Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbegu asili matumaini mapya kwa wakazi wa Caatinga Brazil.

Shughuli za kilimo nchini Brazil.
World Bank/Scott Wallace
Shughuli za kilimo nchini Brazil.

Mbegu asili matumaini mapya kwa wakazi wa Caatinga Brazil.

Ukuaji wa Kiuchumi

Mbegu asilia za mazao zimebaki kuwa tumaini kubwa kwa wakulima wa Caatinga nchini Brazil ambao wameshuhudia athari za mabadiliko ya tabia nchi kutokana na ukataji na uchomaji miti pamoja na ufugaji za mifugo mingi.

Mradi wa kuwawezesha wakulima walio na mbegu asilia kusambaza kwa wananchi wengine unaoendeshwa na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD, umewawezesha walezi au wahifadhi wa mbegu hizo kulima na kuwauzia wanajamii wenzao. 

Msimu wa Mavuno, Kaskazini Mashariki mwa Brazil, Adelina na Mjukuu wake Jucimara wakiwa shambani kuvuna mazao ambayo mbegu zake zilipandwa na mababu zao.

Familia hii iliyopo katika mji wa Caatinga, inajulikana kwa jina la walezi wa mbegu, mbegu zao ni zile asilia zinazoweza kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na wana zaidi ya mbegu aina 235 zikiwemo mahindi, nyanya, maboga, na mbegu za miti asilimia ambazo kwa zaidi ya muongo mmoja wamekuwa wakipanda, kuvuna, na kuhifadhi mbigu hizo ili ziweze kuwepo kwa kizazi cha sasa na baadae.

Jucimara anasema mbegu hizo pia wanauza kwa wakulima wengine ili waweze kupambana na mabadiliko ya tabianchi. “Kwa sasa, katika maeneo yenye hali ya ukame naona mbegu za asili ndio tumaini let pekee kwa kizazi kijacho”

Brazil, moja ya nchi zilizobarikiwa utajiri wa bayonuai duniani, lakini wakazi wake wa kusini mashariki wako kwenye umasikini mkubwa. Eneo hili awali lilikuwa na rutuba nzuri lakini lakini ufugaji mkubwa wa mifugo, ukataji miti, kuchoma ardhi moto, pamoja na uvunaji wa kuni kupita kiasi vimesababisha uharibifu wa mazingira na bayonuai ya kipekee ya Caatinga.

Kupitia mradi unaoendeshwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa wa maendeleo ya kilimo duniani, IFAD kwa kushirikiana na serikali ya mji wa Bahia, Adeline na mjukuu wake Jucimara ni miongoni mwa walezi wa mbegu zaidi ya 420 katika kijiji cha  Caatinga ambako kunaendeshwa programu maalum ya kuwafundisha namna bora ya kuhifadhi mbegu hizo pamoja na kupunguza uharibifu wa chakula.

“Mbegu hizi zinazo himili eneo lenye hali ya ukame ni muhimu sana kwasababu pamoja na kuhifadhi mimea lakini linasaidia uwepo wa chakula na kusaidia uchumi katika mji wetu, na uchumi ukianza kukuwa maisha ya wananchi nayo yana yanaboreka.” amesema Jucimara.

Familia hii pamoja na nyingine wameanzisha benki maalum ya kuhifadhi na kuuza mbegu asilia ambazo kwa sasa zimepanda bei kutokana na uhitaji mkubwa.

Mbali na kipato hicho lakini bibi Adeline anatamani watu wengi zaidi warithi kazi yake “Natamani sana kila mtu, wajukuu zangu, watoto wao warithi, ilimradi nipo hai na ninaweza kusimama nataka niendelee kufanya kazi na kutunza mbegu zangu”

Japo bayanuai inaendelea kuharibika lakini bado kuna jamii ndogo vijijini ambazo zinafanya jukumu lao la kuhifadhi mbegu asilia ili ziweze kujikimu zenyewe, jamii zilizowazunguka na ulimwengu kwa ujumla.