UNICEF Uganda yawarejeshea matumaini ya maisha yatima wawili baada ya mama yao kufa kwa VVU

Watoto katika kituo cha malezi ya awali wilaya ya Isingiro, Uganda.
© UNICEF/Kalungi Kabuye
Watoto katika kituo cha malezi ya awali wilaya ya Isingiro, Uganda.

UNICEF Uganda yawarejeshea matumaini ya maisha yatima wawili baada ya mama yao kufa kwa VVU

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa msaada wa serikali ya Japan limefungua mlango wa maisha mapya kwa watoto yatima waliopoteza matumaini baada ya kifo cha mama yao.  Yatima hao Paul na Florenc,  miaka sita iliyopita waliachwa yatima na bila makazi ya kuaminika na bila chochote mama yao alipofariki dunia kwa ukimwi katika wilaya ya Kabale nchini Uganda lakini leo hii wanasema makazi mapya waliyojengwa na UNICEF ni ukurasa mpya wa maisha yao.

Kabale Uganda Paul ambaye sasa ana umri wa miaka 17 bado anaendelea kuwa kiongozi wa familia ya watu watatu,  yeye na wadogo zake wawili tangu mama yao alipokufa kwa ukimwi mwaka 2015 na baba yao kuitekelekeza familia na kumuachia Paul jukumu la kulea wadogo zake akiwa na umri wa miaka 11 tu. 

Hivi sasa wadogo zake Paul wana umri wa miaka 14 na miaka 9 na wameishi katika kibada cha matope ambacho hakijamalizika kwani mama yao alikuwa badi anakijenga alipoaga dunia. 

Wadogo zake wote wawili ni waathirika wa VVU pia. Alfred Besigensi ni muelimishaji mkuu wa masuala ya afya wilayani Kabale anasema,“Watoto hawa wamekabiliwa na changamoto lukuki , bila shaka za kupata huduma za afya, matibabu , kupata elimu, kupata chakula bora, kwa sababu utakuta hata baadhi ya familia  wakati wazazi wanapokufa wanawaacha watoto bila ardhi ya kutosha , na bila rasilimali yoyote .” 

Mwaka 2019 UNICEF kupitia mradi wa mama-kwa mama nchini Uganda iliamua kuanza kujenga makazi salama kwa familia hii inayoongozwa na mtoto na ujenzi huo umefadhiliwa na kamati ya kitaifa ya Japan kwa ajili ya UNICEF. Wamewajemghea nyumba ya vyumba vitatu , tangi la maji, choo na bafu na inatumia nishati ya sola ili kupunguza gharama. 

Nyumba hiyo imekamilika mwezi huu wa Mei 2021 na baada ya kukabidhiwa wiki iliyopita Paul ameishukuru sana UNICEF akisema kwake ni ndoto iliyofungua ukurasa mpya wa maisha yao,“Sikuwahi hata kufikiria kama ninaweza kuishi kwenye nyumba kama hiyo, mmenisaidia sana. Kwa hakika mmenipa maji tanki liko nje, mmenipa taa za sola, nyumba inakalika asanteni sana.” 

Paul na dada yake Florence wanasaidiwa na mfanyakazi wa ustawi wa jamii kwa ushauri nasaha na masuala ya kijamii. 

kwa sasa wote ni wanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi ya Rwene kwani kifo cha mama yao hakikuwaacha yatima tuu bali kilivuruka kila ndoto yao ikiwemo maendeleo ya kielimu.