WFP yafikishia misaada ya chakula watu milioni 1 huko Tigray

1 Juni 2021

Idadi ya watu waliopatiwa msaada wa chakula na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP huko jimboni Tigray nchini Ethiopia tangu  mwezi Machi mwaka huu imefikia milioni moja. 

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Mekele nchini Ethiopia imesema mtu wa milioni 1 kupatiwa msaada huo ni Aster Bayene mama wa watoto saba ambaye siku ya Jumatatu alipatiwa unga wa ngano, maharagwe na mafuta ya kupikia. 

 Aster, mwenye umri wa miaka 43, alipoteza nyumba yake pamoja na mazao yote kutokana na mapigano jimboni humo. 

 “Nimekuwa nategemea chakula kidogo ninachopata kutoka kwa majirani zangu. Angalau sasa nimepata unafuu baada ya machungu mengi,” amesema Aster ambaye ni mkazi wa Adi Millen, kijiji kilichoko kilometa 50 kaskazini-magharibi mwa Tigray. 

Yeye ni miongoni mwa wanakijiji 4,500 waliopatiwa msaada katika mgao wa kwanza wa WFP, mgao ambao utakuwa unatolewa kila baada ya wiki sita. 

Mama ambaye amefurushwa kutoka ukanda wa Magharibi wa Tigray nchini Ethipia akizungumza na mfanyakazi wa UNICEF mjini Mekelle
UNICEF/Esiey Leul Kinfu
Mama ambaye amefurushwa kutoka ukanda wa Magharibi wa Tigray nchini Ethipia akizungumza na mfanyakazi wa UNICEF mjini Mekelle

Ameshukuru WFP kuwafikishia msaada wa chakula akisema “eneo letu hili la Adi Millen liko ndani mno na masoko yako mbali.” 

WFP ina wajibu wa kusambaza misaada ya dharura katika kanda za kaskazini-magharibi na kusini jimboni Tigray na lengo lake ni kufikia watu milioni 2.1. 

Tangu mwezi Aprili, WFP imeweza kufikia wilaya zote 13 za kanda ya kaskazini-magharibi na kusaidia watu 885,000 people. 

Halikadhalika kanza ya kusini, WFP ilianza kufikisha misaada tangu mwezi Machi ambako hadi sasa watu 168,000 wamefikiwa na hivyo kufanya idadi ya watu Tigray waliopata msaada kufikia milioni 1.05. 

Hata hivyo WFP imesema inahitaij dola milioni 203 kuendelea na operesheni zake za kusambaza msaada Tigray ili kuokoa maisha ya watu hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter