UNHCR yazindua kampeni ya elimu ya juu kwa wakimbizi vijana 

Vivian Onano, mshauri wa vijana katika ripoti itolewayo kila mwaka ya ufuatiliaji wa elimu duniani, GEMR.
UN News Kiswahili
Vivian Onano, mshauri wa vijana katika ripoti itolewayo kila mwaka ya ufuatiliaji wa elimu duniani, GEMR.

UNHCR yazindua kampeni ya elimu ya juu kwa wakimbizi vijana 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, leo limezindua kampeni ya kusaka kuwezesha wakimbizi vijana wenye vipaji kuweza kuendelea na elimu ya juu. 

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kampeni hiyo imepatiwa  jina, Lenga Juu, ambapo wakimbizi hao viijana watalipiwa gharama za kujiunga na Vyuo Vikuu na taasisi za stadi za kiufundi. 

UNHCR itaendesha kampeni hiyo ya kuchangisha fedha ili kushughulikia mahitaji makubwa ya wakimbizi vijana kwenye elimu, “na kampeni hii inaendana na maadhimisho ya miaka 70 ya UNHCR na mkataba wa kimataifa wa wakimbizi wa mwaka 1951 ambao ndio msingi wa ulinzi wa wakimbizi.” 

Kwa mujibu wa UNHCR, duniain kote, ni asilimia 3 tu ya wakimbizi vijana ndio wamejiandikisha katika baadhi ya Vyuo Vikuu “na hii inashtua sana. UNHCR inalenga kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 15 ifikapo mwaka 2030. Kampeni ya Lenga Juu au Aiming Higher, itachangia kufikia lengo hilo.” 

 Programu ya sasa ya UNHCR ya kugharimia masomo ya elimu ya kati kwa wakimbizi, DAFI ina ukata mkubwa. 

Bajeti ya sasa kwa programu ya Lenga Juu kati yam waka 2021 hadi 2023 ni dola milioni 75 na hadi sasa serikali na watu binafsi wamechangia dola milioni 52 na kuacha pengo la dola milioni 23. 

 “Kampeni hiyo inatoa wito kwa sekta binafsi kuziba pengo hilo la ufadhili na kusaidia kuongeza mtaji huo. Iwapo lengo litafikiwa, dola hizo milioni 75 zitasaidia wakimbizi 1,800 kuingia vyuo vya elimu ya juu na kutimiza lengo la UNHCR la kuwa na wakimbizi vijana 9,200 wamejiandikisha vyuo vya elimu ya juu na wanasoma kwa wakati mmoja ifikapo mwaka 2023,”  imesema taarifa hiyo. 

Akizungumzia mpango huo, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR, Kelly T. Clements amesema, “Kupata elimu ya juu ni jambo la kubadili maisha. Kwa wakimbizi, hiyo inaweza kuwa fursa ya kusimamia maisha yao ya baadaye na kurejesha neema kwa jamii zao. Oja njia bora zaidi ya kuweza kusaidia wakimbzi vijana ni kwa kuwasaidia kupata fursa za aina hiyo na ziweze kupatikana zaidi.”