Skip to main content

UNFPA yaongeza watendaji Tigray ili kuimarisha msaada kwa wanawake na wasichana barubaru

Wasichana na wanawake waliofurushwa makwao Tigray wapokea vifaa vya afya ya ulinzi.
UNFPA
Wasichana na wanawake waliofurushwa makwao Tigray wapokea vifaa vya afya ya ulinzi.

UNFPA yaongeza watendaji Tigray ili kuimarisha msaada kwa wanawake na wasichana barubaru

Msaada wa Kibinadamu

Shirika La Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA limeongeza idadi ya watendaji wake kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia kwa lengo la kusaidia mamia ya maelfu ya wanawake na barubaru wa kike kupata huduma za dharura za afya na ulinzi. 

Taarifa ya UNFPA iliyotolewa leo jijini New York, Marekani inasema kuwa hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za raia na vitendo vya ukatili ikiwemo wa kingono tangu kuanza kwa mapigano mwezi Novemba mwaka jana. 

UNFPA inasema ustawi wa wanawake na barubaru wa kike unatishiwa zaidi kutokana na ukosefu wa uhakika wa chakula, kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, na ukosefu wa vituo vya afya vinavyotoa huduma. 

Ni kwa mantiki hiyo watendaji wanaoongezwa huko Tigray watasaidia kuimarisha huduma hizo za kuokoa maisha kwa kuwa hivi sasa zaidi ya watu milioni 3.8 hawana huduma za msingi huku ni asilimia 38 tu ya vituo vya afya ndio vinafanya kazi kwa ukamilifu. 

Kwa upande wa huduma za uzazi, nazo zimekumbwa na mkwamo ambapo huduma za dharura kwa mama na mtoto zinapatikana kwa asilimia 6 pekee jimboni kote Tigray. 

“Wanawake wanajifungua wakiwa safarini, shuleni au msituni kwa msaada wa wasafiri wenzao au jamii inayowapokea. Wanawasili wakiwa hoi bina taaban na wakiwa na afya dhoofu na njaa,” ameesma mratibu wa kituo cha mapokezi cha Mekele alipozungumza na mtendaji wa UNFPA. 

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem amesema, “hali ya wanawake na wasichana barubaru ni mbaya huko Tigray na maeneo ya mpakani kama vile Amhara na Afar. Tunaona viwango vya kutia hofu vya ukatili wa kingono, na maelfu ya wanawake hawana huduma za afya na ulinzi.” 

Kwa mujibu wa UNFPA, hivi sasa zaidi ya wanawake 110,000 ni wajawazito na kila mwezi 10,000 wanajifungua, kati yao hao 5,800 wanaweza kukumbwa na changamoto za uzazi zinazoweza kusababisha kifo iwapo hawatopata huduma zinazotakiwa. 

UNFPA inatoa wito wa kusaidia kulinda haki za usalama na utu wa wanawake na wasichan huko Tigray wakati huu ambapo ukosefu wa usalama unakwamisha watoa misaada kufikia wahitaji.