Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ya Sinovac dhidi ya COVID-19 sasa rukhsa kutumika kwa dharura:WHO 

Sinovac-CoronaVac chanjo ya COVID-19
Sinovac
Sinovac-CoronaVac chanjo ya COVID-19

Chanjo ya Sinovac dhidi ya COVID-19 sasa rukhsa kutumika kwa dharura:WHO 

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, leo limeithibitisha chanjo ya Sinovac-CoronaVac dhidi ya corona au COVID-19 kwa matumizi ya dharura, ikizipa nchi, wafadhili, wakala wa ununuzi na jamii hakikisho kwamba inakidhi viwango vya kimataifa vya usalama, ufanisi na utengenezaji.  

Chanjo hiyo inatengenezwa na kampuni ya dawa ya Beijing ya Sinovac.  

"Dunia inahitaji sana chanjo nyingi za COVID-19 kushughulikia ukosefu mkubwa wa ufikiaji wa chanjo kote ulimwenguni," amesema Dkt. Mariângela Simão, mkurugenzi mkuu msaidizi wa Upataji wa bidhaa za afya katika shirika la WHO.  

Ameongeza kuwa "Tunawahimiza watengenezaji kushiriki katika kituo cha kimataifa cha upatikanaji wa chanjo COVAX, na washiriki maarifa yao, takimu zao na wachangie kudhibiti janga hilo."  

 

Matumizi ya dharura ya chanjo 

 

Orodha ya matumizi ya chanjo ya dharura ya WHO (EUL) ni sharti kwa ajili ya usambazaji wa chanjo kupitia mkakati wa kituo cha kimataifa cha chanjo COVAX na ununuzi wa kimataifa.  

Pia inaruhusu nchi kuharakisha idhini yao ya kisheria ya kuagiza na kusimamia chanjo za COVID-19. 

EUL inatathmini ubora, usalama na ufanisi wa chanjo za COVID-19, pamoja na mipango ya usimamizi wa hatari na program zinazofaa, kama mahitaji ya mnyororo wa mipango ya uhifadhi wa baridi.  

Tathmini hufanywa na kikundi cha tathmini ya bidhaa, kilichoundwa na wataalam wa sheria kutoka duniani kote na kikundi cha ushauri wa kiufundi (TAG), kinachohusika na kufanya tathmini ya faida na hatari kwa ajili ya kutoa mapendekezo huru ya ikiwa chanjo inaweza kuorodheshwa kwa matumizi ya dharura na, ikiwa ni hivyo, chini ya hali gani. 

Katika chanjo ya Sinovac-CoronaVac, tathmini ya WHO imejumuisha ukaguzi wa kituo cha uzalishaji. 

 

Kuhusu chanjo ya Sinovac-CoronaVac 

 

Bidhaa ya Sinovac-CoronaVac ni chanjo inayotumia virusi vilivyokufa vya corona. Urahisi wake wa kuihifadhi hufanya iweze kudhibitiwa vyema na inafaa haswa kwa mazingira yenye rasilimali ndogo. 

Kikundi cha wataalam wa kimkakati cha ushauri wa chanjo (SAGE) pia kimekamilisha ukaguzi wake wa chanjo hiyo.  

Kwa msingi wa ushahidi uliopo, WHO inapendekeza chanjo hiyo kutumiwa kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 na zaidi, katika ratiba ya kupatiwa dozi mbili na kwa nafasi ya wiki mbili hadi nne.  

Matokeo ya ufanisi wa chanjo hiyo yameonyesha kuwa chanjo ilizuia dalili za ugonjwa kwa asilimia 51% ya wale waliopewa chanjo na kuzuia  hali mbaya ya COVID-19 na kulazwa hospitalini kwa asilimia 100 ya watu walioitumia kwa majaribio. 

Watu wazima wakubwa (zaidi ya miaka 60) waliandikishwa katika majaribio ya kliniki, kwa hivyo ufanisi hauwezi kukadiriwa katika kikundi hiki cha umri.  

Lakini, WHO haipendekezi kikomo cha juu cha umri kwa chanjo hii kwa sababu takwimu zilizokusanywa wakati wa matumizi ya majaribio katika nchi nyingi na takwimu za kinga ya mwili zinadhibitisha kuwa chanjo hiyo inaweza kuwa na athari nzuri ya kinga kwa wazee.  

Hakuna sababu ya kuamini kuwa chanjo ina maelezo tofauti ya usalama kwa idadi ya wazee na vijana.  

WHO inapendekeza kwamba nchi zinazotumia chanjo hiyo kwa wazee zifuate usalama na ufuatiliaji wa ufanisi ili kudhibitisha athari inayotarajiwa na kuchangia kulifanya pendekezo kuwa thabiti zaidi kwa nchi zote.