Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanufaika wa Ziwa Victoria Tanzania walalama kina cha maji kuongezeka

Ngalawa hii iliyotengenezwa kwa taka za plastiki ilisafirishwa kutoka Mwanza hadi Dar es salaam kuelimisha jinsi taka zinaweza kugeuzwa kuwa kitu cha  manufaa.
Fredy Anthony Njeje
Ngalawa hii iliyotengenezwa kwa taka za plastiki ilisafirishwa kutoka Mwanza hadi Dar es salaam kuelimisha jinsi taka zinaweza kugeuzwa kuwa kitu cha manufaa.

Wanufaika wa Ziwa Victoria Tanzania walalama kina cha maji kuongezeka

Tabianchi na mazingira

Tarehe 5 mwezi huu wa Juni, Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la mazingira, UNEP unazindua muongo wa Umoja wa Mataifa wa mrejesho wa mfumo wa ikolojia ulioharibika.Hii ina maana miaka 10 ya kurejesha hali ya mazingira iwe angani, ardhini au majini. Uzinduzi huu unafanyika kuelekea siku ya mazingira duniani tarehe 5 mwezi huu wa Juni. 

 

Soundcloud

Kauli mbiu ni Fikiria Upya! Jenga Upya na Rejesha Upya! Hii ni kwa kuzingatia kuwa hivi sasa mazingira duniani yameharibiwa na kuwa chanzo siyo tu cha magonjwa bali pia majanga ya asili. Mathalani katika Ziwa Viktoria maji yanaongezeka ambapo shuhuda ni mvuvi aitwaye Mtima.

Dagaa wamepotea uduvi ndio umeshamiri

Mtima anasema “maji yanaongezeka. Mimi kweli nina hasira kwa sababu maji yanavyoongezeka hivi ina maana haya maji ni machafu ya mwaloni na yanaingia kwenye mtumbwi na inakuwa ni shida.”

Kilio hicho ni cha Mtima, mvuvi huyu katika Ziwa Viktoria mkoani Mwanza nchini Tanzania ambalo hivi sasa maji yanajaa kupita kiasi na kuleta adha kwa wavuvi. Kilio cha Mtima kinaungwa mkono na  Mwajuma Chamhiro mkazi na mdau wa mwalo wa Mswahili  ambaye pia yuko katika kikundi cha kutunza mazingira.

Mwajuma anasema “hali ya zamani ya maji ilikuwa ni vizuri na maji yalikuwa kina cha karibu, na tulikuwa tunapata kwa urahisi mazao ya ziwani. Hivi sasa hali ni mbayá maji ni mengi. Vitu vimepanda bei, dagaa tunanunua kisado elfu 15, hatuna kitu tunachokifanya.”

Mvuvi Mashauri Yohana anasema maji zamani yalikuwa kimo cha kati lakni sasa “ni mengi sana kulingana na mvua zinavyonyesha. Uvuvi sasa umekuwa mgumu kiuchumi. Dagaa wanapatikana au wasipatikane, Hivi sasa hakuna dagaa na uduvi ndio mwingi.”

Chupa hizi za plastiki zilikuwa taka lakini sasa zimegeuzwa pambo na kuoneshwa wakati ngalawa iliyotokana na taka za plastiki na kandambili ilipowasili Mwanza nchini Tanzania.
Fredy Anthony Njeje
Chupa hizi za plastiki zilikuwa taka lakini sasa zimegeuzwa pambo na kuoneshwa wakati ngalawa iliyotokana na taka za plastiki na kandambili ilipowasili Mwanza nchini Tanzania.

Bodi ya bonde la Ziwa Viktoria nayo iko makini

Kwa mujibu wa afisa habari wa bodi ya bonde la ziwa Victoria Gerald  Itembu, mwezi Mei mwaka 2020 wastani wa kina cha maji  ziwani ulikuwa  mita 1134.27 lakini kwa mwaka huu wa  2021 kiwango kimeongezeka kwa 0.60 na kufikia mita 1134.87 ambazo hazijawahi kufikiwa katika kipindi chote. 

Sasa bodi hiyo inachukua hatua akisema, “tumekuwa tunatoa elimu kwa njia mbali mbali. Mfano watu wa viwanda, badala ya maji yale kuyamwaga ziwani basi watafute njia ya kuyatakasa na kuyatumia tena hata kwa bustani ili kuhakikisha matumizi sahihi ya maji na pia mazingira yasiathirike. Halikadhalika kuepuka ufugaji kupita kiasi na kilimo tuzingatie kisichoharibu mazingira.”

Melissa Deogratius anatoka Umoja wa Wauza Samaki Kamanga na pia anahusika na hatua za kuhifadhi mazingira akisema kwamba wanashiriki harakati za kulinda mazingira “kuna gari la Green Waste huwa linakusanya uchafu. Kuna sehemu ya kukusanyia uchafu na gari linabeba na kupeleka dampo. Na wageni wakija hapa kuchanga samaki kuna mahali pa kutupa taka na pia kujisaidia kuna vyoo.”

Serikali piteni mara kwa mara kutuelimisha

Kwa mfanyabiashara wa samaki, Filbert Magere anasema sheria zipo, na taka za kuchomwa zinachomwa na za kutupa zinakusanywa na gari na zaidi ya yote, “serikali iwe inapita mara kwa mara ili kutuelimisha kwa sababu wengine hawaelewi na hivyo wakielewa tutaweza kuhifadhi mazingira kando mwa ziwa.”

Baraza la Taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini Tanzania, NEMC nalo linatambua changamoto za kimazingira katika Ziwa Viktoria ambapo Kaimu Meneja wa NEMC kanda ya Ziwa Boniphace Chacha anafafanua akisema, “tunaendelea kutoa elimu kwa umma kwamba maeneo yaliyo ndani ya mita 60 kutoka Ziwani  yanatakiwa yaachwe wazi na yasitumike kwa shughuli ambazo zinaharibu bayonuai ya viumbe vilivyoko kwenye maeneo hayo.

Serikali iwe inapita mara kwa mara ili kutuelimisha kwa sababu wengine hawaelewi na hivyo wakielewa tutaweza kuhifadhi mazingira kando mwa ziwa.- Filbert Magere- Mfanyabiashara Mwanza

Kwa mujibu wa Clara Makenya, Mwakilishi wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP nchini Tanzania tayari chombo hicho kimechukua hatua kurejesha ikolojia.

Muongo wa Mrejesho kuondoa makovu

Mkutano Mkuu wa UNEP wa mwaka 2019 ulitangaza mwaka 2021 hadi 2030 kuwa muongo wa mrejesho wa mfumo wa Ikolojia. “Kwa hiyo huu muongo unazinduliwa rasmi tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu wa 2021 ambayo ni siku ya mazingira duniani kwa lengo la kuangalia ni vipi kila mdau kuanzia mtu binafsi hadi kitaifa na kimataifa tunaweza kushirikiana kurejesha mfumo wa kiekolojia ambao umeharibika vibaya sana. Tunataka kuangalia uwezekano wa kurejesha hekta milioni 350 za ardhi duniani ambazo zimeharibika.”

Amesema changamoto zilizosababisha kuanzishwa kwa muongo huo ni matumizi mabaya ya rasilimali ambayo yamesababisha uharibifu wa bayonuai na pia uharibifu wa mazingira ikiwemo ardhi na udongo ambao kwa kiasi kikubwa ndio chanzo cha uchumi na chakula kwa viumbe vya dunia.