5, Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Uvuvi Haramu, usiyoripotiwa na usiodhibitiwa, inasisitiza ujumbe kwamba juhudi za kimataifa za kuhakikisha uendelevu wa uvuvi wa kawaida zimeathiriwa sana. 

Siku hii ilipitishwa mnamo mwaka 2017 katika azimio la Mkutano Mkuu. Hati hiyo pia inatangaza kwamba 2022 utakuwa Mwaka wa Kimataifa wa Uvuvi mdogo na Kilimo cha Baharini ambacho kinajumuisha ugugaji wa viumbe bahari pamoja na ukuzaji wa mimea. 

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linakadiria kuwa uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa husababisha upotezaji wa tani milioni 11 hadi 26 za samaki kila mwaka. Hasara za kiuchumi ni kati ya dola bilioni 10 hadi 23. 

Shughuli inayozingatiwa kama chanzo muhimu cha chakula, ajira, starehe, biashara na ustawi wa uchumi inakabiliwa na mazoea haramu katika ulimwengu ambao idadi ya watu inakua, na njaa inaendelea. Samaki inachukuliwa kuwa bidhaa muhimu kwa kuhakikisha uhakika wa chakula. 

Mifumo ya ikolojia ya pwani na baharini hutoa chakula, maisha, na ulinzi wa pwani kwa zaidi ya watu bilioni moja ulimwenguni.
UNCTAD
Mifumo ya ikolojia ya pwani na baharini hutoa chakula, maisha, na ulinzi wa pwani kwa zaidi ya watu bilioni moja ulimwenguni.

 

FAO inakadiria kuwa uzalishaji wa ulimwengu ulifikia karibu tani milioni 179 mnamo 2018. Sekta za uvuvi na ufugaji wa samaki zimekua sana katika miongo ya hivi karibuni. 

“Watumiaji, wataalam na wapenzi wa bahari ulimwenguni kote lazima wazuie mazoea haramu.” FAO imesisitiza. 

Lengo la 14 la Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu linalenga hasa kudhibiti uvuvi wa samaki, kutokomeza uvuvi wa samaki kupita kiasi na haramu, uvuvi usioripotiwa na usiodhibitiwa, pamoja na vitendo vya uharibifu vinavyofanyika katika sekta hii.