Baiskeli siyo tu inapunguza uchafuzi wa mazingira bali pia inajenga afya

3 Juni 2021

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya uendeshaji baiskeli duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uendeshaji baiskeli siyo tu unahifadhi mazingira kwa kupunguza utoaji wa hewa chafuzi za kwenye magari bali pia unapunguza gharama kwa mtumiaji na kujenga afya. 
 

Kupitia ujumbe wake wa siku ya leo, Katibu Mkuu anasema, “baiskeli ni uhuru; baiskeli inafurahisha. Ni nzuri kwa afya ya mtu- kimwili na kiakili na ni nzuri kwa sayari yetu pekee ya dunia. Baiskeli ni maarufu sana kwa uwezo wake wa kumpatia mtu mazoezi na usafirishaji siyo tu kwenda shuleni, madukani na kazini lakini pia kwa uendelevu wa mustakabali wetu.”
Amefafanua kuwa ndio mantiki ya siku ya leo ya uendeshaji baiskeli duniani akisema inatoa fursa ya kuangazia umuhimu wa usafiri huu usiotumia nishati ya mafuta au umeme na nafasi yake katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na wakati huo huo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hii leo kuna takribani baiskeli bilioni 1 duniani kote , idadi ambayo ni kama ya abiria wanaotumia usafiri wa magari.
Guterres anasema matumizi ya baiskeli yanakwenda kizazi hadi kizazi na pindi mtu anapokuwa amejifunza katu hatosahau.
“Hata kabla ya janga la COVID-19, uendeshaji baiskeli ulikuwa moja ya njia muhimu za usafiri na mipango ya kupeana baiskeli ili kuendesha inazidi kuongezeka na hivyo kutoa fursa nafuu zaidi ya kutumia baiskeli wa safari fupi,” amesema Guterres.
Ameongeza kuwa janga la Corona limebadilisha mahitaji ya usafiri na tabia za binadamu na kuchochea miji kufikiria upya mifumo yao ya usafiri huku baiskeli zikiwa na dhima muhimu zaidi za usafiri nafuu na usiochafua mazingira.
Ni kwa mantiki hiyo anasema mabadiliko hayo yanatoa fursa zaidi ya kutumia baiskeli sambamba na kuimarisha usalama barabarani kwa watumiao usafiri huo ikiwemo kuwepo kwa eneo maalum la waendesha baiskeli.
“Tunapojiandaa kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa usafiri endelevu utakaofanyika Beijing China mwezi Oktoba, hebu na tuahidi kusaidia ili usafiri wa baiskeli uwe bora na salama.”
Na kwa siku ya leo, Katibu Mkuu aesema baiskeli iwe kwa michezo au mazoezi au kwenda madukani, “hebu tuendelee kuitumia.”
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter