Zuia ndoa za utotoni kuokoa maisha ya wasichana :UNICEF

Ndoa za utotono zinasalia kuwa changamoto katika Chad eneo la Sahel.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Ndoa za utotono zinasalia kuwa changamoto katika Chad eneo la Sahel.

Zuia ndoa za utotoni kuokoa maisha ya wasichana :UNICEF

Haki za binadamu

Unaelewa nini unaposikia kutoka kwenye vyombo vya habari au sehemu mbali mbali watu wakisema ndoa za utotoni?, tuungane na Flora Nducha anayetuambia maana yake, hali ilivyo ulimwenguni na nini kifanyike kuzitokomeza.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto UNICEF, ndoa za utotoni ni zile zote zinanofungwa kabla ya wanandoa kufikia umri wa miaka 18, huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Japokuwa sheria zinapinga ndoa hizi, lakini tabia hii mbaya bado inaendelea ulimwenguni kote.

Ndoa hizi za utotoni zinaweza kusababisha matatizo makubwa ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, kunyima haki ya masomo, na kubwa zaidi huleta matesa maishani, hususan kwa wasichana.

Shirika hilo limeongeza kwamba wasichana hawa pale wanapopata mimba, wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua, ikilinganishwa na wale wenye umri wa kuanzia miaka 20 na kuendelea, na hata wakipona, Watoto wao wapo kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua au miezi michache baadae.  

Pia UNICEF imetoa Takwimu ambazo zimegawanyika kwenye makundi manne.

Mosi, Asilimia 21 ya wanawake vijana walikuwa wameolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Hii inamaanisha kuwa, wanawake milioni 650 wameolewa chini ya umri unaotakiwa sawa na wanawake milioni 12 kila mwaka.

Pili, idadi kubwa ya ndoa za utotoni, asilimia 37 zinatokea kusini mwa Jangwa la Sahara na nchi zinazoongoza ni Niger, Jamhuri ya Afrika ya kati CAR, na Chad.

Tatu ni habari njema, ambayo inaonesha tatizo hili linaweza kukabiliwa kwani zaidi ya ndoa milioni 25 ziliweza kuzuiliwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, lakini hapa kuna angalizo, ukanda wa Asia umeanza kupunguza kasi ya kuzuia ndoa hizo. 

Na mwisho ni wito kwa kila mmoja wetu kuzuia ndoa hizo, kwakuwa tusipofanya hivyo, katika miaka 10 ijayo wasichana milioni 110, watakuwa hatarini kufungishwa ndoa wakiwa chini ya miaka 18.