Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MobiPay na ITC yajengea wakulima stadi mpya za kujiwekea akiba 

Mchuuzaji anatumia app kufikia wateja wakati wa masharti ya kufungwa kwa ajili ya COVID-19 Kampala, Uganda.
UNCDF
Mchuuzaji anatumia app kufikia wateja wakati wa masharti ya kufungwa kwa ajili ya COVID-19 Kampala, Uganda.

MobiPay na ITC yajengea wakulima stadi mpya za kujiwekea akiba 

Ukuaji wa Kiuchumi

Ubia kati ya kampuni binafsi ya huduma za malipo kwa njia ya simu, MobiPay nchini Uganda na kituo cha Umoja wa Mataifa cha biashara, ITC umeondoa usumbufu wa malipo kwa wakulima baada ya mauzo yao na hata kuwajengea mbinu ya kisasa zaidi ya kujiwekea akiba ya fedha badala ya kuzitumia kiholela baada ya mauzo.

Nchini Uganda, katika moja ya shamba, wakulima wake kwa waume wakiendelea na shughuli za kilimo huku mmoja wao, Muwagabaza Jessica akikumbuka machungu waliyopitia awali kabla ya Mobipay, ambapo malipo ya mauzo, wakati mwingine kwa baadhi ya wakulima yalikuwa yanacheleweshwa. 

Kwa mujibu wa Eric Agyei, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mobipay, lengo la shirika lao ni kuwezesha wakulima kupata mikopo, pembejeo na taa pamoja na mitambo ya umwagiliaji ituamiayo sola. 

Wakulima walikopeshwa simu za kiganjani kuweza kupata malipo lakini pia huduma za pembejeo kupitia  wajasiriamali wa kidijitali kwenye jamii, au DCE. 

Mmojawao ni Mirembe Berna. “Kama DCE natembelea wakulima kufahamu mahitaji ya kuinua kilimo chao, kisha naenda kwa afisa ugani au nampigia simu na kumwelezea mahitaji.” 

Kupitia simu, afisa ugani anatambua mahitaji ya pembejeo na kisha kusambazia wakulima katika maeneo yao. 

Sasa Jessica anasema  kilimo kimekuwa  bora na kinalipa, wanapata pembejeo na wana uhakika wa malipo. Na zaidi ya yote Jessica anasema “tangu Mobipay imekuja, mambo ni mazuri. Kila mtu anapokea fedha kwenye simu yake. Sasa familia zina furaha, na familia pia. Awali tulilipwa fedha taslimu na tulitumia hovyo. Lakini sasa tunapokea fedha kwenye simu, tukiwa na familia na tunapanga bajeti pamoja. Unaona hata tabia ya utunzaji wetu wa fedha imebadilika.” 

Mobipay mpaka sasa imesambaza kupitia mpango wake wa mkopo simu Elfu 12 kwa wakulima, huku kaya Elfu 13 zikipatiwa taa za sola na mitambo ya umwagiliaji kwa kutumia nishati ya sola.