Wakati Afya ipo hatarini, kila kitu kipo hatarini: WHO 

1 Juni 2021

Baraza la Afya duniani, limehitimisha kikao chake cha 74 kwa kupitisha azimio la kihistoria la kuimarisha utayari wa uwajibikaji wa shirika la afya ulimwenguni -WHO pindi dharura inapotokea.

Baraza hilo limepitisha azimio hilo huku Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt.Tedros Ghebreyesus, akipongeza nchi wanachama, kwa kupunguza vifo vitokanavyo na COVID-19 na kuonya litakuwa kosa kubwa iwapo watafikiri hatari ya janga hilo imeondoka. 

“Mchanganyiko wa mbinu za afya zinazoendana na uhalisia wa eneo, pamoja na chanjo, imesalia kuwa ndio njia sahihi. Nawasihi nchi wanachama, kujitolea katika kusaidia malengo tuliyoweka ambayo ni kuhakikisha angalau asilimia 10 ya watu wote ulimwenguni wamepata chanjo ifikapo mwezi septemba mwaka huu, na angalau asilimia 30 ifikapo mwisho wa mwaka.” Amesema Ghebreyesus 

Ameongeza kuwa siku moja, akiwa na matumaini hivi karibuni, janga hili litapita, lakini athari za kisaikolojia na makovu yataendelea kuwepo, hasa kwa wale waliopoteza wapendwa wao, watoa huduma wa afya ambao wamefanyakazi kupita kipimo, na mamilioni ya watu wa rika zote ambapo wamekaa miezi mingi wapweke wakiwa wamejitenga. 

“Usalama wa watu ulimwenguni hauwezi kuwa msaada kutoka serikali. Kila serikali inajukumu la kuhakikisha usalama wa raia wake, na nchi wanachama wataweza kuhakikisha raia wao wapo salama iwapo watatekeleza malengo yao kwa viwango vya kimataifa.” 

Nini kinachangia Janga kuleta athari kubwa 

Mkuu huyo wa WHO amesema, jambo kubwa linalosababisha janga liweze kutokea ni ukosefu wa ushirikiano, ushirikiano kwenye kutoa takwimu, taarifa za vimelea, teknolojia na rasilimali. Na hizo ndio changamoto wanazokabiliana nazo mpaka sasa, wamekuwa wakikabiliana nazo tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 na hata kabla ya janga hilo. 

Anaamini uwepo wa mkataba, ungesaidia ushirikiano bora , uaminifu na uwajibikaji na kuimarisha msingi thabiti wa kujenga mifumo mingine ya usalama wa afya ulimwengu, ya kutathmini uwezo wa nchi, kufanya utafiti na ubunifu, kutoa tahadhari mapema, kuweka mapema mahitaji na uzalishaji wa bidhaa zitakazo hitajika kipindi cha janga litakapo tokea, kuweka mikakati ya chanjo na makubaliano, pamoja na mengine mengi. 

Ametilia mkazo umuhimu wa wanachama wote, kufikia makubaliano ya kutengeneza na kuwa na makubaliano ya kimataifa, ambayo yataungwa mkono na kila mmoja kwakuwa kumekuwa na uwasikishi na ujumuishi. 

Anaamini iwapo mamuzi hayatafikiwa na kukubaliwa na wote, basi iwapo janga jingine litatokea kutakuwa na mzunguko wa yale yaliyotokea katika janga hili kitu ambacho ni hatari. 

Baraza hilo limemalizika likiwa limepitsha maazimio na maamuzi ziadi ya 30, juu ya ugonjwa wa kisukari, watu wenye ulemavu, kumaliza ukatili dhidi ya watoto, huduma ya macho,Virusi vya Ukimwi,Homa ya ini na maambukizi ya magonjwa ya zinaa,uzalishaji wa dawa ndani ya nchi,malaria, magonjwa yasiyo ambukiza, uuguzi na ukunga, afya ya kinywa, mwelekeo na mkakati wa afya pamoja na wafanyakazi wa sekta ya afya. 

Kauli mbiu ya mwaka huu ya baraza hilo ni “Maliza janga, na jikinge na jingine” 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter